Na Mpalule Shaaban
KAMPUNI ya Twiga Cement ya jijini Dar es Salaam, jana imefanikiwa kuzindua rasmi Chama cha Wachezaji wa Nafasi ya Golikipa wanaoshiriki ligi kuu ya Tanzania, ambapo katika uzinduzi huo timu hiyo ya Makipa ilicheza mchezo wa Kirafiki dhidi ya Timu ya Kombaini ya Waandishi wa Habari TASWA F.C. uliofanyika kwenye Uwanja wa Bora Kijitonyama jijini Dar es Salaam.
Katika mchezo huo ambao ulikuwa na Ushindani wa Kipekee kutokana na Timu zote kuwa na Wachezaji Nyota na Tegemeo katika Vipaji vyao, Mashabiki waliofika kushuhudia mchezo huo walifurahishwa na jinsi kila mchezaji alivyoonyesha Ujuzi binafsi na kiwango cha hali ya juu.
Timu ya makipa ndiyo iliyokuwa ya kwanza kufanya shambulizi kwenye lango la timu ya TASWA ambapo dakika ya 26 mchezaji Shaaban Kado alikosa Penalt kutokana na beki wa Taswa Martin Peter kunawa akiwa eneo la kumi na nane na penalt hiyo ilidakwa na kipa nyota wa TASWA Ahmed Famau.
Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika kikosi cha timu ya Makipa kilikuwa mbele kwa bao 1-0,lililofungwa na Juma Kaseja baada ya kutokea piga nikupige langoni mwa TASWA, ambapo kipindi cha pili kila timu ilifanya mabadiliko ambapo Taswa iliwatoa, Majuto Omary, Ibrahim Masoud, Ally Mkongwe, Zahoro Mlanzi, Shafii Dauda, na nafasi zao kuchukuliwa na Salum Jaba, Juma Ramadhani, Hatibu Naheka, na Paul Limoy, mabadiliko ambayo hata hivyo yalishindwa kupunguza kasi ya wachezaji hao Makipa wa Ligi kuu waliokuwa muda wote wakilisakama lango la TASWA FC.
Pamoja na kuwa na wachezaji wa akiba timu ya Makipa lakini walishindwa kufanya mabadiliko, kutokana na wachezaji wengi kuwa na pumzi ya kuwamudu TASWA ambapo Makipa hao walisaidiwa na mlinda mlango kutoka timu ya Taifa ya Wanawake Twiga Stars, Fatuma Omary ambaye hata hivyo alionyesha kiwango kikubwa baada ya kudaka michomo ya wazi kutoka kwa washambuliaji wa Taswa, Ibrahim Masoud, Shafii Dauda, Majuto Omary pamoja na Ally Mkongwe waliokuwa wakilisakama Lango la timu ya makipa kila wakati.
Goli la pili lilipatikana kunako dakika ya 67 kupitia kwa Ivo Mapunda aliyefunga kwa shuti kali lililomshinda mlinda wa TASWA Ahmed Famau,kabla ya shaaban Kado kuhitimisha Kapu la Magoli kwa timu hiyo ya Makipa.
Pamoja na Kufungwa kwa Taabu 3-0 timu ya TASWA FC, iliweza kuwachezesha mputa mputa wachezaji hao nyota wa Ligi kuu pamoja na kwamba wachezaji hao muda mwingi wanakuwa kwenye Mazoezi Makali na Timu zao za ligi kuu ya Vodacom Tanzania Bara,kitendo ambacho kiliwafanya kuonekana wakiwa na Uhai wa kukimbiza huku na kule katika kipindi cha dakika zote za mchezo.
Taswa ambayo kwa asilimia kubwa iliwachezesha wachezaji wake wengi ambao ni wafanyakazi wa vyombo mbali mbali vya habari, ilisifiwa na mashabiki waliohudhulia mchezo huo kwa kuwa Muda mwingi wanakuwa katika shuguli za kiofisi ambapo kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Timu hiyo wachezaji ukutana mara moja kwa wiki kwa ajili ya mazoezi ya Pamoja.
