*Wasema tusipokuwa makini tunauza uhuru wetu
MAASKOFU nchini jana walitumia ibaada ya Krismasi, kuzungumzia mambo kadhaa ya kitaifa yakiwamo nyongeza ya posho za wabunge na mchakato wa katiba mpya na kuonya kuwa Watanzania wasipokuwa makini watauza uhuru wao.Wakihubiri kwa nyakati tofauti katika makanisa mbalimbali viongozi hao wa kidini walisema Tanzania ambayo sasa imefikisha miaka 50 ya uhuru wake, inahitaji viongozi wenye maono na mwelekeo thabiti katika maslahi ya taifa badala ya ya kuwa lelemama na wabinafsi.
Askofu Paulo Ruzoka wa Kanisa Katoliki Jimbo la Tabora alisema wingi wa posho wanazojilimbikizia wabunge na watumishi wengine wa umma, ni maslahi binafsi ambayo kimsingi ni hatari kwa mustakabali wa taifa hasa ikizingatiwa kuwa zinaligawa taifa katika makundi ya walionacho na walala hoi.
“Kujilimbikizia posho ni kupuuza dhana ya utawala bora, lakini pia ni ubinafsi na hii ni hatari kwa taifa. Tunapaswa kufanya uamuzi mgumu wa kuleta mabadiliko ya kifikra na mtazamo kwa faida ya nchi yetu,”alisema.
Askofu Ruzoka alisema hayo alipokuwa akihubiri katika ibada iliyofanyika katika Kanisa la Mtakatifu Tereza, mjini Tabora. “Tunaweza kutunza uhuru wetu kama tu tutaweka mbele maslahi ya kitaifa na si viongozi kuweka maslahi binafsi,” alisema.
“Sikukuu hii ya Noeli inakwenda sambamba na maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanganyika. Maana yake ni kwamba tumeshaadhimisha Noel 50 tangu uhuru. Ni lazima tujiulize miaka hii 50 ya uhuru, imetufikisha wapi,”alisema.
Akizungumzia mchakato wa katiba mpya, Askofu Ruzoka alisema ni vema ukawa wa wazi ili kila mwananchi ashiriki na kujua mambo mbalimbali yanayoendelea.”Mchakato wa katiba lazima uwe wazi ili suala la ardhi lijulikane kwa kuwa kilimo ndio uti wa mgongo wa Mtanzania. Kama tutaendelea kuwapa wawekezaji ardhi yetu, hatutakuwa watumwa,”alihoji.
Askofu Ruzoka alisisitiza kuwa sera ya kilimo inaonyesha kuwanufaisha wawekezaji badala ya Watanzania, jambo linaowafawanya wazalendo kurudi katika maisha ya manamba kwenye mashamba ya wawekezaji hao.
Mang’ana naye akerwa na nyongeza ya posho
Askofu Mkuu Kanisa la Menonite Tanzania (KMT), Dayosisi ya Mashariki Jimbo la Upanga jijini Dar es Salaam, Steven Mang’ana, amesema nyongeza ya posho za wabunge inaongeza chuki baina yao na wananachi.
“Watunga sheria na wawakilishi wa wananchi, wanafanya madudu kujipandishia posho. Kwani huko Dodoma hakuna walimu wala wanafunzi ambao maisha kwao pia ni magumu kama ilivyoelezwa na Spika Makinda),” alihoji Askofu Mang’ana.
Katika mahubiri yake jana katika ibada ya Krismasi, Askofu huyo aliwataka Wakristo nchini, kuwaombea viongozi ili waondokane na roho za ubinafsi.
Mokiwa: Nchi inayumba
Askofu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Valentino Mokiwa, amesema nchi inayumba kutokana na kukosa viongozi wenye maadili, wanaojua matatizo ya wananchi kwa kuwa wengi wao, walisoma nje na hawana uzoefu wa mazingira ya Tanzania.
Akizungumza katika ibada ya Krismasi iliyofanyika katika Kanisa la Mtakatifu Alban jijini Dar es Salaam jana, kiongozihuyo wa kidini alisema nchi inaelekea kubaya kutokana na matabaka ya wenye nacho na wasiokuwa nacho kuzidi kuongezeka.
“Hali hiyo ikiachwa, inaweza kusababisha uhusiano mbaya katika taifa kwa sababu wengi wao wanatengwa na kupewa wanaoonekana kuwa wamesomea nje. Lakini hawa waliosoma nje wakirudi nchini, hufanya mambo ambayo hayalingani na mazingira ya Tanzania,” alisema.
Akizungumzia maadhimisho ya Miaka 50 ya Uhuru Askofu Mokiwa alisema ni aibu kuona taifa linaadhimisha miaka 50 katika hali ngumu ya uchumi huku mfumuko wa ukiwa umefikia asilimia 19.5.
Mokiwa alisema Serikali ilikuwa haina sababu ya kutumia fedha nyingi katika maadhimisho hayo na Jeshi la Wananchi kuonyesha nguvu na uwezo wake, badala yake ingetumia fedha hizo kulipa madeni ya walimu na kujenga vyumba madarasa ili kutoa huduma bora za elimu.
“Kwanza siku hizi hatuna adui hata mmoja, watu wote tunazungumza nao, sasa hizi zana za kijeshi ni za nini,”alihoji.
