MABINGWA watetezi wa Kombe la Dunia, Hispania wameondolewa kwenye michuano ya kombe la dunia mwaka 2014, inayoendelea nchini Brazil baada ya kuchalazwa mabao 2 kwa mtungi na timu ya taifa la Chile.
Matokeo ya jana yamewaaibisha mabingwa hao watetezi baada ya kutoka mapema kwenye mashindano hayo tena bila pointi yoyote katika kundi lao ‘B’. Hispania inaungana na timu ya Cameroon kuondoka mara baada ya michezo yao ya mwisho baada ya kuchapwa bila huruma katika mechi zao mbili za awali mfululizo. Cameroon wanafunga virago baada ya kubugizwa bila huruma mabao manne na timu ya Croatia katika uwanja wa Manaus.
Cameroon walimaliza mechi hiyo wakiwa wachezaji kumi baada ya mchezaji wa Barcelona, Alex Song kutolewa nje kwa kadi nyekundu. Cameroon hawakuwapa upinzani Croatia kabisa katika mchuano huo wa kundi A.
Croatia sasa wana matumaini ya kuwania nafasi ya pili katika kundi hilo dhidi ya Brazil na Mexico ili kuendelea katika raundi ya pili. Croatia wanajua kuwa mshindi katika mechi yao na Mexico, ataendelea kwa michuano ya raundi ya pili, huku Cameroon wakisubiri mchezo na wenyeji, Brazil ili waondoke.
Chile pamoja na Uholanzi wanafuzu katika raundi ya pili. Kufuatia ushindi huu wa mabao 2-0 mikononi mwa Chile mabingwa watetezi wa kombe la dunia Uhispania sasa wamehakiki tikiti za ndege kurejea nyumbani pamoja na Australia .
Hii ni baada ya Uholanzi kushinda mechi yake ya pili na kuongoza kundi B ikiwa na alama 6 sawa na Chile. Chile na Uholanzi hata hivyo zitakutana katika mechi ya kuamua yupi kati yao ataongoza kundi hilo. Mshindi wa pili katika kundi B atachuana na bingwa katika kundi A inayojumuisha wenyeji Brazil na washindi wa pili katika kundi hilo Mexico.
Kwa upande wao Hispania ambao sasa wamefungwa jumla ya mabao 7 watachuana na Australia katika mechi ambayo haitakuwa na umuhimu wowote.