Na Mwandishi Wetu, Arusha
KATIKA hali ya kushangaza madiwani watatu waliotimuliwa uanachama ndani ya Chama Cha Maendeleo na Maendeleo (CHADEMA), na kuvuliwa nafasi zao za udiwani leo wamevamia mkutano bila ya kualikwa na kutaka kuhudhuria mkutano huo.
Madiwani hao John Bayo, Rehema Mohamed (Viti maalumu) na Estomii Mallah wamefanya tukio hilo katika mkutano uliofanyika Ukumbi wa Polisi mjini Arusha (Police Mess) wakati mkutano wa wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Arusha. Mkutano huo uliokuwa ukimtambulisha Mkuu wa Mkoa mpya uliwahusisha wakuu wa idara, wataalam wa Manispaa ya Arusha, madiwani, vingozi wa dini, taasisi za Serikali na asasi zisizokuwa za kiserikali na viongozi wa mitaa ya manispaa hiyo.
Hata hivyo tukio la uvamizi wa madiwani hao limefanyika ikiwa ni siku chache tangu Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha, kutupilia mbali kesi ya madai namba 17/2011 iliyofunguliwa na madiwani hao pamoja na wezao wakipinga kuvuliwa uanachama ndani ya CHADEMA.
Madiwani hao walifika mkutanoni hapo, pasipo kualikwa na waliingia mkutanoni na kujitambulisha kwa nafasi zao walizovuliwa jambo ambalo lilizua minong’ono kwa washiriki wengine wa mkutano huo, huku wengine wakicheka kwa kituko hicho.
Hata hivyo mtandao huu ulipotaka ufafanuzi kutoka kwa Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Estomii Chang’a, alisema naye ameshangazwa na uwepo wa watu hao kwani hawatambui na walishafukuzwa. Alisema hawatambui kwa kuwa mahakama imetupilia mbali ombi lao walilokuwa wamelifikisha mahakamani na kutoa uamuzi kuwa wameshavuliwa nyadhifa zao za udiwani. Aliongeza hata katika barua za mualiko wa mkutano huo hakuwaita.
Mmoja wa madwani hao John Bayo alipotakiwa kuonesha barua ya mwaliko aliyopewa na manispaa aligoma huku akidai kuwa uamuzi uliotolewa na mahakama bado haujawasilishwa kwa mkurugenzi hivyo wao bado ni madiwani.
Hata hivyo mtandao huu ulipotaka ufafanuzi kutoka kwa Msajili wa Mahakama wa Wilaya Kanda ya Arusha, George Hurbet alisema si jukumu la mahakama kupeleka nakala ya hukumu kwa mkurugenzi, bali Manispaa ndiyo inayotakiwa kwenda kufuata nakala hiyo mahakamani.