Mabadiliko kudhibiti uchakachuaji mafuta hayamuathiri mtumiaji wa mwisho-Ewura

Mkuu wa Idara ya Mawasiliano na Mahusiano wa EWURA, Titus Kaguo alipokuwa akizungumza na wanahabari kutoa ufafanuzi juu ya mabadiliko hayo.


Na Jochim Mushi

MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji nchini (EWURA) imesema hatua ya mabadiliko ya kuongeza kodi ya mafuta ya taa kudhibiti uchakachuaji wa mafuta ikiwemo diseli haujamuathiri mtumiaji wa mafuta ya taa kama inavyodhaniwa na baadhi ya watu.

Kauli hiyo ilitolewa jana mjini Dar es Salaam na Mkuu wa Idara ya Mawasiliano na Mahusiano wa EWURA, Titus Kaguo alipokuwa akizungumza na wanahabari kutoa ufafanuzi juu ya mabadiliko hayo.

Katika mabadiliko hayo, EWURA imepandisha kodi ya mafuta ya taa kwa waagizaji wan je kutoka sh. 52 hadi sh. 400.30, ikiwa ni kudhibiti udanganyifu ambao ulikuwa ukifanywa na baadhi ya waagizaji wasiowaaminifu.

Kaguo alisema awali kabla ya mabadiliko baadhi ya waagizaji walikuwa wakiagiza mafuta ya taa kwa wingi kwa ajili ya uchakachuaji kutokana na urahisi wa bidhaa hiyo kwa kodi tofauti na nishati za mafuta mengine.

Alisema mbali na EWURA kupandisha kodi hiyo ili kudhibiti vitendo vya uchakachuaji imeamua kuweka punguzo la sh. 224.50 ikiwa ni kinga kwa mtumiaji wa mwisho yaani mwananchi hali ambayo haitamuathiri mtumiaji huyo.

“Unajua tofauti ya awali kodi ya mafuta ya taa ilikuwa ndogo zaidi kitendo hiki kiliwafanya baadhi ya waagizaji ambao si waaminifu kuagiza mafuta ya taa kwaajili ya shughuli ya uchakachuaji maana yalikuwa rahisi kwa kodi na walikuwa wakipata kiasi kikubwa cha fedha endapo watafanya hivyo. Sasa tumedhibiti hakutakuwa na hali kama hiyo tena…kutokana na mabadiliko hayo na sheria zitakavyo simamiwa kwa ataeendelea kufanya hivyo,” alisema Kaguo.

Aidha aliongeza kuwa takwimu zinaonesha kumekuwa na ongezeko kubwa la uagizaji wa nishati ya mafuta ya taa tofauti na mahitaji ya kawaida, jambo ambalo linabainisha, waagizaji wengi walikuwa wakifanya hivyo si kutokana na mahitaji ya bidhaa hiyo bali uhalifu (uchakachuaji).

Hata hivyo, Kaguo alibainisha kuwa kuna uwezekano mkubwa wa kupungua kwa bei ya mafuta ya taa kutokana na mabadiliko hayo na kwa mujibu wa majadiliano yanayoendelea kati ya wadau wote hivyo kuwataka wananchi wasihofu juu ya hatua hiyo ya udhibiti uchakachuaji.

Hivi karibuni EWURA imefanya mabadiliko ya kodi za mafuta ya taa ili kudhibiti uchakachuaji, ambapo katika mabadiliko hayo ongezeko kwa mteja wa mwisho kwa lita itafikia kiasi cha sh. 123 gharama ambayo huenda ikashuka tena.