TIMU ya madaktari wa watoto katika hospitali ya rufaa ya Bugando wameungana ili kuokoa maisha ya mapacha walioungana. Mapacha hao wamezaliwa na Elena Paulo, mwenye umri wa miaka 20, Januari 3, mwaka huu katika hospitali ya hospitali ya mkoa ya Mara na baadaye kuhamishiwa katika hospital ya rufaa ya Bugando mkoani Mwanza kwa ajili ya matibabu zaidi. Watoto hao walikuwa na uzito wa kilo 4.6 kwa pamoja wakati walipozaliwa na walikuwa wameungana vifua na matumbo.
Kwa mujibu wa Dk. Festo Manyama, daktari wa watoto hospitali ya rufaa ya Bugando, timu ya madaktari wa upasuaji na wataalamu wengine wamekusanyika kuamua namna bora ya kukabiliana na hali yao. “tunafanya kila liwezekanalo katika uwezo wetu ili kuokoa maisha ya watoto hawa,” alisema.
Alisema kabla ya upasuaji, mapacha hao walitakiwa kupitia tomografia (CT) na kufanya kipimo kijulikanacho kama Ultra sound ili kujua kama watoto hao wameungana baadhi ya maeneo na viungo muhimu.
“Tumeshafanya kipimo cha Ultra Sound na kupata matokeo yanayoonyesha kuwa hakuna sehemu nyingine muhimu walizoungana, lakini tunahitaji kufanya vipimo vingine kwa kutumia mashine ya CT scan, ambayo itatupatia hitimisho, “alisema Manyama.
Alisema madaktari wataweza kufanya upasuaji endapo watoto hao hawatakuwa wameungana sehemu muhimu katika miili yao.
Kwa mujibu wa Dk Manyama, watoto hao wawili wanahitaji ufuatiliaji wa karibu wa daktari ili waweze kuepukana na magonjwa. “tuwapa dawa na kuwalinda na magonjwa ya kuambukiza, pia wanatumia mashine ya oksijeni kwa kupumua na mirija ya chakula,” anaongeza Dr Manyama.
Aliongeza kuwa uongozi wa hospitali hii inatazamia kutoa rufaa ili watoto hawa wapelekwe Hospitali ya Taifa Muhimbili. “Tutawahamishia hospitali ya muhimbili kwa sababu hospitali yetu haina uwezo mkubwa wa kukabiliana na kesi hii, lakini kwa wakati tunafanya kila tuwezalo ili kuokoa maisha yao.” Alisema.
Mama wa mapacha hao, Bi Elena Paulo aliwaomba serikali kumuunga mkono ili kuhakikisha watoto wake wanapata huduma ya afya bora inayohitajika katika hali yao.
“Hofu yangu kubwa ni kwamba hospitali zetu hawataweza kukabiliana na hili, nimeambiwa upasuaji unaweza kufanyika nje ya nchi na Mimi ni mama maskini hivyo ninaomba serikali inisaidie”, alisema.
Tanzania imekuwa ikishuhudia matukio kadhaa ya mapacha walioungana katika miaka ya hivi karibuni.
Mwishoni mwa mwaka jana hospitali ya Apollo imetangaza kufanikiwa kutenganisha mapacha waliokuwa wameungana kutoka Tanzania katika upasuaji ambayo ulichukua masaa 11 na wataalamu 50.
Mapacha Abriana na Adriana walikuwa wameungana katika kifua chini ya tumbo, hali ya kitaalamu inajulikana kama ‘Thoraco Omphalopagus’. Mapacha hao walitenganishwa baada ya mipango ya kina na ushirikiano kati ya madakitari bingwa wa mfumo wa mkojo, figo ini na moyo na madakitari bingwa wa watoto na kuteua dakitari bingwa mmoja kama kiongozi wa timu ambaye alisimamia utaratibu mzima wa upasuaji. Mapacha hao waliokuwa wameungana kuanzia chini ya kifua na tumbo, halikadhalika walikuwa wakitumia mvungu mmoja wa moyo na walikuwa wameungana Ini.
Upasuaji huu wa mafanikio wa kutenganisha mapacha walioungana kutoka nchini Tanzania sio wa kwanza kufanywana hospitali ya Apollo. Mwishoni mwa mwaka 2013 mapacha wengine wakiume waliokuwa wameungana wajulikanao kitaalamu kama Pygopagus, Ericana na Eluidi kutoka Tanzania walifanikiwa kutenganishwa nawataalamu wa hospitali hiyo. Matukio amabayo yamepandisha chati nakuipa hadhi ya juu hospitali ya Apollo iliyopo nchini India kwa ujumla kama kiongozi katika sekta ya afya na mfano wakuigwa na nchinyingine ikiwemo Tanzania. Hospitali hiyo inamahusiano mazuri na nchi ya Tanzania na imekuwa ikipokea idadi kubwa ya wagonjwa kutoka nchini Tanzania.