Madaktari 21 wa China wajitambulisha Ikulu Zanzibar

Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein

Na Rajab Mkasaba, Zanzibar
MADAKTARI wapya 21 kutoka China wamefika Ikulu mjini Zanzibar kwa ajili ya kujitambulisha kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein na kueleza kuwa watahakikisha wanatoa huduma bora kwa jamii ya Kizanzibari kwa lengo la kuinua sekta ya afya nchini.

Madaktari hao wakiwa pamoja na Balozi Mdogo wa China Bi. Chen Qiman walimueleza Rais Dk. Shein kuwa wamefarajika na mapokezi mazuri waliyapata kutoka kwa wenyeji wao Wizara ya Afya, na kusisitiza kuwa lengo kubwa ni kutoa huduma bora kwa jamii.

Walieleza kuwa Zanzibar na China zina historia ya muda mrefu ambapo ni miaka takriban 46 sasa nchi hizo zimekuwa na uhusiano mwema na China imekuwa ikileta madaktari bingwa hapa Zanzibar kila baada ya miaka miwili huja na wengine huondoka.

Madaktari hao wakiongozwa na kiongozi wao mkuu Dk. Lu Jianlin walieleza kuwa mara baada ya Mapinduzi ya Januari 12, 1964 China ilijenga mahusiano mema na Zanzibar hatua ambayo ilipelekea mnamo mwaka 1965 China kuanza kuleta Madaktari Zanzibar.

Walieleza kuwa tokea miaka hiyo Madaktari kutoka nchini mwao wamekuwa wakifanya kazi kwa mashirikiano na maelewano mazuri na Zanzibar na kuweza kuimarisha udugu kati yao na wananchi wa Zanzibar ambao walieleza kuwa umepelekea kupata mapezi makubwa kwa wananchi kutokana na huduma wanazozitoa.

Madaktari hao walieleza kuwa timu hiyo ya Makatari 21 ni timu ya 24 tokea kuanza kuja Madaktari hapa nchini mnamo mwaka huo wa 1965. Madaktari hao walieleza kuwa tayari wameshaanza kazi na wanafurahia mashirikiano mazuri wanayoyapata kutoka kwa madaktari wazalendo na wamekuwa wakifanya kazi bega kwa bega.

Madaktari hao pia, walimueleza Dk. Shein kuwa wanatarajia mnamo mwezi wa Octoba ujumbe kutoka Idara ya Afya ya Jimbo la Jiangsu utakuja Zanzibar nakukutana na Dk. Shein kwa lengo la kufanya mazungumzo na kuweka mikakati zaidi ya kuimarisha sekta ya afya hapa Zanzibar.

Sambamba na hayo, Madaktari hao walitoa salamu zao za rambirambi kwa Rais Dk. Shein kufuatia msiba mkubwa wa kuzama kwa meli ya Mv. Spice Islandar hivi karibuni huko Nungwi, Mkoa wa Kaskazini Unguja na kusababisha vifo na majeruhi kadhaa.

Akiongozana na Madaktari hao wapya kutoka China Katibu Mkuu wa Wuizara ya Afya Mohamed Saleh Jidawi, alieleza kuwa Madaktari kutoka China wamekuwa na mchango mkubwa katika kutoa huduma kwenye hospitali za hapa Zanzibar na pia, ni nchi ya mwanzo kuleta Madaktari hapa Zanzibar mara baada yaMapinduzi ya Januari 12, 1964.

Nae Balozi Mdogo wa China Bi Chen Qiman alimueleza Dk. Shein kuwa China itaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta mbali mbali za maendeleo ikiwemo sekta ya afya. Balozi Qiman alieleza kuwa ujio wa timu hiyo ya Madaktari wakiwemo Madaktari Bingwa itasaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha sekta ya afya na kutoa huduma bora kwa jamii Unguja na Pemba.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, alitoa pongezi na shukurani kwa China kwa juhudi zake za kuendelea kuisaidia Zanzibar katika kuimarisha sekta ya afya ikiwa ni pamoja na ujio wa Madaktari hao bingwa.

Katika maelezo yake Dk. Shein alisema kuwa kumekuwa na historia nzuri ya ujio wa madaktari hao kwa miaka 46 sasa, hali ambayo imeonesha wazi kuwa Madaktari hao wamekuwa na mchango mkubwa katika kuinua sekta ya afya hapa Zanzibar.

Dk. Shein alisema kuwa anamatumaini makubwa kuwa jopo hilo la madaktari wataendeleza sifa za madaktari waliopita wa kutoka nchini humo ambao wamefanya kazi vizuri na kujijengea sifa na mapenzi makubwa kwa wananchi wa Zanzibar.

Aidha, Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imedhamiria kuimarisha sekta ya afya katika kuhakikisha kuwa baadhi ya huduma ambazo zilikuwa hazipatikani hapa nchini ziweze kufanyika zikiwemo za upasuaji mkubwa.

Alieleza kuwa serikali kupitia Wizara yake ya Afya ina mpango kapambe wa kuanzisha kitengo cha kushughulikia maradhi yatokanayo na matatizo ya figo, maradhi ya moyo, maradhi ya saratani na huduma nyengine na kusisitiza kuwa uwepo wa Madaktari hao bigwa nako kutasidia kufikia lengo hilo.

Dk. Shein pia alipokea salamu za rambi rambi kutoka kwa Madaktari hao pamoja na kutoka kwa Balozi Mdogo na kueleza kuwa kwa niaba ya wananchi wa Zanzibar wanatoa shukurani kwa salamu hizo.