Maadhimisho ya Siku ya ‘Mashetani’ Nchini Marekani

 Wana maruhani wakiwa katika wakionesha manjonjo yao. (Picha na Jefferson Siegel/New York daily news) 

 Wana maruhani wakiwa katika wakionesha manjonjo yao. (Picha na Jefferson Siegel/New York daily news) 

KILA ifikapo tarehe 31 Oktoba ni “Siku ya Maruhani” nchini Marekani. Siku hii ijulikanayo kama “Halloween” husherehekewa kila tarehe 31 Oktoba, na ina historia ndefu.
Siku ya Maruhani ilianzia huko barani Ulaya kiasi miaka 2,000 iliyopita ikifungamana na imani za kishirikina. Wazung walipoyavamia mabara ya Amerika walihamia pia na utamaduni mila, desturi, dini, na silka zao – na sema upendavyo. Miongoni mwa hayo ilikuwa ndiyo hii siku ya Maruhani ambayo jina lake la asili ni “Samhein”.
Sherehe za Maruhani  Photograph by treasuredragon/iStock.
Tuyaachie ya historia kwa wanahistoria, lakini kwa ufupi hii iliaminika kuwa ni siku ambayo pepo, majini, maruhani, mazimwi na mizimu au mizuka ya watu waliokufa hurejea hapa duniani katika maeneo yao ya asili na kujichanganya na watu waliohai.
Maudhui kuu ya siku hii ni kutisha, kuadhibu na mauti, ingawaje katika enzi zetu za leo imekuwa ni siku kuu ya watoto zaidi kuliko watu wazima. Sherehe zake hufanyika kuanzia familia, mitaa, makazini na hadi kufikia Ikulu yenyewe. Rejea kwenye toleo la jana la Swahilivilla uone Ikulu ya Marekani ilivyoadhimisha siku hii akiwepo rais Obama na familia yake.
Kama ambavyo kila siku kuu au sherehe huwa zinaaambatana na ada maalum ambazo zikikosekana basi siku hiyo huwa kana kwamba haijatimia, Siku ya Maruhani nayo pia ina ada na desturi zake. Na kama zilivyo sherehe nyingi hapa Marekani siku hii pia nayo imekuwa fursa ya wafanyabiashara kujipatia rizki zao.
Mapambo: Shamra shamra za Siku ya Maruhani huanza mapema, pengine tangu mwezi wa Septemba kwa kuweka mapambo kwenye majumba, mabarabara na hata sehemu za kazi na biashara.
Na kama tulivyotangulia kusema, mapambo yote huwa yanalenga kwenye hali ya kutisha, kuadhibu na mauti. Miongoni mwa mapambo hayo ni buibui na nyumba zao, popo wakining’inia, mifupa na mabufuru ya vichwa vikiashiria watu waliokufa, panga, paka weusi, masanamu ya mizuka au mazombi na vimbwanga vyengine. Almradi kuonesha kuwa nyumba zimesibiwa na maruhani (haunted house). Si hasha ukapita vichochoroni ukakutana na kitu ukashtuka. Kwa ufupi ni kama vile tunavyoona kwenye picha za kutisha (scary movies).
Halloween Live HD Image
Maboga yaliotengenezwa kwajili ya Maruhani
Maboga nayo ni sehemu muhimu katika Siku ya Maruhani. Hukaushwa, kutobolewa kwa mitindo maalum na kupakwa rangi na kuwa katika umbo la kutisha, kisha kutiwa mshumaa ndani. Boga hili maarufu huitwa kandili ya Jack ‘O (jack-o’-lantern). Kiasili, mshumaa uliondani unaashiria roho iliyoko kifungoni ikiadhibiwa.
Mavazi (Costumes): Inaaminika kuwa Wazungu wa kale huko Ulaya, walikuwa wakivaa mavazi ya kutisha katika siku hii ili kuwababaisha pepo, majini, maruhani na mazimwi wanapokuja, wadhani kuwa ni wenzao na hivyo kuwaacha na kutowadhuru. Kwa hivyo mpaka leo mavazi ya siku hii huwa ni ya kutisha, na watu hutembea kama mizuka, mazimwi (mazombi) au mtu aliyechagawa.
Makazini watu huruhusiwa kuvaa mapambo maalum ya kutisha almradi hayahatarishi usalama. Utawakuta watu wamejipaka masinzi, au rangi za ajabu ajabu mwilini, kuvaa masoksi usoni, kuvaa mavazi ya kivita na silaha zao na vikorobwezo vyengine. Baadhi ya sehemu za kazi hufanya mashindano maalum kuchagua mshindi wa mavazi bora ya siku hii.
