MAELEZO YA MHESHIMIWA MIZENGO P. PINDA (MB), WAZIRI MKUU, WAKATI AKIJIBU HOJA ZA WABUNGE KUHUSU HOTUBA YA BAJETI YA OFISI YA WAZIRI MKUU NA TAASISI ZAKE KWA MWAKA WA FEDHA 2013/2014
UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika,
• Niruhusu nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa Afya njema hadi leo ninapohitimisha Majadiliano ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu; Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa; Taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2013/2014.
Mheshimiwa Spika,
• Katika mjadala huu, jumla ya Waheshimiwa Wabunge 217 Walichangia. Waheshimiwa Wabunge 119 waliochangia kwa kuzungumza moja kwa moja hapa Bungeni na Waheshimiwa Wabunge 98 wamechangia kwa njia ya maandishi.
• Kama ilivyo miaka yote Idadi ya Wachangiaji ni kubwa. Hii inaonesha dhahiri jinsi ambavyo Waheshimiwa Wabunge mnavyoweka umuhimu katika majukumu yanayotekelezwa na Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zilizo chini yake.
• Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri wamejitahidi kujibu hoja mbalimbali lakini bado zimebaki nyingi. Kama ilivyo ada tutajitahidi kujibu hoja zilizosalia kwa njia ya maandishi.
MAJIBU YA HOJA
Mheshimiwa Spika,
• Kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge, Kanuni ya 99(9) inayohusu kujadili Bajeti ya Wizara, nichukue nafasi hii sasa kujibu na kufafanua baadhi ya hoja zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge kama ifuatavyo.
VIPAUMBELE VYA SERIKALI VYA MPANGO WA MAENDELEO WA MIAKA 15 NA MIAKA MITANO
Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani, Mheshimiwa Freeman A. Mbowe (Mb.) anasema kuwa:
“Tatizo kubwa la Serikali inayoongozwa na CCM ni kukosa Weledi wa kutekeleza kikamilifu Vipaumbele vyake pamoja na kuviainisha kupitia Mpango wake wa Miaka Mitano, Bajeti na Programu”
JIBU:
Mheshimiwa Spika,
• Serikali ilikwishaandaa Mpango Elekezi wa Maendeleo wa Miaka 15 wa kutekeleza Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025 ambao umegawanyika katika vipindi vya miaka Mitano Mitano.
• Mpango wa kwanza wa Maendeleo wa Miaka Mitano kuanzia mwaka 2011/2012 hadi 2015/2016 uliokuwa na Vipaumbele vya kufungulia fursa za ukuaji wa Uchumi wa Tanzania ulijadiliwa hapa Bungeni mwaka 2011/2012 na tukapata maoni ya Wabunge ambayo tuliyazingatia yakawa sehemu ya Mpango huo.
• Ndani ya Mpango Elekezi wa Miaka 15, tulikubaliana kuanza kutekeleza Mpango wa kwa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/2012 – 2015/2016) ambao ndio tunaoendelea nao hivi sasa.
• Katika Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano na ule wa Miaka 15, Vipaumbele vya Msingi vimefafanuliwa waziwazi na ambavyo ni vifuatavyo:
i) Miundombinu hasa uwekezaji mkubwa katika miundombinu ya Nishati, Usafirishaji, TEHAMA, Maji Safi na Majitaka na Umwagiliaji;
ii) Kilimo kwa shabaha ya kuleta Mapinduzi ya Kilimo kwa tafsiri pana inayojumuisha Kilimo Mazao, Mifugo, Uvuvi, Misitu na Ufugaji Nyuki;
iii) Maendeleo ya Viwanda hasa vile vinavyotumia malighafi zinazopatikana hapa Nchini, Viwanda vinavyoongeza thamani ya Mazao, Madini pamoja na kujenga Viwanda vikubwa vya Mbolea, Saruji, Viwanda vya Kielektroniki na vinavyohusiana na TEHAMA pamoja na vile vya maeneo maalum ya kiuchumi kwa ajili ya kutengeneza bidhaa za Soko la Ndani, Kikanda na Kimataifa;
iv) Maendeleo ya Rasilimali Watu na ujuzi kwa kutilia mkazo maendeleo ya Sayansi, Teknolojia na ubunifu pamoja na kuimarisha mafanikio yaliyopatikana katika upatikanaji wa huduma za Jamii (Elimu, Afya na Maji);
• Maeneo haya ya Vipaumbele vya Kimkakati ndiyo tuliyokubaliana ili kuleta matokeo ya haraka katika ukuaji wa uchumi na kwa namna ambayo ni shirikishi ya kujumuisha Sekta Binafsi na Wadau wengine.
• Katika Hotuba yangu, nimeeleza kuwa Vipaumbele vya Mpango wa Maendeleo ya Miaka Mitano ndivyo vinavyotuongoza. Hata hivyo hii haina maana kuwa maeneo mengine yanapuuzwa, bali hii ni katika kuhakikisha tunafikia malengo tuliyojiwekea ya Kukuza Uchumi na Kuondoa Umaskini kwa haraka.
• Hivyo inashangaza, msemaji Mkuu wa Upinzani Mheshimiwa Freeman Mbowe (Mb.) kwa niaba ya CHADEMA anadiriki kusema Serikali haina Weledi. Hivi tusingekuwa na Weledi tungekuwa hapa.
• Tumeshuhudia Mataifa Makubwa yanatupongeza kwa jinsi tunavyosukuma maendeleo yetu. Inashangaza kwamba sisi wenyewe Watanzania hususan Viongozi wa baadhi ya Vyama vya Siasa hatuoni hivyo.
• Kwa kifupi nitoe mifano michache.
(a) VIASHIRIA VYA UCHUMI JUMLA
– Uchumi umeendelea kukua kwa kasi ya kuridhisha ambapo kwa mwaka 2012 ulikua kwa Asilimia 6.9;
– Bajeti ya Serikali imeendelea kuongezeka kutoka Shilingi Trilioni 4.2 mwaka 2005/2006 hadi Shilingi Trilioni 16.7 mwaka 2013/2014;
– Makusanyo ya Kodi yameongezeka kutoka Wastani wa Shilingi Bilioni 117 kwa mwezi mwaka 2005/2006 hadi Wastani wa Shilingi Bilioni 680 kwa mwezi mwaka 2012.
(b) MIUNDOMBINU (Barabara, Reli, Bandari, Viwanja vya Ndege na Mawasiliano)
BARABARA
Mheshimiwa Spika,
• Hadi kufikia mwaka 2000, kulikuwa na barabara kuu za lami zenye urefu wa Kilometa 3,904 tu Nchini. Serikali ya Awamu ya Tatu, ilianzisha Miradi 14 ya ujenzi wa barabara zenye urefu wa jumla ya Kilometa 1,226. Kati ya Miradi hiyo, Miradi saba (7) ya barabara zenye urefu wa Kilomita 403 ilikamilika katika kipindi cha Awamu ya Tatu kufikia mwezi Desemba 2005. Hivyo, Serikali ya Awamu ya Nne ilipoingia madarakani ilirithi Miradi saba (7) iliyokuwa bado kukamilika yenye urefu wa jumla ya Kilometa 823 na kuikamilisha.
• Pia Serikali ya Awamu ya Nne ilianzisha Miradi mipya 26 ya ujenzi wa Barabara zenye urefu wa Kilometa 1759.6. Kati ya Miradi hiyo, jumla ya Kilometa 1270.8 sawa na Asilimia 72 zimekamilika kwa kiwango cha lami kufikia mwezi Machi 2013. Kwa Miradi ya barabara zenye urefu Kilometa 488.8 zilizobaki, inaendelea kutekelezwa katika hatua mbalimbali. Hivyo, Serikali ya Awamu ya Nne (4) imejenga barabara kuu mpya zenye urefu wa Kilometa 2093.8 katika kipindi cha miaka saba iliyopita.
• Sambamba na ujenzi wa barabara mpya, Serikali pia imeendelea kufanya ukarabati mkubwa wa barabara kuu za lami. Kati ya mwaka 2006 na 2013, Serikali ya Awamu ya Nne imetekeleza Miradi 10 ya ukarabati mkubwa wa barabara kuu za lami zenye urefu wa jumla ya Kilometa 841.2. Kati ya hizo jumla ya Kilometa 650, sawa na Asilimia 77 zimekamilika. Serikali inaendelea kukamilisha Miradi ya barabara zenye urefu wa Kilometa 191.2 zilizobakia kabla ya mwisho wa mwaka huu.
• Vilevile, pamoja na ujenzi unaoendelea katika Miradi hiyo, kuna Miradi mingine 43 iliyobuniwa katika Awamu ya Nne yenye urefu wa jumla ya Kilometa 5,739 ambayo inaandaliwa kwa ajili ya kuanza ujenzi. Kati ya Miradi hiyo, Miradi 16 yenye urefu wa jumla ya Kilometa 3,817, ipo katika hatua mbalimbali za kukamilishwa Usanifu, na Miradi 27 yenye urefu wa jumla ya Kilometa 1,921 usanifu wake umekamilika na inatafutiwa Makandarasi. Lengo ni kuunganisha kwa awamu Miji Mikuu ya Mikoa yote Nchini kwa barabara za lami ifikapo mwaka 2017/2018.
Mheshimiwa Spika,
• Maendeleo ya ujenzi wa barabara yamepunguza kwa kiasi kikubwa kero iliyokuwepo ya usafiri wa Barabara Nchini. Sambamba na hatua hizo za ujenzi wa barabara mpya kwa kiwango cha lami, Serikali ya Awamu ya Nne imeendelea kuzingatia umuhimu wa kuimarisha mtandao wa barabara zote Nchini kwa kufanya matengenezo kwa viwango vinavyotakiwa kwa kuongeza Bajeti ya Matengenezo ya Barabara kupitia Mfuko wa Barabara.
• Mfuko huo uliimarishwa kwa kuuongezea fedha kwa asilimia 155 kutoka Shilingi Bilioni 85.74 mwaka 2006/07 hadi Shilingi Bilioni 218.47 mwaka 2007/08 na kiwango cha fedha cha Mfuko kimeendelea kuwa cha wastani huo kila mwaka hadi sasa. Pamoja na mafanikio hayo, Serikali inakusudia kuongeza fedha za Mfuko wa Barabara ili kufidia pengo lililopo hivi sasa la mahitaji ya Shilingi Bilioni 435 kwa mwaka kwa ajili ya Matengenezo ya Mtandao wa Barabara Nchini, kutoka kwenye wastani Shilingi Bilioni 222 kwa mwaka zinazotolewa hivi sasa.
UJENZI WA MADARAJA
Mheshimiwa Spika,
• Sambamba na ujenzi wa barabara za lami, Serikali imetilia mkazo ujenzi wa madaraja ambayo kutokuwepo kwake, imekuwa kero ya muda mrefu kwa Wananchi wa maeneo husika. Kati ya mwaka 2006 na 2013 Serikali ya Awamu ya Nne imetekeleza miradi mingi ya ujenzi wa madaraja makubwa na madogo. Baadhi ya madaraja makubwa yaliyokamilika na yanayoendelea kujengwa ni pamoja na: Daraja la Umoja na Madaraja ya Nangoo na Nanganga (Mtwara); Daraja la Ruvu (Pwani); Daraja la Mwatisi (Morogoro); Daraja la Ruhekei (Ruvuma); Daraja la Sibiti (Singida); Daraja la Mbutu (Tabora); Daraja la Malagarasi (Kigoma); Daraja la Kigamboni (Dar es Salaam); Daraja la Kilombero (Morogoro) na Daraja la Kimataifa la Rusumo (Kagera) linalounganisha Tanzania na Rwanda.
UJENZI WA VIVUKO VIPYA
Mheshimiwa Spika,
• Vivuko vipya 10 vimejengwa na Serikali ya Awamu ya Nne kati ya mwaka 2006 na 2013 kwa ajili ya kuvusha Wananchi na mizigo yao kwenye Mito, Maziwa na Bahari. Vivuko hivyo ni vifuatavyo: Mv. Kilombero (Morogoro); Mv. Ruhuhu (Ruvuma); Mv. Misungwi (Mwanza); Mv. Magogoni (Dar es Salaam); Mv. Kome (Mwanza); Mv. Pangani ( Tanga); Mv. Utete (Pwani); Mv. Ruvuvu (Kagera), Mv. Ujenzi (Musoma) na Mv. Kalambo (Mtwara).
USAFIRI WA RELI
Mheshimiwa Spika,
• Katika Dira ya Maendeleo ya Taifa kufikia mwaka 2025 na katika Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano 2010/2011 hadi 2014/2015, suala la uwekezaji wa kutosha kwenye Miundombinu ya Reli Nchini limepewa kipaumbele.