“Timu yetu ni nzuri sana hii TASWA, mwenyewe umeona wachezaji walivyowapeleka mpuata hawa Makipa pamoja na kwamba hii timu ya Makipa ni Wachezaji wa ligi kuu, nasema ligi kuu kwa kuwa wanashiriki hiyo ligi isipokuwa tofauti wao ni makipa, na tunapozungumzia suala la Wachezaji, mwenyewe unajua timu ili iwe bora ni lazima kwanza iwe na Makipa wazuri ndipo iwe bora, na kipa bora ni yule anayeweza kuwapanga wachezaji wake, hivyo kama hawa wachezaji ndiyo wapangaji wa timu zao wakati wa Mashindano, mimi nasema tumecheza na Timu ya Taifa na si kama unavyofikili wewe, na ndiyo maana nathubutu kusema kuwa kufungwa kwetu mabao 3-0 ni sawa na kupata ushindi sisi, maana hata hivyo wametuleta kwenye Uwanja wao, nadhani wakati wa mchezo wa Marudiano bila shaka itakuwa zamu yetu kuibuka na ushindi maana leo wameshinda wao na mpira ni mchezo wa mmoja kushinda, asiyekubali kushindwa siyo mshindani” alisema Majuto.
Aliongeza kwamba mchezo huo kwa pande zote mbili umewapa changamoto ya kuifanya sasa timu hiyo ya Kombaini ya Makipa kutambuliwa kote Nchini. “Mkakati uliopo sasa ni kuhakikisha kwamba timu hii inazunguka kwenye Majiji Makuu kwa ajili ya kufanya michezo yake ya kirafiki na timu za Mikoa, lakini lengo kubwa ikiwa ni kuwapa Fursa wakazi wa Maeneo hayo kuwatambua zaidi hawa Makipa wetu, lakini pia wakati wachezaji hawa wakiwa kwenye hayo maeneo ya Majiji watakuwa na jukumu la kuwaandaa wachezaji wengine zaidi vijana katika nafasi za kipa ili kuweza kuwa na Makipa wengi zaidi kwa ajili ya Faida ya Taifa letu la Tanzania,” alisema Majuto
Naye kocha wa Taswa FC Ally Mkongwe wakati akizungumza na wachezaji wa timu zote alisema kuwa ni jambo la kufurahisha ambalo limeweza kufanikiwa kwa asilimia 100 kwa kuwa lengo ilikuwa ni kufanya uzinduzi na timu zote zimeweza kucheza kwa hali kubwa bila vurugu wala kuonyeshana mchezo mbaya.
“Tumefurahi sana, niwapongeze wachezaji wote yaani Makipa na Taswa, jambo hili si la mzaha kama tulivyofikili hapo mwanzo, lakini kumbe mwitikio wa watazamaji ulikuwa ni mkubwa sana na wengi wamekuja kuwatazama wachezaji na Waandishi wa habari, Watangazaji, na wakati umefika tukae tuangalie namna ya kuboresha mahusiano haya yawe ya kudumu baina ya TASWA na timu hii ya Kombaini ya Makipa wa Ligi kuu, isipokuwa tusameheane kwa yale Mapungufu madogo yaliyotokea maana sisi ni binadamu lakini wakati mwingine nadhani hayatatokea kwa pande zote mbili endapo yametokea kwa mchezo wa leo,” alisema Mkongwe.
Hata hivyo wachezaji hao Makipa wametakiwa kufanya jitihada za kuhakikisha wanakuwa chachu ya kuleta Makipa wengine nyuma yao kutokana na kwamba nafasi ya Makipa kwa Tanzania inazidi kupungua kutokana na nafasi hiyo kuwa ngumu ukilinganisha na nafasi za wachezaji wengine wa ndani ambao wanakuwa ni wengi.
