VIONGOZI wa nchi tajiri, G20 wanakutana nchini Ufaransa wakiwa na hofu kuu kuhusu athari za mzozo wa madeni barani Ulaya kwa uchumi wa dunia.
Mkutano huo unafanyika siku moja baada ya viongozi wa umoja wa ulaya kusimamisha misaada ya euro bil. 8 kwa Serikali ya Ugiriki hadi matokeo ya kura ya maoni kuhusu mpango wa kunusuru uchumi wa nchi hiyo yajulikane.
Waziri mkuu wa Ugiriki George Papandreou amesema kura hiyo ndio itakayoamua ikiwa nchi yake itaendelea kuwa kwenye umoja wa sarafu moja au eurozone. Kura hiyo ya maoni itafanyika December tarehe 4 na 5. Serikali ya China nayo imekataa kuwekezea fedha zake kwenye mfuko uliobuniwa wa kuimarisha uchumi wa ulaya hadi hatma ya Ugiriki ijulikane.
Rais wa Marekani Barack Obama amepanga kukutana na mwenzake wa Ufaransa Nicolas Sarkozy ambapo watajadili kwa kina mzozo huo.
Naye Chansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema viongozi wa umoja huo wanapendelea serikali ya Ugiriki iendelee kuwa mwanachama wa umoja huo wa sarafu na kuwa uamuzi wa utawala huo unatishia kuyumbisha umoja huo.
“Naamini kuwa raia wa Ugirki wameafikiana kuhusu suala hili na hivi karibuni sauti yao itasikika” alisema waziri mkuu George Papandreou baada ya mkutano wa dharura na Rais Sarkozy na Bi Merkel.
Wadadisi wa masuala ya kiuchumi wanasema ikiwa raia wa Ugiriki watapiga kura ya kuondoka kwenye umoja huo wa sarafu huenda nchi zingine wanachama kama vile Ureno na Ireland zikafuata mkondo huo.
Hali hii wanasema wadadisi, itazua taharuki kwenye sekta ya mabenki na uwekezaji barani Ulaya.
-BBC