Kuimarisha Reli ya Kati
Mheshimiwa Spika,
• Mnamo mwezi Machi 2010, Serikali iliamua kuchukua Hisa Asilimia 51 zilizokuwa zinamilikiwa na Kampuni ya RITES katika TRL hivyo kuiwezesha Serikali kuchukua jukumu la kuendesha Kampuni hiyo. Aidha, ili kuimarisha usafiri katika Mtandao wa Reli unaohudumiwa na TRL, Serikali ilitenga jumla ya Shilingi Bilioni 101 katika mwaka 2011/2012 na imetenga Shilingi Bilioni 135 katika mwaka 2012/2013 kwa ajili ya kununua injini za treni na mabehewa (Rolling Stock).
• Katika kuimarisha Njia ya Reli ya Kati, Serikali ilikarabati njia ya Reli, kati ya Kilosa na Gulwe iliyoharibiwa na Mafuriko kwa gharama ya Shilingi Bilioni 26.36 kati ya mwaka 2009 na 2012. Aidha, Serikali ilitumia Mkopo wa Dola za Marekani Milioni 33 kununulia Sleepers, mataruma ya Reli na vifaa vya kufungia na hivyo kuwezesha kuanza kwa kazi ya kubadilisha Reli zenye uzito mdogo wa Ratili 45 kwa yadi hadi Ratili 80 kwa yadi kati ya Kitaraka na Mlongwe (km 89). Kazi hii ilianza mwezi Septemba 2012 na itakamilika ifikapo mwezi Septemba 2013. Kazi ya kubadilisha njia ya Reli kutoka Igalula hadi Tabora (km 32) itaendelea katika mwaka 2013/2014.
Ujenzi wa Reli Mpya ya Kati
Mheshimiwa Spika,
• Serikali ya Tanzania imeingia makubaliano na Serikali za Rwanda na Burundi ya kutekeleza Mradi mkubwa wa ujenzi wa Reli Mpya yenye urefu wa Kilometa 1,661 kutoka Dar es Salaam – Isaka – Keza – Kigali hadi Musongati (Burundi). Upembuzi yakinifu wa Mradi huu ulikamilika mwaka 2009 na usanifu wa kina wa Mradi huu ulianza mwaka 2011/2012.
Reli ya TAZARA
Mheshimiwa Spika,
• Serikali za Tanzania na Zambia zimepata mkopo wa Dola za Marekani Milioni 39.9 kutoka Serikali ya China kwa ajili ya kuboresha Njia ya Reli kwa ukarabati pamoja na ununuzi wa Injini na Mabehewa katika Reli ya TAZARA.
Mipango ya Ujenzi wa Reli Mpya
i) Ujenzi wa Reli Mpya ya Tanga – Arusha – Musoma – Kampala
• Serikali imeanza kufanya upembuzi Yakinifu kwa ajili ya kuboresha Reli ya Tanga hadi Arusha kuanzia mwaka 2011/2012. Lengo ni kuimarisha Reli hiyo ili iweze kuunganishwa na Reli Mpya iliyopangwa kujengwa kati ya Arusha – Musoma hadi Kampala. Mkataba wa Makubaliano kuhusu ujenzi wa Reli hii ulitiwa mwezi Juni 2011 kati ya Serikali ya Tanzania na Uganda. Mradi huu utajumuisha pia ujenzi wa Bandari za Tanga, Musoma na Bandari iliyopo upande wa Uganda.
ii) Ujenzi wa Reli ya Ukanda wa Mtwara
• Serikali imekamilisha kazi ya Upembuzi yakinifu wa Reli Mpya itakayotoka Bandari ya Mtwara hadi Mchuchuma na Liganga. Kazi hii imegharimiwa na Shirika la Maendeleo la Japan (JICA) na hivi sasa Serikali inamtafuta mwekezaji kwa ajili ya ujenzi wa Reli hii.
USAFIRI WA MAJINI NA UIMARISHAJI WA BANDARI
Bandari Mpya ya Bagamoyo
Mheshimiwa Spika,
• Upembuzi yakinifu kuhusu upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam umebaini kuwa ili kujenga Bandari itakayokuwa Kitovu (Hub) kwa ajili ya kuhudumia Nchi Jirani, bandari kubwa ya kisasa itapaswa kujengwa katika eneo la Mbegani, Bagamoyo ambapo Hekta 2,518 zimetengwa. Upembuzi yakinifu wa Bandari Mpya ya Bagamoyo ulikamilika mwezi Julai 2010. Aidha, tayari Serikali ya Tanzania na Serikali ya China kupitia Kampuni ya China Merchants zimeingia Mkataba wa Makubaliano ya ujenzi wa Bandari hiyo kwa utaratibu wa Ubia wa Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP).
Bandari ya Mtwara
Mheshimiwa Spika,
• Serikali imetenga eneo kubwa la Ardhi yenye ukubwa wa Hekta 2,647 litakalotumika kwa ajili ya upanuzi wa Bandari ya Mtwara. Hivyo, Serikali imenza upembuzi yakinifu wa Mradi wa Upanuzi wa Bandari ya Mtwara tangu mwaka 2011/2012 na kazi hiyo itakamilika katika mwaka huu wa 2013.
Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano Nchini
Mheshimiwa Spika,
• Mojawapo ya Mafanikio makubwa ya Serikali ya Awamu ya Nne ni ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (National ICT Broadband Backbone). Utekelezaji wa awamu ya I na II ya ujenzi wa Mkongo huo umekamilika. Mkongo huo una jumla ya Kilomita 7,560 zikiwemo Kilomita 5,448 zilizojengwa na Serikali na Kilomita 2,112 zilizojengwa na TANESCO. Mkongo huo umejengwa kwa kiwango cha ubora wa Kimataifa ambao unakidhi mahitaji ya ndani na nje ya Nchi. Mkongo huo una mizunguko (rings) mitatu ya Kaskazini, Kusini na Magharibi. Hivyo kunaufanya Mkongo kuwa na huduma ya uhakika isiyotetereka kirahisi kwani hata pale inapotokea Mkongo kukatika upande mmoja huduma itaendelea kuwepo bila ya matatizo yoyote.
Kuunganisha Mkongo na Zanzibar na Mikoa
Mheshimiwa Spika,
• Mkongo wa Taifa Mawasiliano wenye urefu wa Kilometa 7,560 umeunganishwa na Makao Makuu ya Mikoa 24 ya Tanzania Bara.
• Kwa upande wa Zanzibar, Pemba imeunganishwa na Mkongo kwa kutumia Msongo wa Umeme wa TANESCO kutokea Tanga wakati Unguja itaunganishwa kwa kutumia Msongo wa Umeme kati ya Dar es Salaam na Unguja. Uwekaji wa Mkongo huu umeanza hivi sasa.
Kuunganisha Mkongo na Nchi Jirani
Mheshimiwa Spika,
• Vituo tisa (9) vya Mkongo (Cross-border Connectivity Stations) vimejengwa mpakani na Nchi jirani za Rwanda, Burundi, Uganda, Kenya, Malawi, na Zambia. Hivi sasa nchi za Rwanda, Burundi, Malawi, na Zambia zinatumia huduma ya Mkongo wa Taifa kwa malipo kwa ajili ya kuunganishwa na Mikongo ya Kimataifa ya Baharini ambayo ni SEACOM na EASSy.
• Mradi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano umelenga kuunganisha Makao Makuu ya Mikoa na Wilaya zote Tanzania Bara na Visiwani. Mkongo ukifika Wilayani watoa huduma za mawasiliano na TEHAMA watasambaza huduma hizo hadi Vijijini kwa haraka na kwa gharama nafuu, hivyo kuharakisha ukuaji wa uchumi na maendeleo ya Taifa kwa kuwa Wananchi watapata fursa ya kutumia TEHAMA katika juhudi za kupambana na umaskini na kujiletea maendeleo kwa kasi zaidi. Manufaa ya Mkongo huo yameanza kuonekana kutokana na kupungua kwa gharama za mawasiliano ya simu Nchini kwa zaidi ya Asilimia 60 hivi sasa.
MAFANIKIO KATIKA MATUMIZI YA MITANDAO YA MAWASILIANO
Mheshimiwa Spika,
• Tangu Serikali ya Awamu ya Nne iingie madarakani, matumizi ya Simu za Mkononi na mawasiliano kupiti Mtandao wa Internet yameongezeka sana.
Simu za Mikononi
• Kiwango cha matumizi ya Simu za Mezani na Mkononi kimeongezeka kutoka Watumiaji 3,118,157 sawa na Asilimia 10 ya idadi ya Watu Nchini mwaka 2005 hadi Watumiaji 27,395,650, sawa na Asilimia 61 ya Watu Nchini mwaka 2012.
Mtandao wa Internet
Mheshimiwa Spika,
• Matumizi ya Mtandao wa Internet yameongezeka kutoka Watumiaji 1,681,012, sawa na Asilimia 4.5 mwaka 2005 hadi Watumiaji 7,519,078, sawa na Asilimia 16.8 mwaka 2012.
NISHATI
MPANGO WA KUONGEZA UZALISHAJI WA UMEME NCHINI
Mheshimiwa Spika,
• Kwa sasa (2013) uwezo wa kuzalisha umeme MW 1,438. Lengo ni kuzalisha MW 2,780 hadi MW 3,000 ifikapo mwaka 2015. Ipo miradi mingi inayotekelezwa na Serikali ili kufikia lengo hilo. Miongoni mwa miradi hiyo ni pamoja na ifuatayo:
(i) Ujenzi wa Mitambo ya kusafisha Gesi Asilia na Bomba la kusafirisha Gesi Asili kutoka Mnazi Bay hadi Mtwara na Songosongo Kisiwani (Lindi) kupitia Somanga Fungu hadi Dar es Salaam. Gharama za Mradi huu ni Dola za Marekani Milioni 1,225.3, sawa na Shilingi Trilioni 1.96. Kati ya fedha hizo Asilimia 95 ni Mkopo Nafuu kutoka Benk ya Exim ya China na Asilimia 5 itachangiwa na Serikali.
(ii) Serikali inatekeleza mradi wa kujenga Mtambo wa Kufua Umeme wa Kinyerezi I utakaozalisha MW 150 na Kinyerezi II wa MW 240.
(iii) Serikali imekamilisha Mradi wa Ujenzi wa Mtambo wa kufua umeme wa MW 105 wa Ubungo II, Dar es Salaam. Vilevile, Serikali inatekeleza mradi wa ujenzi wa Mtambo wa kufua umeme wa MW 60 Nyakato, Mwanza.
(iv) Miradi mingine ni Mradi wa Somanga Fungu unaotekelezwa na Kampuni ya Kilwa Energy unaotarajiwa kuzalisha MW 320.
(v) Mradi mwingine ni ule wa kufua umeme wa Mchuchuma wa kuazalisha MW 600 na Mradi wa Makaa ya Mawe wa Ngaka utakaozalisha MW 40.
• Miradi hii ikikamilika itaongeza uwezo wa uzalishaji umeme Nchini na kuondoa tatizo lililopo kwa kiwango kikubwa.
Mafanikio mengine katika Sekta ya Nishati
• Serikali imefanikiwa kusambaza Umeme katika Wilaya 117 (sawa na Asilimia 89) kati ya Wilaya 133 zilizopo Nchini.
• Idadi ya Watanzania wanaopata umeme imeongezeka kutoka Asilimia 10 mwaka 2005 hadi Asilimia 14.5 mwaka 2012/2013.
• Kutokana na kuhamasisha uwekezaji katika Sekta ya Nishati, Makampuni makubwa yamefanya utafiti na Kugundua Gesi Asilia kiasi cha Fiti za Ujazo Trilioni 32 kwenye kina kirefu cha bahari.
• Serikali inatekeleza Mradi mkubwa wa ujenzi wa Bomba la Gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam ambao ukikamilika utatuwezesha kuwa na uhakika wa Umeme Nchini na wa bei nafuu. Hatua hii itasaidia kuokoa Dola za Kimarekani Milioni 850 kwa mwaka kwa kutumia Gesi Asilia badala ya Mafuta kuzalisha Umeme.
(c) KILIMO
Mafanikio ya Sekta ya Kilimo
Mheshimiwa Spika,
• Katika kipindi cha mwaka 2006/2007 hadi 2012/2013, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali zenye lengo la kuimarisha Sekta ya Kilimo na kuleta Mapinduzi ya Kijani hapa Nchini. Hatua hizo ni pamoja na kutekeleza programu ya kuendeleza Sekta ya Kilimo (ASDP), azma ya KILIMO KWANZA, Mipango wa Ruzuku ya Pembejeo za Kilimo na Mifugo, Kuanzishwa kwa mpango wa kukopesha wakulima Matrekta, Uanzishwaji wa Benki ya Kilimo, kuanzisha Mpango wa Kuendeleza Kanda za Kilimo (SAGCOT) na kadhalika.
