Madiwani: Serikali itueleze Mwakyembe anaumwa nini

Dr. Harrison Mwakyembe

Baadhi ya Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyela pamoja na wazee maarufu wa mji Kyela mkoani Mbeya, wamekutana kujadili suala la ugonjwa unaomsumbua Mbunge wao, Dk. Harrison Mwakyembe, na kutoa tamko la kuitaka serikali ieleze kinachomsumbua.

Katika mkutano huo uliofanyika jana katika viwanja vya Siasa mjini hapa, viongozi hao wamefikia hatua hiyo ya kuitaka serikali itoe tamko baada ya kuibuka kwa malumbano ya viongozi wakiwemo mawaziri kuhusu utata juu ya ugonjwa unaombua Dk. Mwakyembe.

Taarifa kutoka katika kikao hicho zimeeleza kuwa, madiwani hao wapatao saba na wazee hao wameitaka serikali kutoa kauli inayoeleweka kwani tangu kuugua kwa Dk. Mwakyembe viongozi wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Wizara ya Mambo ya Ndani na Jeshi la Polisi wamekuwa wakitoa taarifa zinazokinzana na hivyo kuzua utata kwa wananchi.

Hadi tunakwenda mitamboni jana mkutano wa madiwani na wazee hao ulikuwa bado unaendelea na wameahidi kutoa maazimio waliyoayafikia leo kwa vyombo vya habari.

Tangu kuugua kwa Dk. Mwakyembe Oktoba mwaka jana kumekuwa na utata ni ugonjwa gani unaomsumbua huku kukiwa na madai kuwa amelishwa sumu.

Hata hivyo taarifa za kwamba Dk. Mwakyembe alilishwa sumu zilikanushwa na Mkurugenzi wa Upelelezi Makosa ya Jinai, Kamishna Robert Manumba.

Manumba akizungumza na waandishi wa habari, alisema uchunguzi uliofanywa na jeshi hilo na kupata taarifa kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ugonjwa unaomsumbua Dk. Mwakyembe hautokani na kulishwa sumu.

Hata hivyo siku moja baada ya Kamishna Manumba kukanusha madai juu ya Dk. Mwakyembe kulishwa sumu, Naibu Waziri huyo alilishambulia Jeshi la Polisi kwa kueleza kuwa lina ufinyu wa uelewa.

Dk. Mwakyembe alisema kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari kuwa sumu si lazima mtu anyweshwe ili imdhuru wakati inaweza kudhuru hata kwa kugusishwa tu.

Alisema Jeshi la Polisi limejiingiza kwenye suala ambalo kwa takriban mwaka mzima halijawahi kuwa na dhamira ya dhati ya kulielewa au kulichunguza mbali na kulifanyia mzaha kupitia magazetini.

Dk. Mwakyembe alisema msimamo huo wa Jeshi la Polisi umemkera sana hasa kutokana na hali aliyonayo ya ugonjwa, kwanza kwa kuingilia mchakato wa matibabu yake na uchunguzi wa kina kuhusu kiini cha kuumwa kwake unaoendelea kufanywa katika Hospitali ya Apollo nchini India, ambako bado hajahitimisha matibabu yake.

Kauli ya Manumba pia imekwepwa na mawaziri wawili, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Haji Mponda na Waziri wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha, ambao wametaka Manumba aulizwe alikopata taarifa kuhusu sumu ya Dk. Mwakyembe.

CHANZO: NIPASHE