Na Mwandishi wetu – Canberra, Australia
WAFANYAKAZI wa Hospitali ya wanawake na watoto ya Centenary ya mjini Canberra wameonyesha nia ya kufanya kazi nchini Tanzania ili kumuunga mkono Mke wa Rais, Mama Salma Kikwete katika juhudi zake za kupunguza vifo vya kina mama wajawazito na watoto.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji anayeshughulikia afya za wanawake, vijana na watoto wa Hospitali hiyo Liz Chatham wakati akiongea na Mama Kikwete na ujumbe wake walipotembelea Hospitali hiyo.
Liz alimshukuru Mama Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) kwa kutembelea Hospitali hiyo na kujioneka kazi wanazozifanya pia alimpongeza kwa juhudi zake anazozifanya za kuhakikisha wanawake na watoto wa Tanzania wanapata huduma bora ya afya.
Mkurugenzi huyo alisema katika Hospitali hiyo wafanyakazi wengi wa sekta ya afya wanapenda kwenda kufanya kazi Tanzania ili waweze kutoa huduma ya afya kwa ajili ya mama na mtoto pamoja na watu wengine na kubadilishana ujuzi wa kazi na wenzao.
Kwa upande wake Mama Kikwete alisema ni jambo la kufurahisha kuona katika Hospitali hiyo wanawake wenye afya njema wanajifungua katika mazingira mazuri na watoto ambao ni wagonjwa wanapewa matibabu na uangalizi wa hali ya juu.
“Nawapongeza kwa kazi nzuri mnayoifanya ya kuwahudumia kinamama wajawazito na watoto, kujifungua iwe sababu ya kuwa na furaha na kusherehekea lakini siyo tofauti na hapo, nasema hivi kutokana na mazingira halisi ya kule ninakotoka”.
Pamoja na kuwa jitihada za makusudi zinafanywa na Serikali bado wanawake na watoto wanapoteza maisha wakati wa kujifungua kutokana na sababu zinazoweza kuzuilika,” alisema Mama Kikwete.
Akiwa katika Hospitali hiyo Mama Kikwete alipata nafasi ya kuongea na watoto ambao ni wagonjwa ambao kwa wakati huo walikuwa darasani wanasoma na aliwaona na kuwajulia hali wazazi waliojifungua Hospitalini hapo.
Utaratibu wa Hospitali ya wanawake na watoto ya Centenary mtoto akiwa amelazwa kipindi ambacho shule hazijafungwa anafundishwa masomo ambayo wenzake wanafundishwa darasani kwani Hospitalini hapo kuna madarasa na walimu wanaofundisha watoto wagonjwa. Mama Kikwete ameambatana na mmewe, Rais Jakaya Mrisho Kikwete nchini Australia kwa ajili ya ziara rasmi ya Kiserikali ya siku nne.