• Mpango wa Uwekezaji wa Ukanda wa Kusini (SAGCOT). Huu ni mpango wa kilimo ambao unashirikisha Sekta binafsi wakiwemo Wadau wa Maendeleo, Wawekezaji wa Ndani, Wawekezaji wa Kimataifa na Taasisi mbalimbali za ndani na nje ya Nchi.
• Wakati Mpango wa SAGCOT unaanza mwaka 2010/2011, jumla ya wakulima walikuwa takriban 265 tu walijiunga na Mpango huo, kutokana na usimamizi mzuri wa Mpango huu hadi mwaka 2012/2013 idadi ya wakulima imeongezeka hadi kufikia 3,000.
• Tayari matokeo ya awali ya kutia moyo yameshaanza kuonekana ambapo Wakulima wadogo wameweza kuvuna kiasi cha Tani 8 za mpunga kwa Hekta kutoka Tani 1.5 walizokuwa wanavuna kabla ya kujiunga na Mpango wa SAGCOT na wameweza kuzalisha mara mbili ya wakulima wakubwa wanaowazunguka ambao wanavuna Tani 4 tu kwa Hekta). Haya ni mafanikio makubwa ambayo Serikali yetu inapaswa kujivunia.
Benki ya Kilimo
Mheshimiwa Spika,
• Serikali imekamilisha maandalizi ya kuwepo kwa Benki ya Kilimo ambayo inatarajiwa kuanzishwa katika mwaka wa 2013/2014 ili kuwawezesha wakulima kupata mikopo kwa riba nafuu. Aidha, Benki hiyo tayari imeshasajiliwa na Serikali imeshateua Wakurugenzi wa Bodi wa muda na Mtendaji Mkuu wa muda. Nafasi za kazi kwa watendaji wakuu wa Benki hiyo zimeshatangazwa.
Pembejeo na zana za Kilimo
Mheshimiwa Spika,
• Utaratibu wa utoaji wa Ruzuku ya Pembejeo umewezesha jumla ya Kaya takriban Milioni 2 kunufaika na Mpango huo.
• Kutokana na juhudi hizi za Serikali matumizi ya mbolea yameongezeka kutoka Tani 73,000 mwaka 2006/2007 hadi kufikia Tani 240,350 mwaka 2012/2013, na matumizi ya Mbegu bora yameongezeka kutoka Tani 11,056 mwaka 2006/2007 hadi Tani 30,443 mwaka 2012/2013.
Matumizi ya Zana za Kilimo
Mheshimiwa Spika,
• Kutokana na juhudi za kuhimiza matumizi ya zana bora za kilimo, Matrekta yameongezeka kutoka Matrekta Makubwa 7,823 na Madogo 3,400 mwaka 2010 hadi kufikia Matrekta Makubwa 8,466 na Madogo 4,571 mwaka 2011. Serikali za mikoa zilifanya kazi nzuri sana ya kuwasaidia wakulima kupata matrekta hayo jambo lililofanya matrekta ya mkopo kuchukuliwa yote. Sasa hivi Serikali imeshaandaa mpango wa kuingiza Matrekta yapatayo 3,000 kutoka India kwa ajili ya kuwakopesha Wananchi.
Kilimo cha Umwagiliaji
Mheshimiwa Spika,
• Eneo linalotumika kwa Umwagiliaji limeongezeka kutoka Hekta 233,398 mwaka 2006/2007 hadi kufikia Hekta 450,392 mwaka 2012/2013. Kwa vile skimu nyingi zipo katika hatua mbalimbali za ujenzi, Serikali inaamini kuwa eneo la umwagiliaji litaongezeka maradufu katika siku za usoni.
(d) VIWANDA
Mheshimiwa Spika,
• Ukuaji wa Sekta ya Viwanda umeongezeka kutoka Asilimia 8.4 mwaka 2005 hadi Asilimia 9.9 mwaka 2008. Licha ya kutokea Mdororo wa Kiuchumi mwaka 2008/2009 na matatizo ya umeme, ukuaji wa Sekta ya Viwanda umeendelea kuwa juu ya Asilimia 8.2 kwa mwaka.
• Viwanda vikubwa vya Saruji, Bia, Karatasi, Sigara, ambavyo vilibinafsishwa katika miaka ya 1990 vimeongeza uzalishaji mara dufu.
• Katika kuhamasisha na kuvutia Uwekezaji, jumla ya Wawekezaji 59 tayari wameanzisha Viwanda vya kuzalisha bidhaa mbalimbali na wamewekeza Mtaji wa Dola za Kimarekani Milioni 792.2.
• Mauzo ya bidhaa nje za Viwanda yameongezeka kutoka Dola za Marekani Milioni 156.1 mwaka 2005 hadi Dola za Marekani Milioni 861.5 mwaka 2011/2012.
(e) MAENDELEO YA RASILIMALI WATU (Elimu, Afya na Maji)
MAFANIKIO YA ELIMU
(i) Elimu ya Msingi
Mheshimiwa Spika,
• Idadi ya Shule za Msingi imeongezeka kutoka Shule 14,400 mwaka 2006 hadi 16,331 mwaka 2012.
• Idadi ya Wanafunzi imeongezeka kutoka Wanafunzi Milioni 7.9 mwaka 2006 hadi Wanafunzi 8.3 mwaka 2012.
• Idadi ya Walimu imeongezeka kutoka Walimu 135,013 mwaka 2005 hadi kufikia 180,987 mwaka 2012 na uwiano wa Mwalimu kwa Mwanafunzi umeimarika kutoka 1:51 mwaka 2010 hadi 1:46 mwaka 2012.
(ii) Elimu ya Sekondari
Mheshimiwa Spika,
• Idadi ya Shule za Sekondari imeongezeka kutoka Shule 1,845 mwaka 2006 hadi Shule 4,528 mwaka 2011/2012.
• Idadi ya Wanafunzi wanaojiunga na Kidato cha Kwanza imeongezeka kutoka Wanafunzi 196,391 mwaka 2006 hadi Wanafunzi 517,993 mwaka 2012.
• Idadi ya Walimu wa Sekondari imeongezeka kutoka Walimu 23,805 mwaka 2005/2006 hadi Walimu 65,086 mwaka 2012.
(iii) Vyuo vya Ualimu
Mheshimiwa Spika,
• Hivi sasa Mafunzo ya Elimu ya Ualimu ngazi ya Cheti na Stashahada yanatolewa katika Vyuo vya Ualimu 34 vya Serikali na Vyuo 82 visivyo vya Serikali vyenye uwezo wa kudahili Wanachuo 47,898 kwa wakati mmoja. Uandikishaji kwa mwaka katika Vyuo hivyo ni takriban Wanachuo 43,258.
(iv) Elimu ya Juu
Mheshimiwa Spika,
• Idadi ya Vyuo Vikuu na Vyuo Vikuu Vishiriki imeongezeka kutoka Vyuo 26 mwaka 2005 hadi Vyuo 46 mwaka 2012 vya Serikali na Binafsi.
• Kati ya Vyuo hivyo vipya, ni Chuo Kikuu cha Dodoma kinachoendelea kujengwa ambacho kikikamilika kitakuwa na Wanafunzi 40,000 na hivyo kuwa ndicho kikubwa kuliko vyote Nchini.
• Wanafunzi wanaojiunga na Vyuo Vikuu vilivyopo Nchini imeongezeka kutoka Wanafunzi 40,719 mwaka 2005/2006 hadi 166,484 mwaka 2011/2012.
• Fedha za mikopo ya Elimu ya Juu zimeongezeka kutoka Shilingi Bilioni 56.1 mwaka 2005/2006 hadi Shilingi Bilioni 326 mwaka 2012/2013.
• Idadi ya Wanafunzi wanaopata mikopo ya Elimu ya Juu imeongezeka kutoka 55,584 mwaka 2006 hadi Wanafunzi 98,772 mwaka 2012.
AFYA
Mheshimiwa Spika,
• Serikali imeongeza uwezo wa ndani wa kutibu Maradhi mbalimbali yakiwemo ya upasuaji wa Moyo ambapo hadi sasa zaidi ya Wagonjwa 450 wamepatiwa huduma hiyo.
• Serikali imekarabati kwa kiwango kikubwa Hospitali mbalimbali Nchini, ikiwemo Hospitali ya Saratani ya Ocean Road kwa kuongeza uwezo wake kutoka Vitanda 120 hadi 270. Pia, jengo maalum la kutoa huduma ya Saratani katika Hospitali ya Bugando limekamilishwa.
• Kutokana na juhudi za kuhamasisha matumizi ya Vyandarua na udhibiti wa Mazalia ya Mbu, kiwango cha Malaria Nchini kwa Watoto walio na umri wa chini ya miaka Mitano kimepungua kutoka Asilimia 18 mwaka 2007 hadi Asilimia Tisa (9) mwaka 2012.
• Jumla ya Vyandarua vilivyowekwa Viuatilifu vya muda mrefu ambavyo vimesambazwa kwa Kaya zenye Watoto walio na umri chini ya Miaka 5 na Wanawake Wajawazito imefikia Milioni 43.
• Jitihada za kudhibiti Malaria zimechangia kupunguza Vifo vya Watoto Wachanga kutoka Vifo 99 kwa kila Watoto 1,000 mwaka 1999 hadi Vifo 51 kwa kila Watoto 1,000 mwaka 2010.
• Vilevile, vifo vya Watoto wenye umri chini ya miaka 5 vimepungua kutoka Vifo 147 kwa kila Watoto 1,000 mwaka 1999 hadi Vifo 81 kwa kila Watoto 1,000 mwaka 2010.
• Aidha, Vifo vya Mama Wajawazito vitokanavyo na Uzazi vimepungua kutoka 578 kwa kila Vizazi hai 100,000 mwaka 2004/2005 hadi Vizazi 454 mwaka 2010.
• Idadi ya Wanafunzi wanaodahiliwa katika Sekta ya Afya wa ngazi ya Cheti, Stashahada na Uzamili imeongezeka kutoka 5,365 mwaka 2010/2012 hadi 7,458 mwaka 2011/2012. Kati ya Wanafunzi hao, wapo Wauguzi 3,136, Wataalam wa Sayansi Shiriki 2,257 na Wataalam mbalimbali wa ngazi ya Shahada wapatao 1,320.
• Maambukizi ya UKIMWI yamepungua kutoka Asilimia 5.7 mwaka 2007/2008 hadi Asilimia 5.1 mwaka 2011/2012.
MAJI
• Hadi mwaka 2012/2013 zaidi ya miradi 138 ya maji ilikuwa imekamilika katika Halmashauri mbalimbali Nchini.
• Mpaka kufikia mwaka 2012/2013 upatikanaji wa maji Vijijini uifikia Asilimia 58 na kwa upande wa Mijini ulifkia Asilimia 86.
• Kukamilika kwa mradi mkubwa wa maji kutoka Ziwa Victoria kwenda Mikoa ya Shinyanga na Kahama.
Mheshimiwa Spika,
Kama Serikali ya Awamu ya Nne isingekuwa na Weledi, je mafanikio haya yangepatikana!
Wahenga wanasema
“Mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni” Serikali inafanya kazi nzuri.
HOJA: TUME YA MABADILIKO YA KATIBA NA MCHAKATO WA KATIBA MPYA
Mheshimiwa Spika,
• Mheshimiwa Mbowe kwa niaba ya CHADEMA amekuja na vipaumbele vyake ambavyo havijumuishi miundombinu, kilimo, Maendeleo ya Viwanda wala Maendeleo ya Rasilimali Watu n.k. Kipaumbele chake kikubwa alichoanza nacho katika hotuba yake ni Tume ya Mabadiliko ya Katiba na Mchakato wa Katiba Mpya. Mimi nadhani Mheshimiwa Mbowe ameanza kuchanganya mambo na kupagawa na Uchaguzi wa 2015 wa nani atakuwa Rais 2015. Katika hotuba yake yapo maneno yanayosema “Tume ya Mabadiliko ya Katiba imethibitisha haina Weledi wa kusimamia mchakato huru usiofungamana na upande wowote”. Mimi nadhani hii siyo lugha ya kiungwana kwa Tume ambayo imeundwa kwa mujibu wa Katiba na yenye Watu wanaoheshimika sana Nchini.
• Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba wanaotokana na orodha ya majina yaliyopendekezwa na Vyama vya siasa vyenyewe. Katika Tume hii, wapo Wajumbe Wawakilishi kutoka CHADEMA, wenye Weledi mkubwa wengine ni Maprofesa. Siamini kama Mheshimiwa Mbowe anashindwa kutambua kwamba Mjumbe wake katika Tume hii ni Profesa Mwesige Baregu. Sasa ni Weledi upi anaozungumzia ambao Profesa Baregu hana.
Mheshimiwa Spika,
• Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba waliteuliwa na Mheshimiwa Rais kutokana na orodha ya majina yaliyopendekezwa na Vyama Siasa vyenye usajili wa kudumu. Aidha, Jumuiya za Kidini, Asasi za Kiraia, Jumuiya/Taasisi zisizo za Kiserikali na makundi ya watu wenye malengo yanayofanana. Uteuzi wa Wajumbe ulizingatia sifa zilizoanishwa kwenye kifungu cha 6 (3) (a, b, c) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Sura ya 83.
• Kwa kuzingatia utaratibu huo, inaonyesha kuwa Wajumbe wa Tume wana sifa na Weledi wa kutosha kutekeleza majukumu waliyokabidhiwa na Taifa.
Hoja: Tume kutokuwa na nia na dhamira ya kusimamia mchakato huru wa Katiba.
JIBU:
Mheshimiwa Spika,
• Tume inafanya kazi kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, (Sura ya 83) ambayo imeainisha Majukumu na Hadidu za Rejea. Hivyo, kwa muhtasari ni kwamba:
i) Utendaji kazi wa Tume unazingatia majukumu ya Tume kwa mujibu wa Hadidu za Rejea kama zilivyoanishwa kwenye Vifungu vya 9, 17 vya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83;
ii) Katika utekelezaji wa majukumu yake, Tume imepokea na kukusanya maoni ya Wananchi kuanzia mwezi Julai, 2012 na kukamilika mwezi Januari, 2013;
iii) Kwa mujibu wa Kalenda ya Tume, hivi sasa Tume imefanya kazi ya uchambuzi wa maoni yaliyokusanywa ili kutayarisha Rasimu ya Ripoti na Rasimu ya Katiba ambayo itawasilishwa kwa Wananchi kupitia Mabaraza ya Katiba ya Wilaya ambayo uundwaji wake unaendelea hivi sasa;
iv) Kwa mujibu wa Ratiba ya Utekelezaji wa Kazi za Tume hadi kufikia Mwezi Aprili, 2014 Tanzania itakuwa na Katiba Mpya;
Mheshimiwa Spika,
• Tunaposema Tume haina nia na dhamira ya kweli ni kuwavunja nguvu, kuwakatisha tamaa na kuwadharau watu tuliowaamini na kuwapendekeza sisi wenyewe na bila kuzingatia mazingira magumu wanayokumbana nayo katika utekelezaji wa kazi tuliyowapatia.
• Napenda kutumia fursa hii pia kuwapa moyo Wajumbe wote wa Tume na Sekretarieti yake kuendelea na kasi na ari waliyonayo katika kufanikisha jukumu kubwa walilokabidhiwa na Taifa la kuhakikisha kuwa, kufikia mwaka 2014, tunapata Katiba Mpya iliyotokana na maoni ya Wananchi.
• Nawasihi wasife moyo, kwani Wananchi wanatambua juhudi zao za dhati katika kutekeleza jukumu walilokabidhiwa. Hivyo, Kauli iliyotolewa na Kambi ya Upinzani Bungeni kuwa Tume hii haina weledi na dhamira ya kweli kusimamia mchakato huru wa Katiba, ni kuwavunja moyo kuwakatisha tamaa na kuwadharau Watu tuliowaamini na kuwapendekeza sisi wenyewe na bila ya kuzingatia mazingira magumu wanayokumbana nayo katika utekelezaji wa kazi nzito tuliyowawakabidhi.
Hoja kuhusu: Mchakato wa Mabadiliko ya Katiba yaliyokusudiwa yanaelekea kuilinda CCM na Serikali yake na kuendeleza baraka za “Status Quo”.
JIBU:
Mheshimiwa Spika,
• “Status Quo” inayozungumziwa ni ipi? Kwa maana, Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba hawatokani na wana CCM peke yake. Wajumbe wale ni mchanganyiko wa watu waliopendekezwa kutoka Vyama vya Siasa vyenye usajili wa kudumu, Jumuiya za Kidini, Asasi za Kiraia, Jumuiya/Taasisi Zisizo za Kiserikali na makundi ya watu wenye malengo yanayofana. Hivyo, siyo kweli kwamba Tume inaelekea kutengeneza Katiba itakayoilinda CCM.
• Kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83, mchakato wote wa kupatikana kwa Katiba Mpya umekuwa ukiwahusisha na utaendelea kuwahusisha Wananchi katika hatua zote:
i) Kwa kuzingatia Kifungu cha 9 (1) Tume ilitumia njia mbalimbali katika kukusanya maoni ya Wananchi;
ii) Kwa mujibu Kifungu cha 18 (1), (2), (3) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83, Rasimu ya Katiba yenye maoni ya Wananchi itawasilishwa kwa Mwananchi kupitia Mabaraza ya Katiba ya Wilaya ambapo Wananchi watapata fursa ya kuijadili na kuitolea maoni Rasimu iliyoandaliwa kutokana na maoni yao wenyewe;
iii) Kwa mujibu wa Vifungu vya 25 (1), 26 (2) Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano na wale wa Baraza la Wawakilishi ambao ni Wawakilishi wa Wananchi watapata fursa ya kuipitia kuijadili na kuipitisha au kuikataa Rasimu ya Katiba na wanaweza kuifanyia mabadiliko kama watakavyoona inafaa;
iv) Kwa mujibu Kifungu cha 36 cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83, Katiba iliyopendekezwa itapelekwa kwa Wananchi ili waweze kuipitisha au kuikataa kwa kupiga kura ya “Ndiyo” au “Hapana”;
v) Mchakato huo unashirikisha Wananchi wa Vyama vyote na wasiokuwa na vyama. Siyo sahihi kusema kuwa Mabadiliko ya Katiba yataendelea kuibeba CCM. Yote yanayofanywa na yatakayofanywa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba ni kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba inayoainisha mchakato ambao ulipitishwa na Bunge hili na kisha kuwekwa mezani katika Baraza la Wawakilishi Zanzibar.
Hoja: Tume haikuwa na utaratibu madhubuti wa kutoa elimu kwa Wananchi juu ya masuala yote yanayohusu Katiba Mpya na kwamba haikutoa elimu ya kutosha kwa Wananchi ili kuwaandaa kuchangia maoni yao kwa Tume wakiwa na uelewa wa kutosha.
JIBU:
Mheshimiwa Spika,
• Katika suala la kutoa elimu kwa Wananchi kuhusu Mchakato wa Katiba Mpya, Tume iliandaa program mbalimbali za Elimu kwa kutumia:
i) Vyombo vya Habari [Redio, Luninga, Magazeti];
ii) Kutoa machapisho mbalimbali yakiwemo:
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Lugha Nyepesi;
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kwa Lugha nyepesi;
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Sura ya 83;
Hadidu za Rejea za Tume ya Mabadiliko ya Katiba;
Kazi za Tume ya Mabadiliko ya Katiba;
Maswali yanayoulizwa Mara kwa mara.
• Tume imehakikisha kuwa Machapisho hayo pamoja na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Katiba ya Zanzibar yalisambazwa Nchi nzima kabla Tume haijafika kukusanya maoni ya Wananchi. Naamini kwamba, Waheshimiwa Wabunge, ninyi ni mashahidi wa suala hili kwani Tume iliwapatia nyaraka hizo ikiwa ni pamoja na Wananchi katika Majimbo yenu.
• Mheshimiwa Mbowe pia, analinganisha mchakato wa Katiba Mpya baina ya Tanzania na Kenya. Eti Tume ya Katiba ya Kenya ilitoa elimu kwa miezi sita kabla ya kuanza kukusanya maoni ya Wananchi.
Mheshimiwa Spika,
• Mimi nisingependa kutumia Kenya kama mfano. Kwa sababu Tume ya Katiba ya Kenya ilikwenda kwa Wananchi mara mbili. Mara ya kwanza ilikwenda kutoa Elimu ya Katiba, na mara ya pili ilikwenda kwa Wananchi kukusanya maoni. Baada ya hapo Tume hiyo haikurudi tena kwa wananchi hadi wakati wa kura ya maoni. Matokeo yake ni kwamba, eneo na idadi ya wananchi wa Kenya waliofikiwa na Tume ilikuwa ndogo.
Mheshimiwa Spika,
• Hadi kufikia hatua ya kupata Katiba mpya, Tume ya Mabadiliko ya Katiba itakwenda kwa Wananchi mara nne kupata maoni yao. Kwanza ni wakati wa kuwaelimisha na kukusanya maoni yao; Pili ni kupitia Mabaraza ya Katiba ya Wilaya; Tatu ni kwa kupitia Bunge Maalum la Katiba kwa Wananchi kuwalikishwa na Wawakilishi wao ikiwa ni pamoja na Waheshimiwa Wabunge na Waheshimiwa Wawakilishi wa Baraza la Wawakilishi la SMZ na Nne ni kwa Wananchi kushirikishwa katika kuiridhia rasimu ya Katiba kwa kupiga Kura ya Maoni.
• Ni wazi kuwa Tume yetu itawafikia Wananchi wengi kuliko Tume ya Katiba ya Kenya. Hivyo Tume ya Kenya haina vigezo vya kulinganishwa na yetu.
Hoja Kuhusu: Muda uliowekwa na Tume wa kukusanya maoni ni mdogo ukilinganishwa na ukubwa wa Nchi na Wingi wa Wananchi. Wananchi walipewa dakika 5 kuwasilisha maoni yao kwenye Mikutano
JIBU:
Mheshimiwa Spika,
• Kwa mujibu wa Kifungu cha 9 (1) (a) Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Sura ya 83, Tume imepewa jukumu la kuratibu na kukusanya maoni ya Wananchi. Katika kutekeleza jukumu hilo Tume iliweka utaratibu wa kutumia njia mbalimbali za kuratibu na kukusanya maoni ya Wananchi. Njia hizo ni:
i) Kukusanya maoni kwenye Mikutano ya hadhara iliyoitishwa na Tume kwenye Mikoa yote, Wilaya zote na Mamlaka za Serikali za Mitaa zote Tanzana Bara na Zanzibar;
ii) Pale ambapo mwananchi hakuweza kumaliza kutoa maoni yake kwa kuongea alipewa Fomu maalum za Tume ili aweze kuandika maoni yake yaliyobakia;
iii) Katika Mikutano ya hadhara, Mwananchi yeyote aliyetaka kutoa maoni yake kwa njia ya maandishi alipewa fomu maalum iliyotayarishwa na Tume;
iv) Kupokea maoni kupitia Sanduku la Barua 1681 Dar es Salaam na 2775 Zanzibar;
v) Kupokea maoni kupitia Mitandao ya Kijamii ya barua pepe ya katibu @katiba.go.tz, facebook yenye anuani ya “tumeyamabadilikoya katiba”, Tovuti ya Tume yenye anuani ya www.katiba.go.tz;
vi) Makala mbalimbali kutoka kwenye Magazeti; na
vii) Katika njia ya ujumbe mfupi wa simu.
• Mimi najiuliza hivi ni Nchi gani ambayo Tume imeweza kuzunguka kila kitongoji?. Kwa mujibu wa kumbukumbu zilizopo, hakuna Tume yoyote iliyoweza kuwafikia Wananchi wengi, kukusanya maoni mengi, kutumia njia nyingi za kukusanya maoni na kufika katika kila Wilaya Nchini na katika baadhi ya Vijiji. Tume nyingine zimetumia “sample” katika baadhi ya maeneo
• Ingawa idadi ya waliotoa maoni ni muhimu lakini suala la msingi ni uzito wa maoni yaliyopatikana. Kwa mujibu wa Tume, Wananchi wametoa maoni katika maeneo yote muhimu ya Katiba. Sasa kwa utaratibu huu, utaratibu wa hovyo utakaozaa Katiba hovyo anaouzungumzia Mheshimiwa Mbowe ni upi?
• Hivyo, kutokana na Taratibu nzuri zilizowekwa na Tume kukusanya maoni, tunastahili kuipongeza kwa kazi inayofanya na siyo kuanza kuishambulia, kuishutumu na kuibeza kwa kazi ambayo tuliwatuma kupitia Sheria tuliyoipitisha sisi wenyewe.
