Na Benedict Liwenga, Maelezo – Dodoma
UMOJA wa Machifu Tanzania (UMT) kupitia wawakilishi wake, umewasilisha nyongeza ya mapendekezo yake kuhusu Katiba Mpya kwa Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Bi. Samia Suluhu Hassan. Akiuwakilisha Umoja wa Machifu Tanzani, Chifu kutoka Magu John Nyanza alimueleza Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba kuwa wanaishauri Serikali kutayarisha mkakati wa Kitaifa wa Utamaduni kwa kuwashirikisha wadau wakuu wa masuala ya Utamaduni ili mpango mkakati huo uwe na Dira ya Utamaduni itakayobainisha cha kufanya kwa dhana ya kujenga, kuhamasisha na kuendeleza Utamduni katika maeneo yote nchini.
“Chifu kutoka Magu, John Nyanza amesema kuwa lengo la kuwasilisha mapendekezo hayo kwaajili ya kusisitiza masuala mazuri ya Utamduni kuendelea ili kuweza kudumisha madili kwa nia nzuri ya kudumisha amni na ushirikiano”. Alisema Chifu Nyanza.
Naye Chifu kutoka Ntuzu, Bariadi Chifu Agnes Ndaturu ameeleza kuwa mapendekezo yao yatasaidia kuweza kuwatambua waganga wa Jadi ambapo hapo zamani, mganga wa Jadi alikuwa anatambulika na kufanya kazi katika eneo husika analotoka, lakini hivi sasa waganga wengi wa jadi wamekuwa na tabia ya kufanya kazi zao bila mipaka.
”Mapendekezo haya yatasaidia viongozi wa waganga wa jadi nchini kuwatambua wale waganga wanaokiuka maadili ya shughuli zao mfano mauaji ya Albino, kwakuwa kila kiongozi atakuwa anawatambua waganga wa eneo lake husika,” alisema Chifu Ndaturu.
Aidha, Machifu hao wameongeza kuwa, Wajumbe wenzao waliowatuma kuwawakilisha wanasisitiza juu ya umuhimu wa Utamaduni kupewa nafasi rasmi katika Katiba mpya na Serikali ili pawepo na kipaumbele katika utekelezaji wake nchini.
Katika maelezo yao, machifu wa Tanzania wamesema kuwa suala la Utamaduni katika Rasimu ya Pili ya Katiba lifanyiwe marekebisho kwa kuzingatia mapendekezo yaliyoibainishwa huku msisitizo wao ukiwa katika Katiba kueleza wazi kuwa sera na Sheria mpya zitakazotungwa zihakikishe kuwa Tume ya Taifa ya Utamaduni inaanzishwa kisheria ili kusimamia masuala ya Utamaduni.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Mhe. Samia Suluhu Hassan amewatotoa wasiwasi wawakilishi wa Umoja wa Machifu hao wa Tanzania aliokutana nao kwa kuwaeleza kuwa atayawasilisha katika Uongozi wa Kamati ya Bunge ambapo Kamati Ndogo ya Uongozi inatarajiwa kukutana leo jioni ili kuweza kuyajadili.
“Nimeyapokea mapendekezo yenu, kwakuwa Kamati zinaendelea na kazi ambapo wiki hii kamati zitakuwa zimemaliza kazi zake na hakutakuwa na nafasi tena ya kuyapokea mapendekezo na maoni mengine”.
Wakati huo huo; Ofisi ya Bunge Maalum la Katiba mjini Dodoma, imetoa ufafanuzi juu ya taarifa zilizotolewa kwenye vyombo vya habari kuhusu kuchelewa kwa malipo ya posho za Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba.
Ufafanuzi huo umetolewa na Mkurugenzi wa Habari na Itifaki Bw. Jossey Mwakasiyuka wakati alopokutana na waandishi wa habari kwa lengo la kutolea ufafanuzi kuhusiana na taarifa hizo zilizoikera ofisi hiyo ya Bunge Maalum.
Mwakasyuka amevieleza vyombo vya habari kuwa, ofisi ya Bunge Maalum imekerwa na kuchapishwa kwa taarifa hizo na baadhi ya vyombo vya habari kwani taarifa hizo ni za upotoshaji na zina lengo la kuwadhalilisha Waheshimiwa Wajumbe na kuwafanya waonekane wenye kuishi na kufanya kazi kwa kutegemea posho wanazolipwa.
“Ni vema ikaeleweka kwamba Wajumbe wa Bunge Maalum wote ni watu wenye nafasi zao katika jamii na ni wenye kazi au shughuli zao mahususi zinazowaingizia kipato na kwamba Ujumbe wa Bunge Maalum ni nafasi ya muda tu ya kutimiza jukumu la kuliandalia taifa Katiba Mpya”. Alisema Mwakasyuka.
Mwakasyuka ameongeza kuwa, si vema kwa vyombo vya habari kuwadhalilisha Wajumbe hao kwa njia yoyote ile kwani kwa kufanya hivyo kunawavunja moyo na kuwafanya washindwe kuifanya kazi ya Bunge Maalum vizuri kama ilivyotarajiwa na wananchi.
Akifafanua kuhusiana na malipo ya posho hizo, Mkurugenzi Mwakasyuka ameviambia vyombo vya habari kuwa, Wajumbe wote wa Bunge Maalum ambao wanahudhuria vikao vinavyoendelea wamekwishalipwa posho zao zote kama wanavyostahili.
“Ni vyema ikaeleweka kwamba malipo ya posho yanafuata taratibu za fedha za umma na yanapita kwenye mchakato maalum unaojumuisha kupata orodha za mahudhurio ya Wajumbe kwenye kikao, upatikanaji wa fedha toka Hazina, na upatikanaji wa fedha toka Benki, hivyo wakati mwingine huchukua siku kadhaa hadi kukamilika.” Alifafanua Mwakasyuka.
Aidha, Mwakasyuka amevitahadharisha vyombo vya habari vinavyondika habari za Bunge Maalum kuzingatia maadili na kanuni za Uandishi wa habari zinazotolewa katika vikao vya Bunge Maalum ili taarifa kama hizo za upotoshaji zisijirudie tena.
“Kumbukeni kuwa wajibu wenu ni kuhabarisha umma na sio kupotosha umma na hata kuleta usumbufu kwa jamii kutokana na uandishi usio makini”. Alionya Mwakasyuka.
Katika kanuni za Bunge Maalum, kanuni ya 77 inawataka waaandishi wa habari kuandika habari za Bunge Maalum kwa weledi mkubwa kwa kuzingatia maadili ya uandishi wa Habari ili kuondoa uandishi wenye kuleta chuki kati ya Serikali na Wananchi wake kwani kinyume na kanuni hiyo, Katibu anaweza wakati wowote kuondoa ruhusa aliyotoa kwa mwakilishi wa chombo chochote cha habari iwapo chombo hicho kitatoa taarifa yoyote kuhusu shughuli za Bunge Maalum ambayo kwa maoni ya Bunge Maalum inapotosha ukweli au vinginevyo inakiuka kanuni, taratibu au haki za Bunge Maalum.