Naye mmoja wa Makocha wasaidizi wa timu ya TASWA Ibrahim Masoud aliwaasa wachezaji hao kuwa kioo kwa wenzao na kuwa kishawishi cha kuwapata vijana wengine watakaokuwa makipa wa Tanzania miaka ijayo”Sina Mengi ya Kusema kwa kuwa Kocha na Mwenyekiti wameeleza kwa kirefu lakini mimi niko tofauti kidogo na wenzangu, kikubwa hapa mimi ni kuhusu nyie Makipa wetu, kumbukeni kwamba nyinyi kina Kaseja, Ivo Mapunda, Shaaban Kado, Dida, mstafa na nyinyi wote, nyie sasa mnaelekea Ukingoni, ni kama kina Mwameja wakati wao, kina Manyika, Mfaume, nk, walikuwapo lakini walipopotea hao makipa Tanzania iliyumba sana kuwapata nyinyi, na hiyo inatokana na kwamba Wachezaji wengi Makipa hawapati Fursa ya kuandaliwa, na niwatake sasa kutumia mwanya huu kwa kuwa tayari mmekuwa ni makipa Hodari kuhakikisha kwamba wakati wa Mapumziko ya Ligi, muweze kuingia Darasani kwa ajili ya kupata ujuzi wa kuwa Walimu wa Makipa, Kila mmoja kwa wakati wake lengo mtakapomaliza muda wenu wa kuitumia Tanzania katika Soka, muweze kuwa walimu wazuri na wazalishaji wazuri wa Makipa wengine,” alisema Ibrahim Masoud (Maestro)
Kwa Upande wao Makipa hao wao hawakuwa na la kusema isipokuwa kwa niaba ya wachezaji wote wa Makipa Ivo Mapunda alisema kuwa wanashukuru kwa Sapoti kubwa kutoka Chama cha TASWA, ambao mara zote wamekuwa mstari wa mbele kuwapa maelekezo, kitendo kilichowaweka karibu zaidi hata wakati wa Uzinduzi wa Chama hicho cha Magolikipa,” Sisi binafsi tumefurahi kukutana na timu hii ya TASWA, maana kiujumla wachezaji wengi wa Taswa wanafahamu mpira, ila tumewafunga kutokana na kukosa Pumzi tofauti na sisi wengi tunafanya mazoezi kila siku na timu zetu tena timu kubwa za ligi kuu, mimi Kesho (Leo) naelekea Zazibar Kambini, kujiunga na Timu yangu, kwa hiyo unaona jinsi mchezo huu ulivyokuwa ni muhimu sana kwetu hata nimeshindwa kuongozana na wachezaji wazangu pamoja na Mwalimu wangu kutaka nisicheze hii leo lakini nimemkatalia kwamba ni lazima nijumuike na Makipa wenzangu kwenye jambo hili la Umoja, maana sasa sisi Makipa pia tumekuwa ndugu wa karibu na Marafiki wa Kweli, zama za kale kwamba huyu na huyu aziivi eti kwa kuwa wote ni Makipa imepitwa na wakati, utatukuta mimi, Kaseja, Kado, Dida, Mstafa, na wengine tukizungumza na kufurahi pamoja, sisi siyo maaduni ni marafiki.
Niwapongeze Wadhamini wa Mpambano huu (Uzinduzi) Kampuni ya TWIGA CEMENT kwa kufanya jambo hili, limezidi kutuweka karibu zaidi, na naamini kwamba watazidi kutuunganisha na kuandaa michezo Mingi zaidi kwa ajili ya kuwapa Raha wakazi na mashabiki wetu Mikoani” alisema Ivo Mapunda.
Akizungumzia mchezo huo Afisa Masoko wa TWIGA CEMENT,Alex Gideon, alisema kuwa maandalizi yamekwenda kama walivyopanga isipokuwa mkanganyiko umetokea kwenye eneo dogo la Uwanja, ambapo awali mchezo huo ilikuwa ufanyike kwenye uwanja wa KARUME kwa mujibu wa Matangazo yaliyofanywa na vyombo vya habari.
” sitaki kulizungumzia sana suala la mkanganyiko wa Uwanja, lakini nadhani TFF katika hatua za mwisho imeshindwa kuruhusu mchezo wetu kufanyika kwenye viwanja vyao ambako vyombo mbali mbali vilitangaza, hivyo mashabiki wengi walifika Karume, na nichukue fulsa hii kuwataka radhi sana wote waliotufuata kwenye viwanja vya Karume, mchezo wetu ulibadilishwa uwanja kutokana na sababu zilizokuwa nje ya uwezo wetu na kwa kuwa ni TFF wenyewe waliopanga hatua za Mwisho Mchezo wa Ligi daraja la kwanza kufanyika humo hatukuwa na kipingamizi, ni jambo la kimchezo na ukizingatia ni ligi yetu pia sisi watanzania hivyo hilo niombe radhi kwa mashabiki wetu wote, lakini kuhusu wadhamini wetu kama ulivyoona mwenyewe wamejitaidi na huu ni mwanzo na maandalizi yamefanyika kwa siku chache zana, wakati ujao tutaboresha na kulifanya jambo hili kuwa la kudumu na lenye kuleta tija ya Maendeleo kwa hawa Makipa wetu, kingine niwapongeze TASWA kwa ushirikiano wao maana wametufariji na kutupa sapoti kubwa,” alisema Alex Gideon.
Aidha mchezo huo ulikuwa kwa ajili ya kujenga mahusiano mema baina ya timu zote, wachezaji pamoja na kufanya Uzinduzi wa Chama cha Makipa Tanzania, waandishi na Makipa wanaocheza ligi kuu Ya Vodacom Tanzania.