Mheshimiwa Spika,
• Aidha, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni pia ametoa tishio la kuitisha maandamano Nchi nzima na kuwataka Wananchi wagomee mchakato wa Katiba.
• Niwaombe Wananchi wote kupitia Bunge lako Tukufu kutokubali kurubuniwa na baadhi ya Wanasiasa wasiokuwa na nia safi na wenye agenda zao za siri zenye kulenga kuvuruga mchakato huu ambao ni muhimu kwa mustakabali wa Taifa letu. Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliwahi kusema kuwa “Akili za Kuambiwa, Changanya na zako”. Napenda kuwakumbusha kuwa, kila maandamano yanayofanyika, wanaoathirika ni Wananchi na sio Viongozi wanaoshinikiza maandamano hayo.
Hoja kuhusu: Tume kutokuwa huru au kuutafsiri uhuru vibaya na kutoa Taarifa zake kwa Mheshimiwa Rais.
JIBU:
Mheshimiwa Spika,
• Kifungu cha 10 cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Sura ya 83 kinatoa Mamlaka na Uhuru kwa Tume katika utekelezaji wa Majukumu yake bila ya kuingiliwa na Mtu au Mamlaka yoyote.
• Tangu ilipoanza kutekeleza majukumu yake, Tume imekuwa na utaratibu wa kutoa taarifa kuhusu jambo lolote linalopangwa kutekelezwa na baada ya utekelezaji wake. Taarifa hizo hutolewa kupitia Mikutano na vyombo vya habari, magazeti, majadiliano katika Redio na Luninga na mitandao ya Kijamii.
• Katikati ya mwezi Desemba, 2012 Mwenyekiti wa Tume aliongea na vyombo vya habari ambapo pamoja na mambo mengine alitoa taarifa ya utekelezaji wa kazi za Tume pamoja na ratiba ya kazi za Tume zinazotarajiwa kutekelezwa kipindi kijacho. Hivyo, hotuba ya Rais ya mwishoni mwa mwaka 2012 ilitokana na taarifa ya Mwenyekiti wa Tume alipoongea na Vyombo vya Habari na alifanya hivyo kwa kutambua kuwa Watanzania wengi huwa wanasikiliza kipindi hicho cha Rais.
• Katiba siyo siri. Kwa maana hiyo, Mheshimiwa Rais kuongea na Wananchi na kutumia taarifa iliyotolewa kwa Vyombo vya Habari Mimi sioni kama ina ubaya. Mheshimiwa Rais amekuwa wazi kwa kuonesha kuwa Hotuba yake ilitokana na Taarifa ya Tume, kosa lake ni nini?. Aidha, Mheshimiwa Rais ndiye msemaji Mkuu wa Nchi. Sasa najiuliza kama yeye ana kosa kwa kuzungumza na Wananchi kuhusu kazi za Tume.
• Aidha, kupitia Kalenda zilizotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba za mwaka 2013, Tume imeainisha ratiba ya utekelezaji wa shughuli zote za Tume kwa kuainisha aina ya jukumu, muda utekelezaji na tarehe ya mwisho ya utekelezaji. Kalenda hizo zimegawanywa kwenye Taasisi za Serikali, Vyama vya Siasa, Jumuiya za Kidini, Asasi za Kiraia, Jumuiya/Taasisi zisizo za Kiserikali, Makundi mbalimbali na kwa Wananchi. Hivyo, ratiba ya utekelezaji wa shughuli za Tume siyo siri. Kwa msingi huo, Kauli ya Kambi ya Upinzani kwamba Tume inatoa taarifa zake za utendaji kwa Rais na Serikali tu siyo sahihi bali taarifa za Tume hutolewa kwa Umma wote wa Tanzania kwa ujumla. Suala linalotakiwa kwa kila mmoja wetu ni kuwa makini kusikiliza taarifa mbalimbali zinazotolewa na Tume, kwani utendaji wao ni wa wazi.
Hoja kuhusu: Tume ya Mabadiliko ya Katiba kutowajibika kwa Bunge
JIBU:
Mheshimiwa Spika,
• Tume ya Mabadiliko ya Katiba ni Taasisi huru inayotekeleza majukumu yake chini ya Wizara ya Katiba na Sheria.
• Katika uwajibikaji wake kwa Bunge kwa maana ya kutoa taarifa za mapato na matumizi, utekelezaji wa kazi zake, mafanikio na cha changamoto, Tume ya Mabadiliko ya Katiba hupitia Wizara ya Katiba na Sheria ambayo ndiyo Wizara Mama inayowasilisha maombi ya fedha za kazi za Tume na kutoa Taarifa ya Utekelezaji.
• Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba anawajibika kwa Tume yenyewe na siyo kwa Taasisi au Mamlaka nyingine yoyote.
• Katibu wa Tume akiwa ndiye Mtendaji Mkuu wa Tume, anawajibika kuwasilisha taarifa za utekelezaji wa masuala ya fedha kwa Katibu Mkuu – Wizara ya Katiba na Sheria ambaye kupitia Waziri wa Katiba na Sheria anawasilisha taarifa hizo Bungeni.
• Sisi hatudhani kwamba Tume imekosea kwa hali yoyote ile. Kwa hiyo siyo busara Kambi ya Upinzani kuitumbukiza Tume katika mgogoro na Taasisi au Mhimili mwingine yaani Bunge. Kimsingi Tume haijakataa kuhojiwa na Bunge. Taratibu zipo kupitia Wizara ya katiba na Sheria.
Hoja : Tume imetengeneza utaratibu wa Mabaraza ya Kikatiba ambao kwa ushahidi wa mwanzo inaonyesha kuwa hayo ni Mabaraza ya CCM na siyo Mabaraza ya Watanzania; kutokana na Wajumbe hao kuchaguliwa na Kamati ya Maendeleo ya Kata.
Mheshimiwa Spika,
• Katika kuwapata Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya, Tume ilitumia Muundo wa Serikali za Mitaa na taratibu za Mikutano katika ngazi hizo ikiwa ni katika Vijiji, Mitaa na Kata. Muundo huu si ubunifu wa Tume bali umeainishwa katika Sheria za Serikali za Mitaa zikiwa ni Sheria zilizotungwa na kuridhiwa na Bunge hili.
• Waheshimiwa Wabunge, mkiwa Wajumbe wa Mabaraza ya Halmashauri katika maeneo yenu, naamini mnafahamu kwamba, katika ngazi ya Kata, tofauti na ilivyo katika ngazi ya Mtaa na Kijiji, Chombo kinachotambuliwa Kisheria kutoa maamuzi kwa niaba ya Wananchi, ni Kamati ya Maendeleo ya Mtaa (WDC). Hivyo, maamuzi ya kutumia Chombo hicho, yana msingi katika Sheria za Serikali za Mitaa. Aidha, propaganda zinazoeleza kuwa, Mabaraza hayo ni ya CCM, na si Mabaraza ya Katiba ya Watanzania wote, siyo za kweli, bali zimelenga kujenga chuki na kupotosha Umma wa Watanzania. Uanachama au kutokuwa Mwanachama wa Chama cha Siasa haikuwa sifa mojawapo ya kuchaguliwa kuwa Mjumbe wa Baraza la Katiba la Wilaya. Madai yaliyotolewa na Mheshimiwa Mbowe kuwa Wagombea wasiokuwa wa CCM walienguliwa katika Chaguzi hizo si za kweli na yamelenga kupotosha Umma. Kwa mujibu wa Mwongozo, Wananchi walitakiwa kuomba kwenye ngazi za Vijiji na Mitaa kwa Tanzania Bara na Shehia kwa Zanzibar.
Mheshimiwa Spika,
• Kwa Tanzania Bara: Mikutano Mikuu ya Vijiji/Mitaa ilitumika kuwapigia Kura ya Siri Wananchi walioomba kuwa Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya bila kujali itikadi za Vyama vyao.
• Aidha, majina ya Wananchi waliochaguliwa kwenye ngazi ya Vijiji /Mitaa yaliwasilishwa kwenye Kikao cha Kamati ya Maendeleo ya Kata ili yapigiwe Kura za Siri na Wajumbe kwa utaratibu wa uchaguzi wa kawaida.
• Utaratibu wa Kamati za Maendeleo za Kata kuhusika katika uchaguzi huu, haujaanzishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Kamati hizo zimekuwa zikitumika kuchagua Wajumbe mbalimbali katika ngazi ya Kata, kama vile Kamati za Maji, Shule, Ukimwi, Afya, Mazingira, n.k.
• Suala la Wajumbe wa Kamati za Maendeleo za Kata kuwa na Wajumbe wengi kutoka Chama kimoja ni matokeo ya maamuzi ya Wananchi waliowachagua.
• Hoja kwamba Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya wachaguliwe na Wananchi moja kwa moja katika ngazi ya Kata, hilo HALIWEZEKANI. Mantiki yake ni kwamba, kwa mujibu wa Sheria za Serikali za Mitaa Na. 7 na 8 na Mamlaka za Wilaya na Miji za mwaka 1982 hakuna Mkutano wa uchaguzi unaowahusisha Wananchi wote katika ngazi ya Kata.
Hoja: Tume kukataa kubadilisha Muundo wa Mabaraza ya Katiba hata baada ya kupewa maoni na Wadau.
Mheshimiwa Spika,
• Baada ya kuandaa Rasimu ya Mwongozo kuhusu Muundo, Utaratibu wa kuwapata Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya, Tume iliusambaza Mwongozo huo kwa Wadau mbalimbali na kuutangaza kwenye Vyombo vya Habari ikiwemo Magazeti, Luninga na katika Tovuti ya Tume ambapo ilitoa muda kwa Wadau kuwasilisha maoni yao kuhusu Rasimu hiyo.
• Tume ilipokea maoni mbalimbali kutoka kwa Wadau na kwa kiwango kikubwa maoni hayo yalizingatiwa na kuingizwa kwenye Mwongozo. CHADEMA haikutoa maoni yake kwenye Tume kuhusu Rasimu ya Mwongozo. Badala yake ilitoa maoni yao katika Mikutano ya hadhara baada ya Mwongozo kuchapishwa na kusambazwa.
• Uzoefu unaonesha kwamba, lipo tatizo kwa upande wa CHADEMA kushinikiza kila jambo wanalolitoa Bungeni au katika Mikutano yao ya hadhara, bila ya kuzingatia kuwa lina maslahi ya Taifa au la, wakitaka litekelezwe na Serikali au Taasisi zake. Serikali imekuwa ikiwasikiliza mara nyingi, lakini inapotokea kuwa masuala wanayoyashinikiza yasipotekelezwa na Serikali kwa sababu za msingi, Chama hicho kimekuwa na tabia kupitia kwa Viongozi wake kutishia kuchukua hatua kadhaa ikiwemo kuitisha maandamano Nchi nzima na kususia masuala mbalimbali ya Kitaifa.
• Hali hiyo pia ilijitokeza hata wakati wa mchakato wa awali wa kutunga Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, ambapo licha ya kususia vikao vya Bunge vilivyokuwa vikijadili Muswada wa Sheria hiyo, bado Mheshimiwa Rais aliwapa fursa ya kuwasilikiza na kuchukua baadhi ya maoni yao. Hivyo, si sahihi kuisema Serikali ya CCM kuwa si sikivu na isiyojali maoni ya Wadau. Nawashauri CHADEMA kufuata na kuzingatia masharti ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ambayo kama nilivyosema hapo awali kuwa, si taratibu zilizoanzishwa na Tume.
Hoja: Sheria ya Marekebisho ya Katiba imefanyiwa marekebisho mara moja tu kinyume na Makubaliano ya CHADEMA na Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Spika,
• Utakumbuka kuwa, tarehe 10 Februari, 2012 Bunge lako Tukufu lilipitisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, 2011; na hatimaye Mheshimiwa Rais kuridhia Marekebisho hayo tarehe 20 Februari, 2012. Baada ya Marekebisho hayo, Mheshimiwa Rais aliteua Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambayo ilianza kutekeleza majukumu yake rasmi tarehe 01 Mei, 2012.
• Marekebisho hayo yalitokana na maoni kutoka Serikalini, pamoja na Wadau mbalimbali wakiwemo Vyama vya Siasa (CHADEMA, CUF na NCCR MAGEUZI) na Asasi mbalimbali za Kijamii; ambapo wote walipata fursa ya kukutana na Mheshimiwa Rais na kujadiliana naye kuhusu mapendekezo ya marekebisho ya Sheria hiyo.
