SHIRIKA moja la hisani limesema licha ya uhaba mkubwa wa vituo vya afya nchini Sierra Leone, kiwango cha visa vitano vya maambukizi ya ugonjwa wa Ebola kinatokea kila saa nchini humo. Shirika la Kimataifa linalohudumia watoto (Save the Children) linasema kuna jumla ya visa 765 vipya vya Ebola ambavyo vimeripotiwa katika taifa hilo la Afrika Magharibi huku kukiwa kuna vitanda 327 pekee nchini humo.
Wataalam na wanasiasa wanatarajiwa kukutana mjini London ili kujadili mbinu mpya za kutatua tatizo hilo. Ni mlipuko hatari wa ugonjwa huo kuwahi kutokea baada ya kuwaua watu 3338 kufikia sasa. Kuna visa 7,178 ambavyo vimethibitishwa huku mataifa ya Sierra Leone, Liberia na Guinea yakiathirika vibaya. Shirika hilo linasema kuwa ugonjwa huo unasambaa nchini Sierra Leone kwa kasi mno huku visa vipya vinavyoripotiwa vikiongezeka mara mbili kila wiki.
Limesema kuwa hata baada ya maofisa wa afya kukabiliana na mlipuko huo katika eneo moja, ugonjwa umekuwa ukisambaa katika maeneo mengine. Vilevile viwango vya ugonjwa huo havijaripotiwa kama inavyotakikana kwa kuwa watoto wengi wanaendelea kufariki majumbani mwao ama hata barabarani bila kujulikana.
Mapema mwezi huu, Uingereza ilisema kuwa itajenga vituo vya afya vyenye vitanda 700 nchini Sierra leone, lakini vitanda hivyo havitakuwa tayari baada ya wiki moja na kwamba vyengine vitachukuwa miezi kadhaa kukamilika.
Save the Children limesema kuwa iwapo jamii ya kimtaifa haitachukua hatua, raia wengi wataendelea kufariki majumbani mwao mbali na kutishia kuwaambukiza watu wengi wa familia na jamii nzima kwa jumla.
-BBC