BAADHI ya madiwani wa Halmashauri ya Kongwa wametishia kujiondoa kwenye mfuko wa Bima ya Afya ya Taifa baada ya kutoridhishwa na utaratibu uliowekwa na Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF).
Wakizungumza kwenye semina kabla ya kuanza kwa kikao cha madiwani katika Halmashauri hiyo, madiwani hao walidai utaratibu wa mfuko huo ni mgumu kutokana na kutoza fedha nyingi kwa ajili ya matibabu.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Nghumbi, Sina Munde alisema madiwani hutakiwa kuchangia kiasi cha asilimia sita, ambapo kati ya asilimia hizo halmashauri huchangia asilimia tatu na kusema kuwa kiasi kikubwa na hivyo kushindwa kumudu.
Alisema madiwani wamekuwa wakichangia fedha nyingi kiasi ambacho hakilingani na kipato chao hivyo ni bora wajiondoe na kujiunga kwenye mifuko mingine inayotoa huduma hizo ambayo ni nafuu.
Alisema kwa mwaka wamekuwa wakichangia sh. 82,000, ambapo wao hutoa sh. 41,000 na halmashauri huwachangia sh. 41,000. Aliongeza licha ya wao kuchangia fedha hizo wamekuwa wakilazimika kununua dawa mara wanapokwenda kutibiwa katika hospitali ambazo mfuko huo upo lakini hujibiwa dawa zimeisha.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Mtanana, Joel Musa ameutaka Mfuko huo wa Bima ya Afya uwarejeshee fedha zao zilizopo katika mfuko huo kwani hawaridhishwi na utaratibu mzima wa huduma ya afya ambao umekuwa ukitolewa.
Akijibu hoja hizo Meneja wa Kanda ya Kati wa mfuko huo, Emanuel Adina alisema mfuko huo umewekwa kwa mujibu wa Sheria ya Bunge namba nane ya Mwaka 1999 huku akidai madiwani hao hawawezi kujiondoa katika mfuko huo kwani sheria sio hiari bali ni lazima.