• Katika majadiliano hayo, Wadau hao kwa pamoja walikubaliana na Serikali kwamba, Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, yafanywe kwa Awamu tatu. Awamu ya kwanza ikihusu Tume ya Mabadiliko ya Katiba na masuala mengine yanayohusiana nayo, ikiwa ni pamoja na Utaratibu wa kuwapata Wajumbe wa Tume na kuruhusu Wanasiasa kuteuliwa kuwa Wajumbe wa Tume. Vilevile ilikubaliwa kuwa, Awamu ya Pili ya marekebisho itahusu Bunge Maalum la Katiba pamoja na masuala yote yanayohusiana nayo. Aidha, Awamu ya Tatu na ya mwisho itahusu masuala yote ya Kura ya Maoni.
• Kutokana na utaratibu huo, Awamu ya Kwanza ya Marekebisho ilishafanyika, na hivyo kutoa nafasi sasa kwa majadiliano ya Awamu ya Pili ya marekebisho. Hivyo, mwezi Januari 2013, Vyama vya Siasa vya CHADEMA, CUF na NCCR MAGEUZI viliwasilisha kwa maandishi maoni yao yanayohusu mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Serikalini. Kwa nyakati tofauti, tarehe 04 – 08 Machi 2013, Wawakilishi wa Vyama vya CHADEMA, CUF na NCCR – MAGEUZI walikutana na Serikali chini ya Uongozi wa Mheshimiwa Waziri wa Nchi OWM (Sera, Uratibu na Bunge) na Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kujadili mapendekezo ya Vyama hivyo. Katika vikao hivyo ilipendekezwa kuwa, mapendekezo kuhusiana na Bunge Maalum la Katiba ndiyo yatakayojadiliwa huku yale yanayohusu Kura ya Maoni yatajadiliwa katika Awamu ya Tatu kwa kuwa, kabla ya zoezi hilo la Kura ya Maoni, Sheria mahsusi kuhusu Kura ya Maoni itatungwa kwa ajili ya mchakato huo.
Mheshimiwa Spika,
• Katika majadiliano hayo, yapo maeneo ambayo Serikali na Wadau walikubaliana na hivyo kuchukuliwa na kuingizwa katika Muswada wa Marekebisho ya Sheria hiyo. Ninapenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa, Muswada huo wa Marekebisho unatarajiwa kuwasilishwa katika Bunge hili la Bajeti.
Hoja: Bado haijulikani Wajumbe 166 watakaotokana na Taasisi mbalimbali zilizotajwa na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba watateuliwa kwa utaratibu gani na nani atakayefanya uteuzi huo.
Mheshimiwa Spika,
• Suala hili lilishabainishwa na kufanyiwa kazi na Serikali tangu awali, ambapo miongoni mwa marekebisho yanayotarajiwa kufanyika, Serikali imependekeza utaratibu utakaotumika kuwapata Wajumbe 166 waliotajwa katika Kifungu cha 22(1)(c) kutoka katika Taasisi mbalimbali kabla ya majina yao kuwasilishwa kwa Rais kwa majadiliano na Rais wa Zanzibar kwa ajili ya uteuzi.
• Utaratibu uliopendekezwa ni kuazima maneno yaliyopo chini ya Kifungu cha 6(6) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, 2011 yatumike katika kualika Asasi hizo kupendekeza majina ya Wajumbe kwa ajili ya uteuzi utakaofanywa na Mheshimiwa Rais kama ilivyokuwa wakati wa uteuzi wa Wajumbe wa Tume.
Mheshimiwa Spika,
• Kwa maelezo hayo, utaratibu huo utatumika mara baada ya Bunge lako Tukufu kupitisha Marekebisho ya Pili ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
Hoja: Hakuna muafaka juu ya uhalali wa idadi kubwa ya Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kutoka Zanzibar kushiriki katika mjadala wa Katiba Mpya kwenye masuala yasiyokuwa ya Muungano.
Mheshimiwa Spika,
• Suala hili pia lilijitokeza katika majadiliano; ambapo CHADEMA walitoa hoja ya kuwa, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wasiwe Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba. Walieleza kuwa, kwa kuwaruhusu Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kushiriki katika Bunge Maalum, kutaiongezea CCM na CUF idadi ya Wajumbe katika Bunge Maalum wakati CHADEMA ikibakiwa na idadi yake ya sasa katika Bunge la Muungano.
Mheshimiwa Spika,
• Naomba kusisitiza kuwa, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wataendelea kuwa Wajumbe katika Bunge Maalum la Katiba kama ilivyobainishwa katika Sheria. Hii ni kwa sababu Baraza la Wawakilishi ndicho Chombo mahsusi kinachowawakilisha Wananchi wa Tanzania Zanzibar katika masuala ya Muungano na yasiyo ya Muungano.
• Aidha, kwa mujibu wa Kifungu cha 26(2) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, msingi wa maamuzi katika Bunge Maalum la Katiba utafanywa kwa kuzingatia theluthi mbili ya idadi ya Wajumbe wote wa Bunge Maalum kutoka Tanzania Bara na theluthi mbili kutoka Tanzania Zanzibar. Hivyo, idadi yoyote ya Wabunge kutoka Zanzibar haitaathiri maamuzi ya Wajumbe kutoka Tanzania Bara.
Hoja: Hakuna Sheria inayompa Mheshimiwa Rais Mamlaka ya kuliitisha upya Bunge Maalum la Katiba na kulielekeza kuboresha masharti ya Katiba Mpya mara baada ya Bunge hilo kuipitisha.
Mheshimiwa Spika,
• Maelezo kuhusu Hoja hii yameainishwa bayana katika Kifungu cha 28 (2) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, 2011. Kifungu hiki kinachotoa fursa kwa Mheshimiwa Rais kuliitisha tena Bunge baada ya kuvunjwa au kukoma kwa lengo la kuboresha masharti yaliyomo katika rasimu ya Katiba inayopendekezwa kabla na baada ya Kura ya Maoni, hususan pale atakapoona kuna umuhimu wa kufanya hivyo kwa maslahi ya Taifa.
• Kwa maelezo hayo, utaona kuwa Sheria tangu awali ilishatoa muongozo kuhusu suala hili muhimu kwa kufanikisha azma ya Taifa ya kupata Katiba mpya.
Hoja: Haujulikani uhalali upi wa Kisheria utakaoiruhusu Tume ya Taifa ya Uchaguzi kusimamia na kuendesha kura ya maoni ya kuhalalisha Katiba Mpya.
Mheshimiwa Spika,
• Sheria kama ilivyo sasa, chini ya Sehemu ya Sita imetoa uhalali na muongozo wa Kisheria kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kushirikiana na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kuendesha na kusimamia zoezi zima la Kura ya Maoni kwa Rasimu ya Katiba Mpya. Hivyo, uhalali wa Tume hizi kuratibu zoezi hilo upo katika Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
Mheshimiwa Spika,
• Hata hivyo, ili zoezi hili lifanyike kwa ufanisi, Serikali pia imekwishaandaa Muswada wa Sheria ya Kura ya Maoni ambao nao unatarajiwa kuwasilishwa katika Bunge hili la Bajeti. Hivyo, ninawasihi Waheshimiwa Wabunge sambamba na maoni yao kuhusu Muswada huo na maoni mengine kwa ajili utaratibu mzima wa Kura ya Maoni katika Sheria iliyopo, tushirikiane kuyaandaa kwa ajili ya Awamu ya Tatu ya Marekebisho ya Sheria hii kama ilivyokubaliwa na Mheshimiwa Rais na Wadau mbalimbali wakiwemo Wawakilishi wa Vyama vya Siasa.
MATOKEO HAFIFU YA KIDATO CHA NNE MWAKA 2012
Hoja: Elimu sio kipaumble cha Taifa kwa CCM na Serikali yake
Jibu:
Mheshimiwa Spika,
• Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani katika eneo hili la Elimu ameanza kwa kumnukuu Rais wa 55 wa Marekani John Kennedy (1917- 1963 kuhusu maendeleo ya elimu katika Nchi yetu. Mimi nadhani hakuna haja ya kwenda mbali mpaka Marekani miaka hiyo ya nyuma ndiyo sisi Tanzania tupate suluhisho la matatizo ya elimu katika Nchi yetu. Jambo la msingi hapa ni kujua sisi tunasemaje. Mheshimiwa Mbowe anasema tufanye nini, siyo nadharia ya John Kennedy wa miaka hiyo.
• Katika hotuba yangu nilieleza juu ya uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali kwenye Sekta ya Elimu katika kipindi cha mwongo mmoja uliopita. Ni ukweli usiopingika pia kwamba, tulianza kupanua elimu ya Msingi na Sekondari kwa kasi sana mwaka 2006. Kipaumbele kiliwekwa katika Sekta ya Elimu ambapo Bajeti ya Elimu ilichukua nafasi ya kwanza kwa miaka nane mafululizo. Aidha, fedha zilizokuwa zinatengwa zilikuwa zinaongezeka mwaka hadi mwaka.
Bajeti ya Elimu Kuanzia Mwaka 2005/2006 hadi 2012/2013
ilikuwa inaongezeka kama ifuatavyo:
MWAKA BAJETI ASILIMIA YA BAJETI YOTE
2005/2006 Bilioni 669.5 16%
2006/2007 Bilioni 891.2 18.4%
2007/2008 Bilioni 1,086 17.9%
2008/2009 Bilioni 1,430 19.8%
2009/2010 Bilioni 1,743.9 18.3%
2010/2011 Bilioni 2,045.3 20.3%
2011/2012 Bilioni 2,283 19.7%
2012/2013 Bilioni 2,890 23.4%
• Matokeo ya uwekezaji huu hayawezi kuonekana mara moja na kwamba pamoja na umuhimu wake upanuzi wa elimu ya Msingi na Sekondari umekuja na changamoto zake, kama vile upungufu wa walimu, vyumba vya madarasa, madawati, vitabu na vifaa vingine vya kufundishia na kujifunzia. Nilieleza pia kwamba, Serikali inaendelea kuzitafutia ufumbuzi changamoto hizo hatua kwa hatua.
Hoja kuhusu: Elimu ya Tanzania imeporomoka kwa kiasi kikubwa cha sasa kuhatarisha mustakabali wetu kama Taifa hasa kutokana na kufeli kwa kutisha kwa Wahitimu wa Kidato cha Nne mwaka 2012.
JIBU:
Mheshimiwa Spika,
• Ni kweli kwamba, Matokeo ya Mitihani ya Kidato cha Nne mwaka 2012 yameonesha kuwa kiwango cha ufaulu kimeshuka kwa kiwango kikubwa ikilinganishwa na miaka ya hivi karibuni. Matokeo yaliyotangazwa yanaonesha kwamba kati ya Wanafunzi 397,132 waliofanya Mtihani huo, Watahiniwa 126,851 ndio waliofaulu. Katika idadi hii, Wanafunzi waliofaulu katika daraja la I-III ni 23,520 na daraja la daraja la IV ni 103,327. Watahiniwa 240,903 sawa na Asilimia 65.5 wamepata daraja la sifuri.
Mheshimiwa Spika,
• Kutokana na matokeo hayo, Serikali iliunda Tume inayoongozwa na Prof. Sifuni Mchome kama Mwenyekiti kufuatilia suala hilo ni Huru na inafanya kazi kwa mtazamo tofauti sana. Ina wajumbe kutoka Vyuo vya Elimu ya Juu; Baraza la Wawakilishi; Mashirika Yasiyo ya Kiserikali; Madhehebu ya Dini; Chama cha Walimu, Muungano wa wenye Shule Binafsi na Muungano wa Walimu Wakuu wa Sekondari.
• Hadidu za Rejea za Tume hiyo ni kama ifuatavyo:
i) Kubainisha sababu za matokeo mabaya ya Mtihani wa Kidato cha Nne mwaka 2012;
ii) Kubaini sababu za kushuka kwa kiwango cha ufaulu katika Mitihani ya Kidato cha Nne kuanzia kipindi cha mwaka 2005 hadi 2012;
iii) Kutathmini nafasi ya Halmashauri katika kusimamia Elimu ya Sekondari katika Halmashauri zake;
iv) Kuanisha sababu nyingine zinazoweza kuwa zimechangia hali hii ya matokeo;
v) Kutoa mapendekezo ya hatua za kuchukua mara moja kwa Wanafunzi 240,903 waliopata Daraja la Sifuri katika Mtihani wa Kidato cha Nne mwaka 2012; na
vi) Kutoa mapendekezo ya hatua za kuchukua kukabiliana na tatizo la mwenendo wa kushuka kwa kiwango cha elimu mara moja, kipindi cha muda mfupi, kati na kipindi cha muda mrefu;
• Kazi hii itafanyika kwa kipindi maalum kuanzia tarehe 1 Machi, 2013, Tanzania Bara na Zanzibar na kuwasilisha taarifa yake kwa Serikali mara baada ya kukamilisha kazi hiyo.
