Jengo la Halmashauri ya Chato
Chato
SAKATA la madiwani katika Halmashauri ya wilaya ya Chato mkoani Kagera
la kugoma kuingia kwenye kikao cha Baraza limeingia sura mpya baada ya
baadhi yao kujitenga na kuunda Baraza jipya la muda pamoja na kumchagua
Mwenyekiti wa Halmashauri.
Katika kikao kilichofanyika juzi mjini Chato madiwani hao 14 kutoka
chama cha mapinduzi CCM kwa kushirikiana na wale wa chama cha Demokrasia
na Maendeleo CHADEMA walimchagua, Elias Malando Diwani wa Kata ya
Katende kuwa mwenyekiti wao wa muda.
Aidha madiwani hao katika kikao cha Baraza kilichopita waligoma kuingia
kwenye Baraza wakimtuhumu mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri hiyo Hamida
Kwikwega amewaburuza kwa kushindwa kuwapa makabrasha mapema pia na
kushindwa kutoa ufafanuzi juu ya matumizi mabaya ya ujenzi wa mabwawa
ya maji yaliyojengwa chini ya kiwango.
Kufuatia hali hiyo madiwani hao 14 waligoma kuingia na kuwaacha wenzao
12 chini ya Mwenyekiti wa Halmashauri, Maisha Charles diwani wa Kata ya
Kigongo kuendelea na kikao hicho ambacho walikipinga wakidai ni batili
kwa sababu kiliendeshwa chini ya idadi ya theluthi tatu kama ilivyo
kwenye mwongozo wa vikao vya Halmashauri.
Pamoja na madiwani hao kuendesha kikao hicho chini ya mwenyekiti wao
wenzao waliogoma kuingia nao waliendesha kikao chao nje ya ukumbi baada
ya kumchagua mwenyekiti wao na kupitisha maadhimio ya kumkataa
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri na kukataa maadhimio yao
waliyoyapitisha kwenye kikao hicho.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Chato alipotakiwa kuzungumzia hali
hiyo alikiri madiwani hao kukataa kuingia kwenye kikao na baada ya
kugoma waliobaki waliendelea na chini ya Mwenyekiti Charles.
Hata hivyo Kwikwega alisema madiwani hao huenda wakawa na madai ya
msingi kwa kuwa ni wawakirishi wa wananchi huku akisisitiza zaidi wapewe
mafunzo ya kujua sheria za utawala katika halmashauri hali ambayo
itaondoa migogoro isiyokuwa ya lazima.
Pia katika madai ya madiwani waliogoma ni pamoja na Halmashauri hiyo
kupewa hati ya mashaka kutokana na ubadhilifu wa matumizi ya fedha na
tayari katika barua yao ya maadhimio ya kumkataa mkurugenzi huyo
wameambatanisha malalamimko yote kwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera na nakala
yake kuipeleka ofisi ya TAMISEMI.
Mkuu wa mkoa wa Kagera, Mohamed Babu akizungumza kwa njia ya simu na
gazeti hili alikiri kupokea kwa malalamiko hayo na kuongeza kuwa
amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Chato, Hadija Nyembo afuatilie na kumpa
taarifa kamili kwa maandishi ili aweze kulifanyia kazi tatizo hilo.
Baadhi ya madiwani waliogoma kuingia kwenye kikao na kuunda baraza lao
akiwemo Diwani wa Kata ya Bwela, Elam Lubagola pamoja na diwani wa Kata
ya Ilemela, Ismail Ruge wametishia kuachia madaraka kwa kujivua gamba
iwapo wataendelea kupingwa wakati wakitetea maslahi ya wananchi.