Maelezo Kusimamia Mkakati wa Taarifa za Utekelezaji wa Ahadi za Serikali

Mkurugenzi Idara ya Habari-MAELEZO, Hassan Abbasi.

Mkurugenzi Idara ya Habari-MAELEZO, Hassan Abbasi.

MKAKATI WA KUWAELEZA WANANCHI UTEKELEZAJI WA AHADI ZA SERIKALI

SERIKALI kupitia Idara ya Habari-MAELEZO itaanza kutekeleza mikakati mbalimbali inayolenga kuwapatia wananchi taarifa za kila mara kuhusu utekelezaji wa ahadi zake. Mikakati hiyo itakayosaidia kuongeza uwazi na ushirikishaji, pamoja na mambo mengine, itahusisha hatua zifuatazo:-

Mosi, kuboresha mfumo wa mawaziri na watendaji waandamizi Serikalini kuzungumza na wananchi ili kuainisha utekelezaji wa vipaumbele vya bajeti, sera na mipango ya Taifa. Kuanzia Agosti 25 mwaka huu, mawaziri wataanza kuzungumza na umma kupitia vyombo vya habari kueleza vipaumbele vya bajeti zao na utekelezaji wake hadi kufikia sasa.

Pili, kuanzisha utaratibu wa Idara ya Habari-MAELEZO kueleza kwa umma kila mara, na haraka iwezekanavyo, utekelezaji wa sekta zote katika ngazi ya kitaifa. Msemaji Mkuu wa Serikali atakuwa akitoa taarifa hizo kuanzia hivi karibuni.

Tatu, Serikali itaimarisha ushirikiano zaidi na wadau mbalimbali katika kutekeleza mikakati yake ya mawasiliano kwa umma. Pamoja na wadau wengine, Serikali itahakikisha inafanyakazi kwa karibu na vyombo vya habari ili vishiriki vyema katika ujenzi wa Taifa.

Mwisho, wakati huu Idara ikiendelea kufanyiakazi mikakati mingine ili kuboresha mawasiliano kwa umma, naomba wadau wote kutoa ushirikiano kwangu binafsi, Idara niliyopewa kuiongoza hivi karibuni na zaidi tumuunge mkono Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli katika ajenda yake ya mageuzi kupitia HapaKaziTu.

Imetolewa na:

Hassan Abbasi,
Mkurugenzi Idara ya Habari-MAELEZO.