Na Kulwa Mayombi, EANA
MABALOZI wa Rwanda na Ufaransa wanaowakilisha nchi zao Tanzania wametembelea Mahakama ya Afrika ya Watu na Haki za Binadamu (AfCHPR) yenye makao yake makuu Mkoani Arusha na kuelezea utayari wa nchi zao kuimarisha shughuli za kisheria za mahakama hiyo.
Katika mazungumzo yake na Rais wa mahakama hiyo Jaji mkuu mstaafu wa Tanzania Augustino Ramadhani, Balozi wa Ufaransa Bibi Malika Berak amesema kwamba kuna fursa kubwa ya kubadilishana uzoefu baina ya Ufaransa na Mahakama hiyo. Katika taarifa iliyotolewa na Mahakama hiyo, balozi huyo alisisitiza kuangaliwa fursa zaidi za kuimarisha ushirikiano baina ya pande hizo mbili.
Kwa upande wake, Balozi wa Rwanda Bwana Eugene Kayihura amepongeza mafanikio yaliyofikiwa na mahakama hiyo baada ya kuelezwa shughuli za mahakama hiyo. Jaji Ramadhani aliishukuru Rwanda kwa kuridhia itifaki na kutoa tamko kuruhusu mashirika yasiyo ya kiserikali na watu binafsi kuweza kupata huduma za mahakama hiyo.
Rwanda ni miongoni mwa nchi saba kati ya nchi 29 za Afrika zilizoridhia itifaki ya kuanzishwa Mahakama hiyo ya watu na haki za binadamu na kutoa tamko. Nchi zingine ni: Burkina Faso, Cote d’Ivoire, Ghana Mali, Malawi, na Tanzania, ambao ni wenyeji wa Mahakama hiyo. Nchi zilizoridhia itifaki ni: Algeria, Benin, Burundi, Cameroon,Visiwa vya Comoro, Congo, Gabon, The Gambia, Kenya na Libya.
Nyingine zilizoridhia ni : Lesotho, Mauritania, Mauritius, Msumbiji, Nigeria, Niger, Uganda, Jamhuri ya kidemokrasi ya watu wa Sahrawi, Senegal, Afrika ya Kusini, Togo na Tunisia.