Madaktari bingwa Muhimbili nao wagoma

Abelina Kitochi Mgonjwa aliyekuwa amelazwa katika wodi ya Sewahaji katika Hospitali ya Taifa Muhimbili iliyopo jijini Dar es Salaam jana akilia nje ya wodi hiyo baada ya kukosa huduma kwa siku kadhaa kufuatiwa na mgomo wa Madaktari bingwa na Wauguzi wanaogoma kuishinikiza Serikali nyongeza ya mishahara.

WAKATI Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii ikianza kazi ya kuzungumza na madaktari walio kwenye mgomo, madaktari bingwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) na walio katika Taasisi ya Mifupa (MOI) wamegoma. Mgomo huo wa jana ulihusisha vitengo vyote huku wagonjwa waliokuwa wamelazwa hospitalini hapo wakipewa taarifa za kuondoka katika wodi walimolazwa.

Azimio la mgomo huo lilifikiwa katika kikao cha dharura kilichoitishwa na jopo la madaktari bingwa wakiongozwa na Dk. James Rwehabura ambaye ni daktari bingwa wa Kitengo cha Uchunguzi wa Magonjwa ya Binadamu.

Habari za ndani kutoka katika kikao cha dharura cha wanataaluma hao, zilisema uamuzi huo ulifikiwa kwenye kikao cha madaktari hao kilichoanza mapema asubuhi jana na kumalizika saa 6:00 mchana. “Kwa pamoja tumekubaliana kuweka vifaa chini, hii ni kutokana na ukweli kuwa hali ya utoaji huduma katika hospitali hii ni mbaya huku taarifa za Serikali zikiwa siyo za kweli,” alidokeza mmoja wa madaktari bingwa.

Daktari huyo aliyekataa kutaja jina lake, alisema, “Tumekubaliana kugoma hadi hapo Serikali itakapotoa majibu ya madai yote yaliyowasilishwa na jumuiya ya madaktari inayoongozwa na Dk Stephen Ulimboka kwa Serikali.” Jumuiya hiyo iliwasilisha madai mbalimbali likiwamo la kuitaka Serikali kupeleka vifaa na dawa katika hospitali za Serikali ili madaktari hao waweze kutoa huduma bora kwa jamii.

Pia, madaktari hao walitaka kusitisha safari za vigogo kwenda kutibiwa nje kwa magonjwa yanayotibika ndani kwa kile walichodai, hali hiyo inachangia wao kudharauliwa na pia kuzorotesha jitihada za Serikali katika uboreshaji wa mazingira ya kazi kwa madaktari hao.

Kwa nyakati tofauti, madaktari hao walibainisha sababu ya mgomo wao na kudai kuwa, kikubwa ni mazingira magumu ya kazi. Daktari mwingine ambaye hakupenda jina lake kuandikwa gazetini alisema, licha ya mishahara na posho ndogo, lakini mazingira ya kufanyia kazi yamekuwa magumu mno.

“Tumeshaamua, ‘tools down’ hospitali haina kitu, hata ‘mask’ hakuna badala yake tunavaa gozi tunapofanya upasuaji, acha hiyo, hata nyuzi za kushonea wakati wa upasuaji hakuna,” alisema daktari huyo. Daktari huyo alisema, hawawezi kufanya kazi katika mazingira hayo kwa sababu yatawasababisha kuwa na utendaji mbovu na baadaye taifa kuwalalamikia.

Alisema hapa nchini madaktari bingwa ni wachache, kwa hiyo kitendo cha wao kufanya kazi peke yao bila wasaidizi, yaani madaktari wa mafunzo na wale wanaomaliza, wanaelemewa na mzigo wa kazi. Dk Henry Mwakyoma, Mhadhiri Mkuu wa Chuo cha Udaktari Muhimbili, (MUHAS) ambaye hakuwapo katika kikao hicho cha dharura alidai kuwa, yeye kama mhadhiri hajagoma, lakini alikiri kuwapo kwa mazingira magumu ya kazi.

“Mpaka sasa hatujalipwa mishahara ya mwezi uliopita, halafu kazi yetu ndiyo kama hii tunatakiwa tufanye utafiti, unategemea tutafanya kazi kwa umakini kweli? Tutawafundisha madaktari kwa umakini?” alihoji Dk Mwakyoma.

Mwakyoma alisema, Serikali haiwezi kudai kuwa haina fedha za kutosha wakati imetumia mamilioni ya shilingi katika sherehe za miaka 50 ya Uhuru na uchaguzi wa Igunga. Alisema ni vyema Serikali ikajipanga na kuamua kushughulikia masuala ya madaktari kwa hekima kwani kukaa kimya bila kutoa suluhu ni sawa na kufanya ushindani usio na maana.

Hata hivyo, Ofisa Habari Mwandamizi wa MNH Aminael Aligaesha alisema jana jambo hilo lilikuwa likishughulikiwa kwani vipo vikao vinavyoendelea.

Wagonjwa watimuliwa wodini
Wodi mbalimbali hospitalini hapo zilitawaliwa na vilio kutokana na wagonjwa na ndugu za wagonjwa kupewa taarifa za kuondoka katika eneo hilo mara moja, kutokana na mgomo huo wa madaktari. Mmoja wa wagonjwa waliokuwa wamelazwa katika wodi ya Sewahaji, Sadick Dimoso (35) mkazi wa Morogoro alisema hali sasa MNH ni mbaya.

“Tumeambiwa tuondoke wodini bila ya kuruhusiwa na daktari, hii ni hatari tena wanasema tuondoke tukakae huku hadi wiki mbili ndio turudi kuangalia,” alisema Amina Ramadhani, aliyekuwa akisubiri kufanyiwa upasuaji wa jicho. Alisema hatua ya kutakiwa kuondoka hospitalini hapo imekatisha matarajio yao ya kuendelea kuwa hai na kuitaka Serikali kufanyia kazi madai ya madaktari.

Wakati kundi la watu wengine wakililia huduma hosptalini hapo, baadhi ya ndugu za wagonjwa waliingia katika mgogoro na walinzi wa wodi hiyo ya Sewahaji wakitaka waandishi wa habari kuingia wodini.

Vikao vya Kamati Wakati hayo yakijiri, vikao baina ya madaktari na Kamati ya Kudumu ya Huduma za Bunge, viliendelea jana katika ofisi ndogo za Bunge huku taarifa zake zikiwa ni siri.
CHANZO: Mwananchi