‘Maandamano ya kudai haki hayahitaji kibali’

Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema

Na Joyce Ngowi

MBUNGE wa Arusha mjini Godbless Lema kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) amesema haogopi kesi za kupigania haki za wananchi hata kama zikifunguliwa 100 kwani thamani ya maisha ni heshima, utu na usafi wa matendo.

Lema alisema hayo Dar es Salaam jana alipokuwa nje ya vikao vya Kamati za Bunge zinazoendelea jijini hapa baada ya kuulizwa juu ya kuongezewa kesi kwa viongozi wa Chadema kutokana na kudaiwa kufanya maandamano bila ya kibali cha polisi Januari 05,mwaka jana.

Alisema hati ya mashtaka iliporejeshwa hakuwepo jijini Arusha hivyo taarifa hizo amezipata kupitia vyombo mbalimbali vya habari hata hivyo Chadema hawajawahi kuwa wadhalimu bali ukweli utasimama na haki itapatikana.
Alibainisha kuwa chama hicho kimekusudia kupigania wananchi bila woga kama alivyofanya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alipo kuwa akipigania uhuru wa nchi hii ambapo alilazimika kushtakiwa pamoja na kuzuiwa kuendelea na kazi yake kama mwalimu.

“Afadhali vita inayotafuta haki na usawa kuliko Amani ya upumbavu inayodhalilisha utu wa mwanadamu, mimi nitakuwa mbabe wa kupigania haki za wananchi walionochagua kwani wamenichagua niwatumikie,” alisema.

Aidha alisema chadema mkoa wa Arusha wamekusudia kufanya maandamanio makubwa kwa lengo la kupinga kupanda kwa gharama za umeme kwani zinasababisha ugumu wa maisha hasa kwa wananchi wenye kipato cha chini.

Alifafanua kuwa maandamano hayo yanatarajia kufanyika baada ya vikao vya kamati kuu ya Chadema vinavotarajiwa kufanyika baada ya kumalizika kwa vikao vya bunge. Alisema kutokana na kupanda kwa gharama hizo nchi ipo kwenyea hatari ya kuporomoka kiuchumi kutokana kupungua kwa uzalishaji wa bidhaa na mambo mengine kwani malaji wa mwisho atashindwa kumudu gharama.

“Aliyesema umeme haujapanda kwa wenye kima cha chini ni mnafiki kwani haiwezekani kwa wazalishaji wa bidhaa hasa za viwandani wazalishe kwa gharama kubwa kisha wauze kwa bei ndogo huo ni uongo mkubwa, aliyesma hayo anastahili kwenda kufundisha somo la uongo kuzimu,” alisema.

Alisema maandamano ya kudai haki hayahitaji kibali bali ujasiri na ukweli wa fikra kwani wote wanaopigania haki wamekuwa wakipewa vibali na baadaye wanageukwa ama kupewa visingizio vya kutokuwepo na amani kwenye maandamano yaliyo kusudiwa.

Alisema viongozo wa Chadema hawawezi kuendelea kukaa kwenye viyoyozi huku waliowachagua wakiendelea kuumia kutokana na ugumu wa maisha unaosababishwa na kupanda kwa gharama za umeme.