Trick-or-Treat
Trick-or-Treat: Kama tulivyogusia hapo awali kuwa Siku ya Maruhani imekuwa ni siku kuu ya watoto zaidi kuliko watu wazima. Kwa hivyo, wakati wa jioni watoto wakiwa wamevalia mavazi yao ya kutisha hupita mitaani, nyumba hadi nyumba, kubisha hodi na kutoa mzaha wa vitisho (trick) kwa wenye nyumba iwapo hawatopewa zawadi (treat).
Mara nyingi hupewa zawadi ambayo zawadi maarufu ni peremendi au vitu vyengine vitamu. Baadhi ya watu huweka ishara maalum kwenye milango ya nyumba zao kuashiria kuwa zawadi zimejaa ndani, au huziweka mlangoni kama chano au tambiko kwa maruhani, na watoto wenye bahati ya kupita mwanzo hufaidika, na hivyo mwenye nyumba kunusurika na kitisho, au nyumba yake hunusurika isisibiwe.
Kwa mujibu wa wanahistoria, inaaminika kuwa huko kale, majini na maruhani walipokuwa wakiingia mitaani siku hiyo huko Ulaya, watu walioshindwa kuwababaisha kwa mavazi yao, basi walikuwa wakiwapa zawadi au muhanga ili wawaachie na wasiwadhuru.
Patry ya Maruhani (Photo: Aaron Favila, AP)
Maparty nayo hufanyika, yakitawaliwa na michezo ya kuigiza ambayo maudhui zake kuu ni zile za kutisha, kuadhibu na mauti. Halikadhalika vipindi vya televisheni na redio pia hutawaliwa na maudhui ya Siku ya Maruhani zikiwemo nganu na picha za kutisha.
Baadhi ya watu huitumia vibaya siku hii kwa kufanya vitendo vya kihalifu. Mpaka wakati tukiingia mitamboni bado hatujapata ripoti kamili ya vyombo vya usalama nchini Marekani kukhusu matukio ya kihalifu yaliyoripotiwa hiyo jana. Tuombe salama iwe hakuna mtu yoyote aliyedhurika.
Lakini, ikiwa hakuna matukio yoyote mabaya yaliyotokea nchini humu, basi jinamizi la Siku ya Maruhani kwa mwaka huu litakuwa limeikumba Zanzibar. Kwani kinyume na Marekani na Ulaya ambako maruhani, majini, pepo na mazimwi hushuka kila mwaka, kwa Zanzibar hushuka kila baada ya miaka mitano. Na kwa vile hushuka kila baada ya muda huo, basi yakishuka huwa makali zaidi. Mwaka huu yameshuka yakiwa yamevalia mavazi ya kutisha, masoksi na masinzi nyusoni na silaha nzito nzito na vimbwanga vyengine yakibisha hodi milangoni na kusema “trick-or-trick”.
Wazanzibari walikuwa wamezoea kuyapa peremendi, pipi na zawadi nyenginezo iwapo watashindwa kuvaa mavazi ya kuyababaisha ili yawaachie kuendelea kuishi angalau katika hali duni. Lakini mwaka huu Wazanzibari wamesema ng’o! Wamekataa kutoa chano, na kwa hivyo tayari yamevinjari kutaka kuwadhuru.
Sherehe za hapa na pale zimekuwa zikiripotiwa, na vyombo vya khabari navyo vimekuwa vikitenga muda maalum kutangaza michezo ya kuigiza na nganu zenye maneno ya kutisha kama vile “hatutoi”, “watarudi” na mengineyo.
Lakini Wazanzibari wamesimama kidete na wamekataa kutoa muhanga.
Zanziba imekuwa nyumba iliyosibiwa na maruhani “haunted house”. Ukipita mitaani siku hizi unaweza kumezwa na mazimwi, maruhani, majini au viumbe vyengine vya khatari, na roho za Wazanibari zimo kifungoni zikiadhibiwa bila kosa lolote lile.
Wamekuwa wakitoa muhanga na vyano kwa viumbe hao wa ajabu kwa miaka mingi mpaka khazina zao zimekauka, na sasa hawana walichobakiwa nacho ispokuwa imani zao thabiti kwa Mwenyezi Mungu na nyoyo za kizalendo.
Chanzo; Swahilivilla Blog, Washington D.C