Na Ngusekela David
MRADI wa Muungano wa Wajasiriamali Vijijini (MUVI) unaendesha mafunzo ya kilimo kama biashara wilayani Muheza yanayotolewa na wakufunzi ambao ni maofisa ugani wa kata na vijiji katika Wilaya za Muheza, Korogwe na Handeni.
Mafunzo hayo yanaratibiwa na mradi wa MUVI na yanahusisha kilimo cha alizeti na machungwa kwa Wilaya zote ambazo mradi wa MUVI unafanya kazi. Lengo la mafunzo hayo ni kuwaandaa wakufunzi ili waweze kuwafundisha wakulima mbinu mbalimbali za kilimo bora ikiwa ni pamoja na kuendesha kilimo cha kibiashara.
Akizungumza katika mafunzo hayo, Mkufunzi wa Mafunzo, Jimmy Ebong amesema mkulima anaweza kufanya kilimo kuwa chenye tija endapo atakua na tabia ya kujiwekea kumbukumbu.
“Kuweka kumbukumbu ndio njia pekee itakayomsaidia mkulima kujua kama anazalisha kwa faida au hasara,” alisema.
Akifafanua zaidi, Ebong amesema, iwapo mkulima atakuwa na kumbukumbu ni rahisi kujua amezalisha kwa gharama kiasi gani hivyo anaweza kujipangia bei yeye mwenyewe badala ya kuwasubiri madalali na hata akiuza kwa madalali kwa bei aliyopanga mwenyewe bado atauza kwa faida.
Mafunzo hayo yamedhaminiwa na mradi wa MUVI mkoani Tanga na yanaendeshwa na Match Maker Associates na kusimamiwa na SIDO. Mada kuu katika mafunzo hayo ni namna ya kutunza kumbukumbu, faida na hasara za mikopo, akiba, matumizi ya mbegu bora na makadirio ya mapato.