Alisema alishangaa kuona zana hizo za kivita na kesho yake magazeti yakiwa yamepambwa na picha za vifaa hivyo na za makomandoo wakivunja mawe kwa kichwa mambo ambayo alisema hayamsaidii mtoto wa Tanzania.
“Hivi picha ya komanda anapasua jiwe inasaidia nini, nani anataka kutazama vitu kama hivyo,inasaidia vipi upatikanaji wa elimu bora na huduma nzuri za afya,” alisistiza.
Chengula alia na ufisadi
Askofu wa Jimbo Katoliki la Mbeya, Evarist Chengula, amesema uchu wa madaraka na maovu kwa baadhi ya viongozi serikalini, ndiyo chanzo cha kutoweka kwa amani na haki miongoni mwa mwananchi.
Aliyasema hayo jana wakati akiongoza misa takatifu katika ibada ya Krismasi iliyofanyika katika Kanisa la Bikira Maria wa Fatima, Jimbo la Mbeya.
Askofu Chengula alisema amani na haki vinatoweka kwa kasi nchini na katika bara la Afrika kutokana na baadhi ya watawala kunga’ang’ania madaraka kwa kipindi kirefu, lengo likiwa ni kulinda maovu wanayoyafanya wakiwa madarakani.
“Baadhi ya watawala hawataki kuachia madaraka kutokana na dhambi wazifanyazo wanapokuwepo madarakani na wanaogopa kusutwa na wananchi,”alisema askofu Chengula.
Alisema kamwe amani haiwezi kuwepo kama viongozi hawawatendei haki wananchi na kuwatumikia kwa misingi iliyothabiti na uadilifu.
Pengo ahimiza mapambano dawa za kulevya
Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinari Pengo, amesisitiza kuwa taifa linahitaji kuongeza kasi katika vita dhidi ya dawa ya kulevya na kuna kila sababu kuamini kuwa wanaopinga vita hiyo wanaongozwa na roho ya mapepo.
Akizungumza katika ibada ya Krismasi katika Kanisa la Mtakatifu Joseph jana, Kardinali Pengo alisema madhara ya dawa za kulevya kwa vijana, yanatambulika na kwamba jamii inapaswa kuunganisha nguvu katika vita hiyo.
“Hata manabii wamesema dawa za kulevya ni maafa kwa taifa letu. Kwa nini wawepo wanaosema ni wongo kwa sababu tu wanashughulika nayo kama hakuna pepo wa shetani hapo,” alihoji Kardinari Pengo.
Askofu Noeyewa awaasa Watanzania
Askofu Wilson Noeyewa wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKK) nchini Sudan ya Kusini, amewataka Watanzania kudumisha upendo na amani. Alisema hayo jana katika Ibada ya Krisma iliyofanyika kwenye Usharika wa Moshi mjini, Dayosisi ya Kaskazini.
Askofu Noeye alisema madhara ya kukosekana kwa upendo katika jamii ni vita na mauaji ya watu wasiokuwa na hatia kama ilivyokuwa nchini mwake Sudan.
Kabla ya Sudan Kusini kupata uhuru wake, nilifanya kazi ya kuhubiri katika mazingira magumu sana, kwa hiyo nawaasa Watanzania mpendane kwa sababu mkihubiri na mkalishika kwa dhati neno upendo, hata utukufu wa Mungu mtauona,”alisema.
Wakati huo huo, Askofu Issack Amani wa Kanisa Katoliki Jimbo la Moshi, alikemea biashara ya kusafirisha binadamu inayoanza kushamiri nchini akisema ni kinyume na utu na mapenzi ya Mungu.
Askofu huyo alitoa kauli hiyo jana mjini Moshi katika Kanisa la Kristu Mfalme, wakati akihubiri kwenye ibada ya kuadhimisha kuzaliwa kwa Yesu Kristu, Krismasi.
Katika mahubiri yake askofu huyo alitoa wito kwa familia zilizotengana kurudisha mahusiano ili kudumisha upendo ambao umekuwa ukihubiriwa katika Biblia.
Malasusa ahimiza uwajibikaji
Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Alex Malasusa, amewataka wananchi kufanya kazi katika misingi ya kumwogopa Mungu ili kuliletea taifa maendeleo.Alitoa kauli hiyo jana wakati wa ibada ya Krismas iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Azania Front jijini Dar es Salaam.Alisema kama kila mtu ataogopa kutenda maovu katika uwajibikaji wake wa kila siku, hakutakuwa na manung’uniko.
“Ninapokumbuka maneno ya Mungu ya kupendana na kufanya kazi kwa kumwogopa, ni dhahiri napatwa na wasiwasi kwani ukiangalia katika maofisi mengi sidhani kama wanafanya hivyo,” alisema Malasusa.
Askofu Malasusa alisema kutoaminiana kumeibua wimbi la viongozi na watu mbalimbali kwenda kutibiwa nje wakihofia kuhujumiwa maisha yao na hili linatokana na matendo yao kwa wananchi.
“Huwezi amini kwani nimesikia siku hizi kuna baadhi ya akina dada wanaamua kwenda nje ya nchi kujifungua kwa madai hapa nchini wanaweza kusababishiwa vifo ama vitendo viovu vya watoto wao,” alisema Malasusa.
CHANZO: Mwananchi