Magari ya Jeshi kutumika kubeba mahindi Tanzania

Gari la Jeshi la Kujenga Taifa ( JKT) Kambi ya Chita, iliyopo Tarafa ya Mngeta, Wilaya ya Kilombero likiwa kwenye harakati ya kupita eneo Kijiji cha Kisegese.

Na Mwandishi Wetu

WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amesema Serikali imefikia uamuzi wa kutumia majeshi yake ili kusomba mahindi yaliyolundikana katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini na kuyapeleka katika mikoa yenye upungufu mkubwa wa chakula.

Amesema uamuzi huo umechukuliwa baada ya kubaini kuwa kasi ya kusafirisha mahindi kwa njia ya reli peke yake ni ndogo na haikidhi mahitaji yaliyoko katika mikoa ya Shinyanga na maeneo mengine ya Kaskazini.

Ametoa kauli hiyo jana Novemba 29, 2011 wakati akizungumza na wakazi wa mikoa ya Rukwa, Ruvuma na mkoa tarajiwa wa Katavi katika chakula cha jioni ambacho aliwaandalia kwenye makazi ya Waziri Mkuu, Oysterbay jijini Dar es Salaam.

Wakazi hao zaidi ya 100 walikuwa wamealikwa kuja jijini Dar es Salaam kushiriki tamasha la Utamaduni la mikoa ya Rukwa na mkoa tarajiwa wa Katavi ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara. Tamasha hilo lilifanyika Novemba 25-27, 2011, katika kijiji cha Makumbusho jijini Dar es Salaam.

“Tunatarajia ifikapo wiki ijayo tutakuwa tumemaliza kulipa madeni ya watu waliouza mazao yao… tunadaiwa kiasi cha sh. bilioni 13.6/-. Tukimaliza kulipa madeni, tumeamua tuwape jeshi kazi ya kusomba mahindi ili yaondoke haraka na yale waliyovuna wakulima yapate mahali pa kuhifadhiwa,” alisema.

Alisema Serikali imekwishapata mkopo sh. bilioni 20 kutoka kwenye mabenki na kwamba fedha hizo ndizo zitatumika kulipa madeni inayodaiwa na wakulima waliouza mahindi yanayohifadhiwa na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) katika vituo vya Makambako, Songea na Sumbawanga.

Kati ya tani 114,117 za mahindi ambazo zimepokelewa katika vituo vya ununuzi, NFRA imeweza kulipia tani 80,615 tu na kushindwa kulipia tani 33,502 zilizopokelewa kutokana na ufinyu wa bajeti.

Alisema ili kukabiliana na tatizo la mlundikano wa mazao katika maghala ya kuhifadhia mazao, wamekubaliana na Rais Jakaya Kikwete kwamba mwakani Serikali itaruhusu mapema sekta binafsi inunue mazao kutoka kwa wakulima ili kuwe na soko la uhakika kwa wakulima.

“Tutaweka bei ya gunia iwe sh. 38,000/- na tani moja iuzwe kwa sh. 380,000/- … Bei inaweza kupanda lakini haipaswi kuwa chini ya hapo ili wanunuzi wasiwalalie wakulima. Tulichoamua ni kwamba wanunuzi waingie mkataba na Mkuu wa Mkoa ili kuwe na ufuatiliaji wa karibu,” alisema huku akishangiliwa.

Alisema utaratibu huo utaanza mapema ili tatizo la mlundikano wa mazao lililojitokeza mwaka huu lisiweze kujirudia. Alisema ameamua kutoa ujumbe huo kwao kwa vile wanaiwakilisha mikoa ya Rukwa, Ruvuma na mkoa tarajiwa wa Katavi lakini hali ni hiyo hiyo hata akienda Iringa au Mbeya.