Madereva wasusia ushuru wa Manispaa ya Moshi

Daladala Mjini Moshi

Na Mwandishi Wetu, Moshi

MADEREVA wa magari madogo na makubwa wa Kituo Kikuu cha Mabasi mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro wamekataa kulipa ushuru mpya uliopangwa na Halmashauri ya Manispaa ya Moshi kitendo ambacho kimesababisha manispaa kukosa mapato kutoka kituo hicho kwa zaidi ya mwezi.

Kwa mujibu wa mazungumzo yao kwa wanahabari madereva hao wamesema hawako tayari kulipa ushuru huo wa sh. 1,500 kwa magari madogo na 2,000 kwa magari makubwa kwa madai kuwa ongezeko hilo ni kubwa ikilinganishwa na hali halisi ya kipato.

Kwa hali hiyo hali ya ukusanyaji ushuru katika kituo hicho imekuwa ngumu kutokana na baadhi ya magari machache tu yanayokubali kulipa ushuru wakati idadi kubwa ya madeva wakiwa katika mgomo kabisa.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi, Bernadetha Kinabo amethibitisha kuwepo kwa tatizo hilo na kutupa lawama kwa msimamizi wa kituo hicho na kwamba kwa sasa halmashauri inafanya taratibu za kumuondoa hivyo kuwataka madereva watii sheria za halmashauri.

Alisema madeva hao kukwepa kulipa ushuru ni kinyume cha sheria iliyopaswa kuanza kutekelezwa Julai Mosi mwaka huu na kwamba hali hiyo inakwamisha mipango ya utekeleza wa maendeleo katika Mji wa Moshi ikiwemo miundombinu ya barabara.

Aliongeza kuwa madereva na wamiliki wa magari hayo wanapaswa kulipa ushuru huo kwa kuwa ushuru uliokuwapo wa sh. 1000 ulidumu kwa takribani miaka 10 bila kubadilishwa.

Sakata la mgogoro wa Ushuru wa magari madogo na baadhi ya magari makubwa yanayofanya safari zake katika maeneo mbalimbali mkoani Kilimanjaro na Arusha ulianza Julai Mosi mwaka huu hali ambayo ilitokana na kupandishwa kwa ushuru kutoka Sh. 1,000 hadi 1,500 kwa magari madogo na sh. 2,000 kwa magari makubwa.

Hivi karibuni baraza la madiwani la manispa hiyo lilikaririwa likimtmata mkurugenzi wa manispaa hiyo kumwajibisha msimamizi wa stendi kwa kushindwa kuiotetea halmashauri hiyo pindi sheria ya ushuru ilipopitishwa.