Na Mwinyi Sadallah
Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, amesema tabia ya watendaji kufungia sheria na kanuni za uhifadhi wa mazingira katika makabati, ndiyo chanzo cha kuenea kwa uchafuzi wa mazingira visiwani humo.
Maalim Seif, alisema sababu za uchafuzi wa mazingira Zanzibar sio ukosefu wa sheria na kanuni, bali sheria hizo hazitekelezwi na watendaji kwa kuhofia kulaumiwa na wahusika na jamii pale watakapowachukulia hatua, tabia ambayo amesema haina tafauti na rushwa.
Alisema hayo baada ya kushiriki katika kampeni ya kusafisha fukwe za bahari eneo la Mji Mkongwe Zanzibar, iliyofanyika jana kati maeneo ya Malindi, Maisara, Ngazi Mia hadi Mazizini, kazi iliyoandaliwa na Jumuiya ya Mazoezi na Usafishaji Mazingira Zanzibar (Zafiaso).
Alisema Wazanzibari lazima wabadilike na warejee kwenye utamaduni wa kupenda usafi uliodumu kwa miaka mingi, ambao sasa unaanza kutoweka na kusababisha maeneo mengi ya miji ya Zanzibar kukabiliwa na hali ya uchafu.
Alisema vitendo vya uchafuzi wa mazingira Zanzibar vimeanza kuathiri fukwe za bahari na nchi kavu, ambapo kwa upande wa baharini athari kubwa ni uharibifu wa matumbawe ambayo ndio mazalia ya samaki na yanatoa mchango mkubwa kulinda fukwe na maji ya baharini yasiathiri nchi kavu.
Alieleza kwamba kutokana na vitendo vya uharibifu wa matumbawe baadhi ya wavuvi wanalalamikia upungufu mkubwa wa samaki na kuonya kwamba iwapo jamii haitabadilika, madhara kama hayo yatakuwa makubwa zaidi katika siku zijazo.