Kiwango cha maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) katika Halmashauri ya Jiji la Tanga kimeongezeka kwa asilimia 8.7 zaidi ya kile cha kitaifa cha asilimia 5.7.
Kiwango hicho ambacho kimeelezwa kuwa kimekuwa kikipungua kwa kasi ndogo sana, kimezidi hata kile cha mkoa ambacho ni asilimia 4.8.
Akihutubia katika kilele cha Siku ya Ukimwi Duniani na ufunguzi wa maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanganyika kwa Mkoa wa Tanga, Mkuu wa Mkoa, Chiku Gallawa, alisema takwimu hizo ni zile za watu waliojitokeza kupima afya mwaka jana.
Gallawa alisema hali bado inatisha hasa kwa kuzingatia kuwa Ukimwi umekuwa ukiathiri zaidi kundi kubwa la vijana ambao ndio nguvu kazi inayotegemewa katika kukuza uchumi wa taifa.
Alisema iwapo jamii haitakubali kubadili tabia zinazochochea maambukizi ya VVU na Ukimwi ni wazi kuwa idadi kubwa ya watu itaendelea kuathirika.
“Serikali kwa kushirikiana na mashirika mbalimbali ya kimataifa imeendelea na jitihada za kupambana na janga hili lakini jamii ambayo ndio mhusika mkubwa inapaswa kutambua juhudi hizi na kuziunga mkono kwa vitendo ili hatimaye tufikie malengo yaliyokusudiwa kwamba Tanzania bila Ukimwi inawezekana,” alisisitiza Gallawa.
Mratibu wa Ukimwi wa Halmashauri hiyo, Moses Kisibo, alisema tafiti za kisayansi bado zinathibitisha kuwa maambukizi ya VVU na Ukimwi kwa kiwango kikubwa hutokana na ngono zembe.
Kisibo alisema miongoni mwa sababu zinazochangia kuendelea kwa kasi ya maambukizi ya virusi hivyo ni kuendeleza mila na desturi zinazopotosha maadili ya kijamii na kutozingatiwa elimu ya makuzi ya vijana.