WAKATI Japani, taifa lenye nguvu kubwa kiuchumi duniani likihaha katika harakati za uokoaji, mamia kwa mamia ya miili watu waliokufa kutokana na tetemeko la ardhi imeendelea kupatikana.
Idadi ya vifo kutokana na tetemeko kubwa la ardhi la kipimo cha 8.9 nchini Japani inaweza kufikia 10,000 katika mkoa wa Miyagi pekee.
Awali polisi ilisema zaidi ya watu 2,000 wamekufa au hawajulikani walipo katika mikoa ilioathirika.
Serikali ya Japan inaendelea na juhudi za uokozi pamoja na kuwaondolea wasiwasi wananchi wake juu ya uwezekano wa kuvuja kwa sumu ya miale ya nyuklia katika mitambo yake miwili iliyoharibiwa na tetemeko hilo.
Hadi sasa imethibitishwa watu 800 wamekufa huko Miyagi na katika maeneo mengine kaskazini mashariki mwa Japani.
Tetemeko hilo la ardhi lililotokea Ijumaa iliyopita na kuandamana na mawimbi makubwa ya tsunami limeelezwa kuwa tukio baya zaidi tangu Vita Kuu ya Pili ya Dunia.
Afisa wa serikali ya mitaa katika mji wa Futaba ulioko mkoa wa Fukushima ameliambia Shirika la Habari la Kyodo kwamba asilimia 90 ya nyumba katika maeneo matatu ya mwambao yamesombwa na mawimbi ya tsunami.
Takriban watu 390,000 wamekimbia nyumba zao wengi wao wakijisitiri katika vituo vya dharura vya jamii na shule.
Wakati huo huo, afisa wa ngazi ya juu wa serikali ya Japani amesema hakuna matatizo kuhusiana na mtambo wake wa nyuklia ulioharibiwa hata kama kuna kiwango fulani cha sumu ya miale ya nyuklia kilichovuja.
Maafisa kwa sasa wanaendelea na juhudi za kuzuia kupanda kwa kiwango cha joto katika mtambo wake huo.
Serikali inasema mtambo wake mwingine nambari tatu pia uko katika hatari ya kuripuka kama ilivyotokea katika mtambo wake namba moja.
Takriban watu 200,000 wamehamishwa umbali wa kilomita 20 kutoka kanda ya salama karibu na mitambo hiyo.
Japani imetoa wanajeshi wake 200,000, wakiwa asilimia 40 ya kikosi chake cha ulinzi kuongoza juhudi ngumu za uokozi na mamia ya meli, ndege na magari yamekuwa yakielekea katika mwambao wa Pasifiki.