Na Mwandishi Wetu
UAMUZI wa kugoma umefikiwa leo mjini Dar es Salaam katika Mkutano uliofanyika Don Bosco Upanga ikiwa ni mwendelezo wa Mikutano isiyokoma iliyoanza Jumatano ya Wiki iliyopita wakishinikiza madai kadhaa dhidi ya Serikali.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo mtandao huu umezipata, madaktari hao wamepanga kuendesha mgomo kuanzia Januari 24, 2012 kwa lengo la kushinikiza madai yao. Januari 18, 2012 ilianza mikutano ya kutafuta suluhu ya matatizo yao na Sekta ya Afya kwa Ujumla, juhudi ambazo hazijazaa matunda licha ya majadiliano kuanzia ngazi ya Wizara ya Afya mpaka Ofisi ya Waziri Mkuu.
Miongoni mwa madai ya madaktari ambayo wanataka yafanyiwe kazi ni Serikali kuboresha huduma za afya nchini (hospitali na vitanda kwa kila mgonjwa inawezekana), kuboreshwa kwa maslahi kwa watumishi wa sekta ya afya, malipo kwa kazi za ziada kwani madktari wanalipwa sh. 10,000 kwa mkesha na kufanya kazi masaa 36 tofauti na taratibu za Serikali ambapo ilitakiwa walipwe sh. 40,000 (half pediem).
Madai mengine ni pamoja na haki ya kupewa nyumba au posho ya pango kama muongozo wa utumishi wa umma wa serikali ya Tanzania unavyoelekeza ule wa mwaka 1994 na wa mwaka 2009, kulipwa posho ya kufanya kazi katika mazingira hatarishi (Risk allowance)
Sharti lingine la madaktari kwa Serikali ni kutaka kuondolewa kwa Katibu Mkuu wa wizara ya afya Bi. Blandina Nyoni ambaye wanadai amekuwa ni kikwazo katika juhudi za msingi katika kuboresha sekta ya afya Tanzania, huku wakimtuhumu kutoa kauli za kejeli kwa watumishi wa afya kuwa; ‘anamshukuru baba yake kwa kumkataza kusomea mambo ya afya kwani sekta ya ya afya haifai na ndio maana licha ya kufaulu masomo ya sayansi baba yake alimshauri asomee uhasibu’.