Maelfu ya raia wa India wamejitokeza mitaani kumunga mkono mwanaharakati wa kupinga ufisadi Anna Hazare wakiwa na mabango yaliyoikemea na kuishinikiza Serikali imwachie huru.
Mwanaharakati huyo,Bw Hazare anashinikiza kufanyika kwa mageuzi katika sheria za kupambana na rushwa na amepanga kuanza kukesha bila kula ili kushinikiza hilo lifanyike.
Mwanaharakati huyo mwenye miaka 74, anapinga mswada uliowasilishwa bungeni kwa kuwa waziri mkuu na majaji hawata chunguzwa.
Hata hivyo Waziri Mkuu wa India Manmohan Singh amemkosoa mwanaharakati huyo akisema, ingawa nia yake ni nzuri anatumia dhana potufu kulazimisha bunge lifuate matakwa yake.
Bw Hazare amegoma kuondoka katika jela hilo hadi serikali ya India itakapo mruhusu kutekeleza mpango wake kwa kususia kula chakula hadharani.
Awali wafuasi wa Bw Hazare walikusanyika nje ya jela mmoja mjini Delhi ambako amekuwa akizuiliwa tangu jumanne.
Maelfu ya watu nchini India wamekerwa na viwango vya ufisadi na kuamua kuunga mkono ambapo Bw Hazare na wafuasi wake 1,200 walitiwa nguvuni na polisi wakiwa kwenye bustani ya JP park saa chache kabla hawajaanza kususia chakula.
Raia hao wa India wanasema lazima serikali ichukue hatua za kukabili ufisadi uliokithiri nchini humo.
Mshirika wa karibu wa Bw Hazare amesema kuwa sasa amekubali kuondoka jela baada ya polisi kuridhia kuwa anaweza kufanya mgomo huo wa kususia chakula kwa siku kumi na tano kwenye bustani mmoja mjini Delhi.
Mwezi April, Bw Hazare alivunja mgomo wake wa kususia chakula baada ya siku nne pale serikali ilikubali kuwa anaweza kuhusika kuandaa mswada wa kupambana na ufisadi nchini humo ambapo kutakuwa ofisi maalum ya kuchunguza wanasiasa na watumishi wa serikali wanashukiwa kuhusika na ufisadi.
-BBC