MADAKTARI, WAUGUZI WATAKIWA KUOKOA MAISHA YA WAGONJWA

Mke wa Rais na Mwenyekiti wa Taasisi ya WAMA mama Salma Kikwete(aliyevaa baibui) akiwa na mke wa Rais wa Comoro mama Hadija Aboubacar Ikililoi Dhoinine (kulia) wakipata maelezo kutoka kwa waziri wa afya wa Comoro Mwanafuraha Mohammed (wa tatu kutoka kulia) kuhusu mtoto ambaye yuko chini ya uangalizi wa madaktari baada ya kuzaliwa katika Hospitali ya Rufaa ya El Maarouf mjini Moroni Comoro - June 28/2011, Picha na Mwanakombo Jumaa- MAELEZO.

Na Aron Msigwa – MAELEZO

28/6/2011, Moroni, COMORO

Madaktari na wauguzi wametakiwa kufanya kazi kwa bidii na kujituma ili kuokoa maisha ya wagonjwa wanaowahudumia. Wito huo umetolewa leo na Mke wa Rais na Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alipotembelea wodi ya watoto katika hospitali ya Rufaa ya El Maarouf iliyoko mjini Moroni nchini Comoro kuona namna huduma za afya zinavyotolewa kufuatia mwaliko wa mke wa Rais wa nchi hiyo Bi. Hadija Aboubacar Ikililoi Dhoinine.

Amesema wataalam wa Afya wana dhamana kubwa ya maisha ya wagonjwa wanaowahudumia huku akisisitiza umuhimu wa madaktari na wauguzi kutoa huduma za afya kwa watoto wadogo kutolewe kwa uangalifu, umakini na kwa kuzingatia umri walionao.

“Napenda kusisitiza kuwa huduma za afya kwa watoto ni za msingi sana katika taifa lolote lile,ukiboresha afya za watoto ina maana unakuwa na taifa lenye afya bora hali inayopelekea kuwa na taifa lenye viongozi bora wa baadaye”

Amefafanua kuwa nchini Tanzania kupitia Taasisi anayoiongoza ya Wanawake na Maendeleo(WAMA) suala la afya kwa watoto ni moja ya jukumu linalopewa kipaumbele na kusifu juhudi zinazofanyika kuwaokoa watoto walio chini ya miaka mitaano nchini Comoro.

Ameongeza kuwa nchini Tanzania taasisi ya WAMA kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta ya afya inashiriki kikamilifu katika kutoa elimu kwa wanawake na watoto dhidi ya maambukizi ya Virusi vya Ukimwi na kuhakikisha kuwa watoto wadogo wanaozaliwa wanakuwa salama.

“ Lazima tukubali kuwa eneo la watoto ni nyeti sana na tuna kila sababu ya kufanya kila juhudi kuhakikisha kuwa watoto wanaozaliwa hawafi mara tu baada ya kuzaliwa huku tukitekeleza malengo ya milenia ambayo nchi zetu zinayatekeleza yakiwemo upunguzaji wa vifo vya akina mama na watoto pamoja na mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi” amesema mama Salma.

Aidha amefafanua kuwa juhudi zaidi zinahitajika katika nchi zinazoendelea kuhakikisha kuwa watoto wadogo wanaozaliwa wanalindwa kwa kuwapatia mahitaji muhimu ya kiafya ikiwemo uzuiaji wa vifo vya watoto wadogo na utoaji wa elimu kwa wanawake kuhusu uzazi salama na uzingatiaji wa matumizi ya vituo vya afya pale wanapoona dalili hatarishi kwa watoto wao.

Kwa upande wake mke wa Rais wa Comoro Bi. Hadija Aboubacar Ikililoi Dhoinine amefurahishwa na ziara ya mama Salma Kikwete hospitalini hapo na kueleza kuwa ujio wake nchini humo utaendeleza zaidi uhusiano wa muda mrefu uliokuwepo kati ya Tanzania na Comoro huku akibainisha kuwa sekta ya afya katika nchi yake inaendelea kupiga hatua licha ya kukabiriwa na vikwazo mbalimbali.

Naye mganga mkuu wa wodi ya watoto katika hospitali hiyo Dkt. Said Hassani amesema kuwa idara yake itaendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuboresha afya za watoto na kupunguza vifo vya watoto wanaozaliwa na wale walio chini ya miaka mitano huku akiomba uhusiano kati ya nchi ya Tanzania na Comoro katika sekta ya afya uendelee kudumishwa zaidi.