• Napenda kusisitiza kwamba Serikali ina dhamira ya dhati ya kupata ufumbuzi wa kudumu wa changamoto zinazoikabili sekta ya elimu kwa kuwashirikisha wadau wote. Naomba tuiache Tume hii huru ifanye kazi. Ifikiri nje ya sanduku na itupe mtazamo mpya. Baada ya hapo ndipo tuweze kusema kweli kama hakukuwa na sababu ya Tume hiyo. Nawaomba pia Waheshimiwa Wabunge tuangalie sana kauli zetu tusije tukakuta wakati mwingine tunawachochea walimu. Tuwape moyo wafanye kazi yao wakati tukishughulikia changamoto zinazowakabili.
HOJA: Serikali iliunda Tume ya kushughulikia suala la kuporomoka kwa elimu nchini 2010 hatua gani zimechukuliwa kufuatia mapendekezo ya Tume hiyo.
JIBU:
Mheshimiwa Spika,
• Mwaka 2011, Serikali iliunda Kikundi Kazi cha Serikali ambacho kilifanya utafiti wa kubaini chanzo cha wanafunzi kutofanya vizuri kwenye mitihani ya Kidato cha Nne mwaka 2010. Kikundi hicho kilikamilisha kazi na kuwasilisha taarifa yake mwezi Juni, 2011. Mapendekezo yaliyotolewa yanahitaji utekelezaji wa muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu. Serikali ilianza kutekeleza mapendekezo hayo hatua kwa hatua kuanzia mwaka 2012/2013. Kwa mfano, idadi ya walimu imeongezeka kutoka 40,517 mwaka 2010 hadi 78,055 mwaka 2013. Kwa mwaka huu wa fedha (2012/2013) peke yake Serikali imeajiri jumla ya walimu 12,969. Aidha, Mfumo wa kuwapangia vituo vya kazi unazingatia mahitaji (ikama) kwa shule zote. Ujenzi wa maabara, nyumba za walimu na hosteli za wanafunzi unaendelea katika Shule mbalimbali za Sekondari Nchini.
• Hata hivyo, bado mwelekeo wa ufaulu wa wanaomaliza Kidato cha Nne unapungua mwaka hadi mwaka. Jambo kubwa zaidi safari hii ni kushuka kwa ufaulu hata katika Shule za Mashirika ya Dini na Watu Binafsi zilizokuwa zinafanya vizuri sana. Hizi ni dalili kuwa hatujapata ufumbuzi wa tatizo hilo. Ndiyo maana, Serikali iliona ni vema kuunda Tume ambayo ni shirikishi zaidi na yenye kufanyakazi kwa kina zaidi kuliko Kikosi Kazi.
• Tume iliyoundwa na Serikali hivi karibuni, ni tofauti na Kikundi Kazi cha mwaka 2011 kwa sababu inajumuisha Wadau mbalimbali wa Sekta ya Elimu kama nilivyokwishaeleza. Aidha, hadidu za rejea za Tume hii ni pana zaidi kuliko zile za Kikundi Kazi cha mwaka 2011.
HOJA: Serikali imechukua hatua gani kuwawajibisha viongozi wanaohusika na Sekta ya Elimu kufuatia kufeli kwa kutisha kwa wahitimu wa Kidato cha Nne mwaka 2012.
JIBU:
Mheshimiwa Spika,
• Kwa sasa bado tunatafuta chanzo cha tatizo. Matokeo ya Tume iliyoundwa itaonesha chanzo cha tatizo. Serikali itajielekeza zaidi katika kupata ufumbuzi wa kudumu wa tatizo linalotukabili, kuelezana tulipokosea na kwa pamoja kurekebisha makosa na kusonga mbele katika safari ya maendeleo ya Elimu Nchini.
Hoja: Ushiriki wa Wanafunzi wa Elimu ya Juu katika Siasa unaonekana kuelekea upande wa kukipendelea CCM.
Jibu:
Mheshimiwa Spika,
• Kwa mujibu wa Sheria ya Vyuo Vikuu Kifungu Na. 52 ni kosa kuendesha harakati za kisiasa katika mazingira/maeneo ya Vyuo Vikuu. Kifungu hiki hakiwazuii Wanafunzi kuwa Wanachama wa vyama mbalimbali au kuwa na itikadi tofauti na ya Chama Tawala. Kinachokatazwa na Sheria hii ni kufungua matawi, kufanya kampeni, kufanya mikutano au kuandikisha Wanachama katika maeneo ya Vyuo Vikuu.
• Kimsingi Vyama vya Siasa vimetumia mbinu nyingi kupata Wananchama. Chama cha Mapinduzi kimeamua kuanzisha Mkoa wa CCM katika Vyuo Vikuu lakini kwa kuweka msisitizo kuwa shughuli zake za kichama zifanyike nje ya mazingira ya Chuo/Vyuo. Vyama vingine havijakatazwa kutumia njia mbalimbali kupata Wanachama ili mradi shughuli zote zifanyike nje ya maeneo ya Chuo/Vyuo na kwa kufuata matakwa ya Sheria. Kuruhusu moja kwa moja harakati za kisiasa kufanyika Vyuoni kutaleta athari zikiwemo uvunjifu wa amani, kuathiri shughuli za kitaaluma. n.k. Napenda kusisitiza kuwa katika hili hakuna upendeleo wowote kwa Chama Tawala.
• Ili kudhibiti harakati za kisiasa katika maeneo ya Vyuo Vikuu, Sheria ndogo ndogo (By-laws) na Hati Idhini za Vyuo hivyo hutumika katika kudhibiti masuala ya kisiasa ambayo yanaweza kuleta athari na kuathiri masuala ya kitaaluma.
• Wanafunzi wanao uhuru wa kutoa maoni yao bila kubugudhiwa kwenye warsha, mikutano, kongamano na semina zinazofanyika katika maneo ya Vyuo.
Hoja: Vigezo vinavyotumiwa na Bodi ya Mikopo kutoa mikopo kuwa vinawapaendelea matajiri.
Jibu:
Mheshimiwa Spika,
• Vigezo vya utoaji mikopo havitoi mwanya wa upendeleo kati ya Watoto wanaotoka katika familia zenye vipato tofauti. Uchambuzi wa waombaji unafanywa na mfumo ambao unatoa majibu kulingana na taarifa alizojaza mwombaji mkopo bila kumwangalia mhusika usoni, dini au kabila lake. Hata Mwanafunzi anayekosa mkopo anapewa nafasi ya kukata rufaa kwenye Bodi ya Mikopo, na ikishindikana anayo nafasi ya kukata rufaa kwa Waziri mwenye dhamana ya Elimu.
• Tofauti ya kiasi cha mkopo anaopewa Mwanafunzi inategemea, pamoja na mambo mengine kama mwombaji anachukua programu ya kipaumbele cha Taifa pamoja na ukomo wa Bajeti.
Hoja: Bodi ya Mikopo imetumia gharama kubwa kununua mfumo wa uchambuzi wa utoaji mikopo ambao haujaleta tija hadi sasa.
Jibu:
Mheshimiwa Spika,
• Ni kweli kwamba Serikali kupitia iliyokuwa Wizara ya Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu, ilinunua mfumo wa utoaji mikopo kabla ya Bodi ya Mikopo kuanzishwa mwaka 2004/2005. Baada ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu kuanzishwa, ililazimika kuboresha mfumo huu ili kuzingatia changamoto zilizojitokeza kama vile wingi wa waombaji, mabadiliko ya mara kwa mara ya vigezo vya utoaji mikopo pamoja na programu za vipaumbele vya Taifa. Hata hivyo, mfumo huu umeleta mafanikio makubwa hasa kwa kuweza kupokea maombi, kuchambua, kupanga viwango vya mikopo na hatimaye kutoa mikopo kwa waliotimiza vigezo vyote vya kupewa mikopo.
Mfumo huu ambao kwa kiasi kikubwa unatumia “Online Loan Applicagtion System (OLAS)” umesaidia kuepuka kutumia makaratasi pamoja na kuokoa muda.
Hoja: Kuna ucheleweshwaji wa Mikopo kwa Wanafunzi waliopo Vyuoni jambo ambalo linasababisha migomo katika Taasisi za Elimu ya Juu.
Jibu:
Mheshimiwa Spika,
• Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu imejipanga kuhakikisha kuwa Wanafunzi wanapata mikopo kwa wakati kwa kushirikiana na wadau wote wakuu kama vile TCU, NACTE, Vyuo pamoja na Wanafunzi wenyewe. Wadau hawa wanatakiwa kuwasilisha taarifa sahihi na kwa wakati kwenye Bodi ya Mikopo ili utoaji wa mikopo uweze kufanyika kwa wakati. Kwa upande wa Serikali, tumejipanga kutoa fedha kwa wakati ili taratibu za utoaji mikopo ziweze kufanyika kwa wakati. Kuanzia mwaka wa fedha 2012/2013, Serikali imetoa fedha kwa muda muafaka na walengwa wameweza kunufaika na mikopo hiyo. Aidha, kila Chuo kimeajiri Afisa Mikopo ambaye ni kiungo kati ya Wanafunzi, bodi ya Mikopo na Menejimenti za Vyuo husika ili kuwezesha Wanafunzi kujikita zaidi kwenye masuala ya Kitaaluma badala ya kutumia muda wao kushughlikia mikopo.
Hoja: Kuna kasi ndogo ya urejeshwaji wa mikopo kutoka kwa wanufaika kwa vile Serikali na Bodi haikuzingatia ushauri wa Kambi ya Upinzani kwenye Bajeti ya 1012/2013.
Jibu:
Mheshimiwa Spika,
• Ushauri wa Kambi Rasmi ya Upinzani kuhusu utumiaji wa Mifumo ya Mawasiliano katika urejeshwaji mikopo umezingatiwa na Serikali pamoja na Bodi ya Mikopo. Kwa mwaka wa masomo 2012/2013, Bodi ya Mikopo imetumia mifumo hii (Tigo pesa, Airtel Money na M – Pesa) kulipia gharama za kutuma maombi ya Mikopo. Kwa mwaka wa masomo 2013/2014, Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu itatumia mifumo hii katika kurejesha fedha za walionufaika na mikopo. Mazungumzo yanaendelea kati ya Bodi, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa, Mamlaka za Mifuko ya Hifadhi za Jamii na TRA ili kuweza kuwabaini walionufaika na hivyo kuwa katika nafasi ya kuwabana kurejesha mikopo.
• Bodi vilevile, imeanza kuwafikisha Mahakamani wanufaika waliokaidi kurudisha mikopo baada ya kuhitimu na kumaliza “grace period”. Nitumie fursa hii, kuwasihi wote walionufaika na mikopo, kuwa na moyo wa uzalendo kuanza kurudisha mikopo badala ya kusubiri kutafutwa.
DAFTARI LA KUDUMU LA WAPIGA KURA
HOJA: Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa unaotegemewa kuletwa Bungeni kwa ajili ya kuufanyia marekebisho, usubiri hadi Katiba Mpya itakapokuwa imeanza kutumika.
JIBU:
Mheshimiwa Spika,
• Kwa kuwa shughuli za Vyama vya Siasa zinafanyika wakati wote ni vizuri Sheria hii ikafanyiwa Marekebisho bila kuathiri mfumo na taratibu zitakazoletwa na Katiba Mpya. Vilevile, kutokuleta marekebisho hayo kutadumaza demokrasia kwa kuingoja Katiba Mpya.
HOJA: Tume ya Taifa ya Uchaguzi iandae Daftari la Kudumu la Wapiga Kura litakalotumika kwa uchaguzi wa Wabunge huko Zanzibar.
JIBU:
Mheshimiwa Spika,
Kwa hivi sasa, Tume inazingatia Sheria ya Taifa ya Uchaguzi (Sura ya 343) iliyopitishwa na Bunge hili Tukufu inayoelekeza kuwa Tume itatumia Daftari lililoandaliwa kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi Zanzibar katika Uchaguzi wa Wabunge huko Zanzibar. Kwa msingi huo, Tume ya Taifa ya Uchanguzi hutumia Daftari lililoandaliwa na Tume ya Uchanguzi ya Zanzibar katika uchaguzi wa Wabunge huko Zanzibar.
TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI
HOJA: Tume ya Taifa ya Uchaguzi ina mpango wa siri wa kuandaa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa kutumia mfumo wa ‘biometric’. Mipango imeanza bila ya kushirikishwa Vyama vya Siasa.
