Na Janeth Mushi, Arusha
JOPO la waendesha pikipiki maarufu kama “bodaboda” mkoani hapa wameteketeza gari kwa moto baada ya gari hilo kumsababishia kifo dereva mwenzao baada ya kugongwa na kufariki papo hapo.
Tukio hilo limetokea mjini hapa Agosti 13 mwaka huu majira ya saa 1:30 jioni katika eneo la Sakina mkoani Arusha. Tukio hilo lililihusisha gari namba T 123 AAW aina ya Landa Cruiser Prado lililokuwa likiendeshwa na Eva Deus (45), likitokea Arusha mjini kuelekea Sakina.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio walisema gari hilo lilipofika katika eneo la Arusha Meat Njia Panda ya Majengo ghafla pikipiki iliyokuwa na namba za usajili T 172 BLM aina ya TOYO ikielekea Majengo Juu.
Pikipiki hiyo iliyokuwa ikiendeshwa na Ntoba Bakari (38) akiwa na abiria aliyejulikana kwa jina la Laurance Lema waligongana na gari lingine ambapo katika kujiokoa dereva huyo alijikuta akidondoka katika uvungu wa gari hilo ambalo lilimkanyaga na kumsababishia kifo huku abiria wake akinusurika baada ya kuruka kutoka kwenye pikipiki hiyo.
Akizungumzia tukio hilo, Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani hapa, Safu Buhatwa alisema baada ya ajali hiyo madereva wa pikipiki kutoka maeneo mbalimbali ya jiji la Arusha walifika katika eneo la tukio na kuanza kumshambulia kwa mawe dereva wa gari hilo (Eva).
Buhatwa alisema kuwa dereva huyo ambaye alikuwa na mumewe aliyefahamika kwa jina la Deus Kamazima (51) mfanyabishara ambaye alifanikiwa kumwokoa mkewe mikononi mwa kundi hilo na kukimbilia kituo kidogo cha polisi cha Sakina.
Alisema baada ya dereva huyo kukimbilia kituo kidogo cha polisi madereva hao waliliteketeza gari hilo kwa kulichoma moto ambalo thamani yake haijaweza kufahamika mara moja.
Alisema jeshi hilo linaendelea na upelelezi juu ya tukio hilo ikiwa ni pamoja na kuweza kuwakamata watuhumiwa waliohusika na tukio hilo ili waweze kufikishwa katika vyombo vya sheria na mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya mkoa wa Arusha Mt. Meru.