Dr Alok Ranjan, mtaalamu wa magonjwa ya mfumo wa fahamu na uti wa mgongo kutoka hospitali ya Apollo akiongea na waandish wa habari katika cliniki iliyoanza tarehe 11 na kuendelea mpaka tarehe 13 katika hospitali ya Hindumandal.
Bwana Hafidhi Rashid Waziri, mmoja wa wagonjwa waliofanyiwa upasuaji wa uti wa mgongo na Dr Alok Ranjan katika hospitali ya Apollo Hyderebad akiongea na waandishi wa habari katika Klinik hiyo.
Shamila Idd mama wa mtoto Zulea mwenye tatizo la uti wa mgongo akiongea na waandishi wa habari katika kliniki iliyoandaliwa na Dr Alok Ranjan, mtaalamu wa magonjwa ya mfumo wa fahamu na uti wa mgongo kutoka hospitali ya Apollo.
Na Mwandishi Wetu,
TANZANIA ni moja ya nchi ambazo ina uhaba mkubwa wa madaktari bingwa wa mfumo wa fahamu kitendo kinachosababisha nchi kupoteza fedha nyingi kuwapeleka wagonjwa wa matatizo ya aina hiyo nje ya nchi kupata matibabu na ushauri.
Inakadiriwa kuwa watoto wachanga 1000 kati 4000 wanaozaliwa na tatizo la mfumo wa fahamu hupatiwa matibabu huku wengine 3000 wakishindwa kupatiwa matibabu. Kutokana na hali hiyo, Hospitali ya Apollo ya nchini India imemleta nchini daktari bingwa wa upasuaji wa uti wa mgongo na mfumo wa fahamu ambaye pia ni Mkuu wa idara ya upasuaji wa magonjwa ya fahamu katika hospitali hiyo DK. ALOK RANJAN ambaye atakuwa akitoa huduma na kuwaona wagonjwa wake aliowafanyia upasuaji siku za nyuma.
Kwa upande wao baadhi ya wagonjwa waliofika katika kliniki hiyo inayofanyikia katika hospitali ya Hindu mandal jijini Dar es Salaam wameiomba serikali kuhakikisha kwamba inasaidia katika gharama za matibabu ya watu wanaosafiri nje ya nchi kufuata matibabu ya magonjwa mbali mbali.
Wamezitaka pia kampuni za bima ya afya kuhudumia wateja wake katika hospitali za kimataifa badala ya kujikita katika hospitali za hapa nchini pekee. Katika mkutano huo na waandishi wa habari ulofanyika tarehe 12 katika hospitali ya hindumandali Dk. Alok Ranjan kutoka Hospitali za Apollo amewashauri watanzania kubadilisha mtindo wa maisha ili kuepukana na magonjwa ya mfumo wa fahamu na uti wa mgongo.
Alisema kuwa kwa watu wazima ugonjwa huu mara nying husababishwa na namna mbovu ya ukaaji ambao hudhuru uti wa mgongo, trauma, shinikizo la damu, ajali, kisukari, uzito wa kupitiliza na sababu nyinginezo.
Tanzania kwa sasa inakadiriwa kuwa na madaktari wa mfumo wa fahamu 7 ambao wote kwa sasa ni watendaji katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam.