Na Mwandishi wetu
Sekta ya Habari ni moja ya sekta za huduma za jamii inayotoa huduma ambayo ni haki ya msingi ya raia kama ilivyotamkwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
Ibara ya 18 (2) ya Katiba inasema kuwa kila raia anayo haki ya kupewa taarifa wakati wowote kuhusu matukio mbalimbali nchini na duniani kote ambayo ni muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi na pia juu ya masuala muhimu kwa jamii.
Aidha, kutafuta na kupewa habari kunatambuliwa duniani kote kuwa ni moja ya haki za binadamu. Haki hii kama zilivyo haki nyingine zote hutolewa kwa kuzingatia wajibu wa kila raia kwa jamii na uhuru binafsi wa binadamu.
Dhima ya sekta ya Habari katika jamii ni kutoa habari, kuelimisha na kuburudisha. Sekta hii inahudumiwa na vyombo vya habari ambavyo ni redio, magazeti, majarida, televisheni, filamu, video, tovuti, intaneti, picha na machapisho kama vipeperushi, katuni, na mabango.
Kasi ya upatikanaji na usambazaji wa habari imetokana na maendeleo ya teknolojia ya mawasiliano na hivyo kurahisisha dhana ya kupashana habari kwa wakati kadhalika kuifanya sekta ya habari kukua kwa kasi na kutumiwa na watu wa rika na mazingira mbalimbali.
Kutokana na kasi ya ukuaji wa sekta hii, idadi ya magazeti ya kila siku imeongezeka kutoka mawili (2) mwaka 1992 hadi kumi na nne (14) mwaka 2015. Aidha, idadi ya magazeti ya kila wiki imeongezeka kutoka matano (5) mwaka 1992 hadi kumi na tatu (13) mwaka 2015.
Idadi ya vituo vya redio Tanzania Bara imeongezeka kutoka kimoja (1) mwaka 1992 hadi 114 mwaka 2015. Aidha, Vituo vya televisheni navyo vimeongezeka hadi kufikia ishirini na nane (28).
Baadhi Mamlaka za Serikali za Mitaa zimeanzisha vituo vya televisheni na redio kwa lengo la kujenga ukaribu na wananchi na kurahisisha upatikanaji wa taarifa kwa wakati ili kutoa haki ya upatikanaji wa habari kwa kila raia.
Serikali ya Awamu ya Nne itakumbukwa kwa mengi ikiwemo utekelezaji na uboreshaji wa Vitengo vya Mawasiliano Serikalini. Vitengo hivi vimeboreshwa na kutoa fursa kwa Maafisa Mawasiliano kuwa kiungo muhimu kati ya Serikali na wananchi katika masuala yote yanayohusu upatikanaji wa habari.
Serikali imeendelea kuajiri Maafisa Mawasiliano na kuboresha Sehemu ya Uratibu wa Vitengo vya Mawasiliano Serikalini ili kusimamia na kuratibu shughuli za Mawasiliano ya Serikalini na Wasemaji wa taasisi za Serikali katika ngazi ya Wizara, Sekretarieti za Mikoa, Serikali za Mitaa, Idara zinazojitegemea na Wakala za Serikali.
Takwimu kutoka katika Ripoti ya mafanikio ya Sekta ya Habari ya mwaka 2014 zinaonyesha kuwa hadi kufikia mwezi Juni, 2014 Maafisa Mawasiliano 302 wameajiriwa katika Wizara na Taasisi mbalimbali za Serikali ukilinganisha na Maafisa Mawasiliano 47 mwezi Juni, 2005. Hili ni ongezeko la asilimia 542.
Ili kulinda weledi katika utendaji kazi wa kila siku, Serikali imekua ikiandaa programu mbalimbali za mafunzo kwa Maafisa Mawasiliano ambayo hufanyika kila mwaka wakati wa vikao kazi vinavyowakutanisha Maafisa Mawasiliano wote nchini.
Aidha, Serikali imeanzisha Tovuti ya Wananchi kwa ajili ya wananchi kuwasiliana na Serikali moja kwa moja. Kupitia Tovuti hii maswali, kero, maoni na hoja mbalimbali kuhusu utekelezaji wa shughuli za Serikali na Utumishi wa Umma kwa jumla, zimekuwa zikitumwa na Serikali kutoa mwitikio kupitia Tovuti hii.
Akizungumzia Tovuti ya Wananchi Afisa Habari kutoka Idara ya Habari Maelezo Bw. Husein Makame alisema kuwa Tovuti hii ilianza kazi tarehe 1 Julai, 2007. Hadi kufikia Machi, 2013, Tovuti hiyo imepokea jumla ya hoja 117,243 na kati ya hizo 78,258 zimeshughulikiwa na kupatiwa ufumbuzi. Hata hivyo, hoja 38,985 hazikuihusu Serikali, ziliingia katika tovuti kwa makosa.
Serikali kupitia Wizara ya Habari, Vijana Utamaduni na Michezo imehakikisha kuwa vyombo vya habari nchini vinaendelea kuwa huru kupokea na kutoa habari za matukio mbalimbali yanayojitokeza katika jamii. Kadhalika kuzingatia maadili ya taaluma ya uandishi wa habari.
Uhuru wa vyombo vya habari umeiwezesha Wizara kusajili magazeti na majarida 357 kwa kipindi cha kati ya mwaka 2005 hadi 2015 ikilinganishwa na magazeti 505 yaliyosajiliwa tangu tupate Uhuru mwaka 1961 hadi 2005. Hali hii imewezesha kufanya magazeti yaliyosajiliwa nchini hadi sasa kuwa 862.
Aidha, ripoti ya mafanikio ya sekta ya habari ya mwaka 2014 inaonyesha kuwa Idara ya Habari imekua ikihifadhi picha za matukio mbalimbali ya kitaifa tokea enzi ya Ukoloni wa Waingereza hadi sasa. Maktaba hii ya picha imehifadhi zaidi ya picha 2, 500,000 pamoja na “negatives” zake ambapo picha hizo zimehifadhiwa katika mfumo wa kidijiti ili kurahisisha upatikanaji, utumiaji na utunzaji wake.
Uhifadhi picha wa aina hii unaendana na teknolojia ya kisasa na pia unaondoa uharibifu wowote unaoweza kutokea kama vile majanga ya moto, maji na mengine ya asili ambayo yangeweza kuharibu kabisa hazina hii muhimu ya taifa.
Kwa upande wa maudhui ya vipindi vinavyorushwa katika televisheni na redio, Kamati ya Maudhui kwa kushirikiana na Wadau wa Sekta ya utangazaji imeandaa maboresho ya kanuni za utangazaji. Pia kamati hiyo imeandaa mwongozo ambao utasaidia kuboresha matangazo ya biashara yenye kuzingatia maadili na weledi katika sekta ya utangazaji.
Sekta ya habari, imeweza kuendana na mabadiliko ya teknolojia kwa kuhama kutoka katika mfumo wa utangazaji wa analoji kwenda mfumo wa dijiti. Pamoja na faida nyingine, Mfumo wa dijiti umeongeza ubora wa picha, sauti na matumizi ya masafa ya utangazaji.
Mabadiliko ya kisiasa, kiuchumi na kijamii yanayotokea nchini yameathiri utekelezaji wa Sheria inayosimamia Sekta ya Habari nchini. Hali hii imeilazimu Serikali kuanza mchakato wa kutunga Sheria mpya ya Kusimamia Vyombo vya Habari. Mchakato wa kutunga Sheria hii unaendelea kwa kushirikisha wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na Wamiliki na Waendeshaji wa vyombo vya habari pamoja na Sekta binafsi.
Ikumbukwe kuwa sekta ya habari inategemewa na jamii, kwani hutoa fursa kwa jamii kupata taarifa ya mambo yanayowahusu na yanayoendelea duniani na kuiwezesha kufanya maamuzi ya maendeleo yao kutokana na kuwa na taarifa za masuala ya kijamii, kiuchumi, kisiasa na kiteknolojia.