Na Joachim Mushi
KAMPUNI ya Bia ya Serengeti Breweries Ltd (SBL) imesema inajisikia faraja kuendelea kudhamini mashindano ya mpira wa miguu kwa timu ya Tanzania kwani, lengo ni kuhakikisha inazipa uzoefu timu ili ziweze kufanya vizuri katika mashindano ya Kombe la Dunia hapo baadaye.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Masoko wa SBL, Phraim Mafuru katika hafla ya chakula cha mchana iliyoandaliwa na kampuni hiyo kuwakutanisha wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari ikiwa ni kubadilishana mawazo kabla ya kuanza kwa Mashindano ya Kombe la Tusker Chalenji yanayotarajia kuanza Novemba 25, 2011.
Akizungumza katika hafla hiyo Mafuru amesema SBL kupitia kinywaji chake cha Tusker imeamua kudhamini mashindano hayo ili kuunga mkono juhudi za kuendeleza mchezo wa soka nchini ambao kiasi kikubwa unapendwa na wengi.
Aidha aliwataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kuzishangilia timu za Tanzania zinazoshiriki katika mashindano hayo ili ziweze kufanya vizuri na kulibakiza tena kombe hilo nyumbani. Pamoja na hayo amewataka kunywa kwa wingi bia ya Tusker ili iweze kufanya vizuri kimauzo na kuendelea kufadhili mpira kwa lengo la kukuza soka nchini.
“Tunavyojitokeza kushangilia kwa wingi, kuiunga mkono pia SBL kupitia kinywaji chake cha Tusker itafanya vizuri hivyo kuendelea kuwekeza kwenye mpira na hata michezo mingine…nawasihi Watanzania tujitokeze kwa wingi,” alisema Mafuru.
Naye Katibu Mkuu wa TFF na Mwakilishi wa Shirikisho la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Angetile Osiah ameipongeza SBL kwa uzalendo iliyouonesha kwa kutumia kiasi kikubwa cha fedha kudhamini mashindano hivyo kuwaomba wananchi wajitokeze kuiunga mkono pamoja na kuzishangilia timu zetu.
Awali Mkurugenzi wa Mahusiano na Mawasiliano wa SBL, Teddy Mapunda akizungumza alivipongeza vyombo vya habari kwa kuonesha uzalendo na kuendelea kuyatangaza mashindano hayo, hivyo kuwaomba waendeleze hali hiyo kwani lengo lililokusudia la kukuza kiwango cha soka litafanikiwa kwa ushirikiano kama huo.
Serengeti imetumia zaidi ya milioni 900 kudhamini mashindano hayo kwa kugharamia gharama mbalimbali pamoja na mafunzo kwa wanahabari watakao nolewa kuripoti mashindano ya Kombe la Tusker.