Kilwa
MADIWANI wa halmashauri mbalimbali za Mkoa wa Lindi wameishauri Serikali kubadili mfumo wa malipo kwa viongozi hao kutoka kulipwa posho na kuanza kulipwa mishahara ili nao waweze kukopeshwa katika taasisi za fedha, kama ilivyo kwa watumishi wengine.
Ombi hilo limetolewa juzi na madiwani hao kwenye mkutano wa Jumuia ya Tawala za Mitaa (ALAT), tawi la Lindi uliofanyika hivi karibuni kwenye ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Kilwa.
Wakichangia katika mkutano huo madiwani hao wamedai kuwa utaratibu wa kulipwa fedha zao kwa mfumo wa posho badala ya mishahara unawafanya washindwe kupata sifa ya kupewa mikopo, kutoka taasisi anuai za fedha jambo ambalo linawafanya wawe na hali ngumu kimaisha.
“Huu mfumo wa madiwani kupewa malipo yetu ya kila mwezi kama posho badala ya mishahara unatunyima fursa muhimu za kupata mikopo, mara zote tunaambiwa hatupo katika mfumo wa ajira kama walivyokuwa wenzetu wabunge,” Walisikika wakisema wajumbe hao.
Hata hivyo wajumbe hao katika majumuisho yao waliiomba Serikali kupitia Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kuwaongezea kiwango cha fedha wanachopata kwani hakikidhi mahitaji huku gharama za maisha zikiendelea kupanda kila uchao.
Akijibu hoja hizo kwa niaba ya wabunge wenzake Tanzania, mbunge wa Jimbo la Kilwa Kusini, Selemani Bungara kutoka Chama cha Wananchi (CUF), alisema amelipokea ombi hilo na ameahidi kulifikisha kunakohusika ili kuona uwezekano wake.
“Sisi wabunge wote, hasa wa kambi ya upinzani tatizo la kulipwa posho ndogo, tunalifahamu na kwa namna moja au nyingine uwa tunalifikisha kunakohusika, lakini hatujafahamu mahali inapokwama,” alisema Bungara.
Bungara aliongeza kuwa hoja hiyo alisema mbunge pekee hawezi kufanya vema majukumu yake bila kushirikiana na madiwani waliopo kwenye maeneo yake, hivyo kitendo cha kulipwa posho ndogo hata wao kinawasikitisha mno.