JIBU:
Mheshimiwa Spika,
• Tume ya Uchaguzi haina mpango wa siri wa kuandaa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa kutumia mfumo wa ‘biometric’. Hata hivyo, Tume ipo katika hatua ya awali ya kuandaa Uboreshaji wa Daftari kwa utaratibu wa kawaida na Tume itawashirikisha wadau.
HOJA: Sheria gani inaruhusu uboreshaji wa Daftari la Wapiga Kura kwa njia ya ‘biometric’?
JIBU:
Mheshimiwa Spika,
• Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, inaipa Tume ya Uchaguzi mamlaka ya kuandaa na kurekebisha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa utaratibu/mfumo unaofaa.
• Kwa sasa Nchi karibu zote za SADC, Afrika Mashariki, Kati na Magharibi zinatumia mfumo wa ‘biometric’ na Nchi nyingine mbalimbali Duniani zinatumia mfumo wa ‘biometric’ katika kuandikisha wapiga kura na kuanzisha Daftari la Uraia. Uamuzi wa kutumia mfumo wa ”Biometric” au la utafanyika kwa uwazi na kwa kuwashirikisha Wadau wote ikiwa ni pamoja na kuifanyia marekebisho Sheria husika.
SALAAM ZA POLE KWA WATU WALIOPATA MAAFA NA AJALI
HOJA: Mheshimiwa Waziri Mkuu alieleze Bunge ni kwa nini kwenye Hotuba yake hakutoa pole kwa Watu walipoteza maisha kutokana na ajali za barabara na majini wakati Watu wengi wamepoteza maisha kutokana na ajali hizo.
JIBU:
Mheshimiwa Spika,
• Katika Hotuba yangu kwenye Aya ya 5 ukurasa wa 3 na 4 nimetoa Pole kwa Watu mbalimbali waliopatwa na matukio ya Majanga na Maafa mbalimbali yaliyojitokeza mwaka 2012/2013.
• Wakati nawasilisha Hotuba yangu Aya hiyo sikuisoma kutokana na makubaliano yetu hapa Bungeni ya kuongeza ufanisi katika kutunza muda.
SENSA YA WATU NA MAKAZI
HOJA: Serikali itekeleze ahadi yake Bungeni ya kuwalipa Posho Watendaji wa Mitaa, Vijiji na Vitongoji waliohusika kuwasaidia Makarani katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012.
JIBU:
Mheshimiwa Spika,
• Katika Makadirio ya Bajeti ya Sensa ya Watu na Makazi, malipo ya Wenyeviti wa Vijiji, Vitongoji na Mitaa hayakuwepo kwa kuwa hapo awali waliopangwa kufanya kazi ya kuwaongoza Makarani na Wasimamizi wa Sensa walikuwa ni Watendaji wa Kata (WEO) na Watendaji wa Vijiji na Mitaa (VEO). Hata hivyo, wakati wa Zoezi la Sensa ilionekana kuwa Wenyeviti wa Vijiji, Vitongoji na Mitaa ni muhimu wawepo kusaidia kuwaongoza Makarani na Wasimamizi wa Sensa.
• Viongozi hao walifanya kazi hiyo vizuri na walistahili kulipwa takriban Shilingi 4,292,501,555.
• Hivyo, katika Kikao cha Kamati Kuu ya Taifa ya Sensa ya Watu na Makazi kilichokutana tarehe 26 Machi 2013, Zanzibar kilijadili suala hilo na kuielekeza Wizara ya Fedha kuhakikisha kuwa malipo ya Wenyeviti wa Mitaa, Vijiji na Vitongoji walioshiriki katika zoezi la Sensa yanafanyika kabla ya mwisho wa mwaka huu wa fedha. Taratibu za kupata fedha hizo zinaendelea na Wahusika wote watalipwa.
HOJA: Serikali iwapatie Waheshimiwa Wabunge nakala ya Taarifa ya Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012 katika Mkutano wa Bunge la Bajeti. Aidha, Serikali itoe Taarifa ya Sensa ya Watu na Makazi ikionyesha wazi mchanganuo wa Idadi ya Watu Kimkoa.
JIBU:
Mheshimiwa Spika,
• Tarehe 5 Aprili, 2013 nilipata fursa ya kuzindua Ripoti ya Idadi ya Watu kwa ngazi za Utawala kuanzia ngazi ya Mkoa, Wilaya na Kata/Shehia.
• Ripoti hiyo ya kwanza ni moja kati ya Machapisho ya Sensa zaidi ya 18 yatakayotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu kuanzia mwezi Aprili, 2013 hadi Juni, 2014 kuonyesha mchanganuo wa Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya 2012.
• Serikali itaiagiza Ofisi ya Taifa ya Takwimu kusambaza kwa Waheshimiwa Wabunge wote Nakala za Taarifa mbalimbali za Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi kila mara zinapotoka. Nakala za Toleo la Kwanza la Taarifa za Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi zitasambazwa kabla ya mwisho wa Mkutano huu wa Kumi na Moja unaojadili Bajeti ya Serikali.
• Taarifa zenye mchanganuo wa Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi zitasambazwa kwa Wadau wote wa ndani na nje kwa kutumia Wavuti (Website) ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu na Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar. Aidha, Taarifa hizo pia zitasambazwa kwa Viongozi na Watendaji wa Mikoa, Wilaya na Halmashauri kupitia Kamati za Sensa ya Watu na Makazi za ngazi ya Mikoa na Wilaya.
MAKAZI BORA KWA ASKARI WA JESHI LA POLISI
Hoja: Serikali iwapatie Askari Polisi Makazi bora yenye staha hususan kwa kuanzisha mfuko wa ujenzi wa Nyumba za Askari
JIBU:
Mheshimiwa Spika,
• Serikali inaendelea kutekeleza Programu Endelevu ya Kuboresha Makazi ya Askari Polisi kwa kujenga nyumba mpya na kuzifanyia ukarabati zile zilizopo ili kuweza kukidhi mahitaji ya nyumba bora za kuishi kwa Askari wetu. Askari Polisi nchini wanahitaji jumla ya Nyumba 41,000 na Nyumba zilizopo ni 10,479 ambapo Nyumba 582 ni nzima na zingine zinahitaji matengenezo makubwa na madogo.
• Ili kukabiliana na uhaba wa nyumba za kuishi Askari Polisi Nchini, Serikali kuanzia mwaka 2006 hadi sasa imekamilisha kujenga jumla ya Nyumba 458 katika maeneo ya Dar es Salaam, Unguja, Pemba, Arusha, Mwanga (Kilimanjaro), Bahi (Dodoma) na Kigoma. Serikali pia, inaendelea na ujenzi wa Nyumba 76 za Polisi katika miji ya Mwanza, Bukoba, Musoma, Kwimba na Ludewa.
• Aidha, Serikali inatarajia kuanza kujenga Nyumba 350 za Polisi katika eneo la Osterbay, Jijini Dar es Salaam pamoja na kufanya mazungumzo na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China ili kupata mkopo nafuu utakaofanikisha ujenzi wa nyumba nyingi maeneo mbalimbali Nchini.
• Katika Mpango wa Muda Mrefu, Serikali imepanga kutumia utaratibu wa PPP kujenga makazi bora ya Askari wetu na kuongeza Bajeti ya maendeleo kwa Jeshi la Polisi kila mwaka ili kukabiliana na mahitaji ya nyumba na Ofisi.
• Katika mwaka 2013/2014, Bajeti iliyotengwa kwa Miradi ya Maendeleo pamoja na ujenzi wa Nyumba ni jumla ya Shilingi Bilioni 8.
• Aidha, Jeshi la Polisi limeanzisha Shirika la Uchumi – The Corporation Sole (Police Force) kwa tangazo la Serikali Namba 66 la tarehe 29 Machi, 2013. Shirika hilo pamoja na masuala mengine, litalijengea uwezo Jeshi la Polisi katika kutekeleza Mikakati na Programu mbalimbali ya muda mfupi na mrefu ikiwa ni pamoja na kujenga nyumba za makazi, Vituo na Ofisi za Polisi Nchini.
Hoja: MASUALA YA UDINI, AMANI NA UTULIVU
JIBU:
Mheshimiwa Spika,
• Suala la Udini na Amani na Utulivu limezungumziwa kwa kirefu katika hotuba ya Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika hotuba yake kwa Wananchi ya tarehe 31 Machi, 2013. Tumefika mahali ambapo kama Viongozi na Waumini wa dini kusisitiza umuhimu wa Waislamu na Wakristo kuishi pamoja kidugu, kwa upendo, ushirikiano na kuvumiliana vinginevyo Nchi yetu itaacha kuwa kisiwa cha amani na kuingia katika orodha ya Nchi zenye migogoro na hata vita vya wenyewe kwa wenyewe. Hatutaki kufikia hatua hiyo kwa namna yoyote ile. Ni lazima sote tulivalie njuga suala hili kuhakikisha kwamba Nchi yetu inaendelea kuwa na mshikamano na upendo kati ya Waislam na Wakristo.
• Aidha, katika siku za hivi karibuni kumejitokeza matukio mbalimbali yanayoashiria uvunjifu wa hali ya amani na utulivu Nchini. Katika maeneo mengi kumeibuka chokochoko za kidini ambazo zimeleta madhara makubwa.
• Vilevile, kutokana na Uhuru na Demokrasia pana iliyopo, baadhi ya Wanaharakati na Vyama vya Siasa wamekuwa wakihamasisha Wanachama wao kuendeleza vitendo vya uvunjifu wa amani na kujenga chuki na uhasama miongoni mwa Jamii na kwa Serikali halali iliyopo Madarakani. Mmeshuhudia katika maeneo mengi kuna baadhi ya Watu hasa wale wa Vyama vya Siasa ambao badala ya kueleza Sera za Vyama vyao na kuhamasisha maendeleo, wao wanataka kubomoa Umoja wa Taifa letu kwa kuendeleza Vitendo vya uvunjifu wa amani na utulivu. Vitendo hivyo ni pamoja na kufanya maandamano kinyume cha Sheria, na kuitisha mikutano ya kutukana, kubezana, kushutumiana na kuzomeana. Chokochoko hizi si dalili nzuri kwa mustakabali wa Nchi yetu inayopenda kudumisha amani na utulivu.
• Serikali iliyopo Madarakani inayo dhamira njema ya kujenga Umoja wa Kitaifa, Mshikamano, Amani na Utulivu. Hii ni kwa sababu tunatambua kuwa Amani na Utulivu uliopo Nchini ni mazingira wezeshi ya kusaidia kila mmoja wetu kufanya shughuli zake za kijamii na kiuchumi na kujiletea maendeleo. Bila Amani na Utulivu hakuna maendeleo ya kweli ya Wananchi wetu.
• Natoa Wito kwa Viongozi wote wa Vyama vya Siasa kuacha tabia ya kuchochea Wananchi kwa kisingizio cha nguvu ya Umma badala yake kuhimiza suala la kupitia Kamati za Ulinzi na Usalama.
• Katika muda si mrefu, tumepanga kukutana na Viongozi na Wadau mbalimbali katika Mikoa/Wilaya ikiwemo Vyama vya Siasa, Madhehebu ya Dini, Vyombo vya Habari, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, Wanataaluma; Viongozi wa Wazee, Viongozi wa Makundi ya Vijana, n.k. kuzungumzia suala hili na kuchukua hatua za kudumisha Umoja wa Kitaifa na Amani na Usalama Nchini.
• Aidha, Serikali itaendelea kuwaelimisha Wananchi wote kuzingatia na kuheshimu Utawala Bora wa Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo na hususan ‘Utii wa Sheria Bila Shuruti’ ili kudumisha Amani na Utulivu tuliojijengea kwa muda mrefu.
• Nirudie kuwakumbusha tena Wakuu wa Mikoa na Wilaya na Wakuu wa Vyombo vya Usalama kutekeleza Agizo la Mheshimiwa Rais kwa kuacha ajizi katika kutimiza wajibu wao kwenye suala la ulinzi na usalama. Tuhakikishe kamba Nchi yetu inabaki na amani na utulivu ili Wananchi wetu waendelee kufanya shughuli za maendeleo. Serikali pia inawahakikishia kuwachukulia hatua kali wale wote wanaotumia udini kwa maslahi ya vyama vyao ili kudumisha amani na utulivu Nchini.
HITIMISHO:
Mheshimiwa Spika,
• Kama nilivyosema, hoja ni nyingi. Pamoja na kurekebisha Kanuni zetu bado hatuwezi kumaliza kuzijibu hoja zote kwa muda huu niliopangiwa. Baadhi ya hoja hizo zitajibiwa na Wizara za Kisekta wakati wa kuwasilisha Hotuba zao za Bajeti.
• Nawashukuru sana!
• Naomba kutoa hoja!