Madaktari Sita kutoka Misri Wawasili Kusaidia Matibabu Muhimbili

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hussein Mwinyi

NA MAGRETH KINABO – MAELEZO

JUMLA ya madaktari sita na wataalamu wawili, mmoja wa teknolojia na mwingine wa utawala kutoka Misri wamewasili nchini kwa ajili ya kutoa huduma ya upasuaji wa tundu ndogo kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) jijini Dare es Salaam.

Kauli hiyo imetolewa leo na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hussein Mwinyi wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ujio wa madaktari hao.

“Madaktari hawa watasaidia kutoa tiba na kuwafundisha madaktari wetu utaalamu huu, hivyo ujio wao utasaidia kupunguza gharama za matibabu kwa wagonjwa wanaotakiwa kwenda nje ya nchi,” alisema Dk. Mwinyi.

Aliongeza kuwa madakatari hao watakuwepo katika hospitali hiyo kuanzia Juni 10 hadi 15, mwaka huu kwa ajili ya kutoa huduma hizo. Dk. Mwinyi aliushukuru ujio huo kwa kuwa utasaidia kubadilishana uzoefu na teknolojia na kuboresha afya ya Watanzania.

Kwa upande wake, Balozi wa Misri nchini Tanzania, Hossam Omar alisema ujio wa madaktari hao ni kuendeleza ushirikiano baina ya nchi hizo mbili katika sekta hiyo, ambapo watauendeleza katika maeneo mengine ya sekta hiyo na nyingine.