Mafunzo kwa ajili ya mfumo wa uhamisho wa wachezaji (Transfer Matching System-TMS) na usajili wa wachezaji kwa klabu za Ligi Kuu ya Vodacom yatafanyika kwa siku tatu kuanzia Juni 27 hadi 29 mwaka huu.
Washiriki wa mafunzo hayo yatakayofanyika makao makuu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ni makatibu wakuu na mameneja wa TMS (TMS Managers) wa klabu hizo.
HATUA YA 16 BORA COPA COCA COLA
Hatua ya 16 bora ya michuano ya Copa Coca Cola 2011 itafanyika Juni 24 na 25 mwaka huu kwenye viwanja vya Kumbukumbu ya Karume na Tanganyika Packers ulioko Kawe.
Mechi hiyo zitachezwa saa 2.30 asubuhi na saa 10 kamili jioni. Juni 24 mwaka huu itakuwa ni Kinondoni na Pwani (Karume- asubuhi), Kilimanjaro na Rukwa (Kawe- asubuhi), Temeke na Mara (Karume- jioni), Shinyanga na Arusha (Kawe- jioni).
Juni 25 mwaka huu ni Kigoma na Dodoma (Karume- asubuhi), Tanga na Mbeya (Kawe- asubuhi), Mjini Magharibi na Ruvuma (Karume- jioni) na Morogoro na Ilala (Kawe- jioni). Robo fainali itachezwa Juni 26 na 27 mwaka huu Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume.
UCHAGUZI WA COASTAL UNION
Kamati ya Uchaguzi ya TFF katika kikao chake kilichofanyika Juni 22 mwaka huu kilipitia fomu za wagombea uongozi wa klabu ya Coastal Union ya Tanga. Kamati ilibaini wagombea Yakubu Nuru Athumani, Titus Munthali Bandawe na Steven Mnguto kutotimiza masharti ya uombaji wa uongozi wa klabu hiyo, hivyo kuwaondoa katika orodha ya wagombea.
Uchaguzi wa Coastal Union utafanyika Julai 2 mwaka huu kwa nafasi ya Mwenyekiti na wajumbe wa Kamati ya Utendaji. Nafasi ya Makamu Mwenyekiti haina mgombea na itajazwa baadaye kwa mujibu wa Katiba ya Coastal Union Ibara ya 29(3).
Boniface Wambura
Ofisa Habari