Maadhimisho ya Mtoto wa Afrika

watoto
Na Ngusekela David,

Maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika yamefanyika mwaka huu, kote nchini kwa kila mkoa kufanya maadhimisho hayo huku yakibeba kauli mbiu ya ‘’TOKOMEZA MIMBA ZA UTOTONI: KWA PAMOJA TUNAWEZA’’ lengo likiwa ni kupunguza idadi ya wasichana wanaopata watoto wakiwa na umri wa chini ya miaka 18.

Siku ya mtoto wa Afrika inayoadhimishwa 16/6 kila mwaka ina lengo la kukuza na kutetea haki na ustawi wa watoto, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa kukuza uchumi na kupunguza umaskini (MKUKUTA) wenye vipaumbele mbalimbali kikiwemo cha ustawi wa watoto.

Aidha mikataba mbalimbali imeridhiwa kote Duniani ikiwa ni pamoja na ule ulioridhiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 10, june 1991uliotoa majukumu kwa Serikali kulinda na kuendeleza haki za watoto pia ulisisitiza kuwa familia ndio kitovu cha malezi na uendelezaji wa haki za watoto na umuhimu wa mzazi kumuongoza mtoto kukabili wajibu wake.

Katika hutuba yao kwa mgeni rasmi watoto wa mkoa wa Singida walimuomba mgeni rasmi, wazazi na walezi kuzingatia malezi ya watoto kwa kuwapatia lishe bora,huduma za afya,elimu na chanjo kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano.

Pia waliomba watoto walindwe dhidi ya vitendo viovu kama kubakwa,kulawitiwa,vitendo vya kikatili kama kuchomwa moto,kubandikizwa kesi na kuhukumiwa kama wakubwa,kufanyishwa kazi ngumu kwa kisingizio cha ugumu wa maisha pamoja na tohara kwa watoto wa kike.Waliwashauri wazazi kuwalea watoto wao wenyewe badala ya kuwaachia walezi ambao hawana mapenzi na watoto na kusababisha hayo kutokea.

Akijibu hoja za watoto hao mgeni rasmi katika shughuli hizo Katibu tawala wa Wilaya ya Singida Bwana Bura Ngwandu aliwaasa watoto kuwa waadilifui ili kuepuka ndoa na mimba za utotoni. ‘’mimba za utotoni zinaathari kwa watoto kwani zinaweza kusababisha kifo kwa mtoto anayezaliwa na mama mwenye umri mdogo’’ amesema.Aidha bwana Ngwandu amesema wasichana wanaopata watoto kabla ya kumaliza masomo wana uwezo mdogo wa kuchangia kipato cha kaya hivyo kuongeza umaskini katika ngazi ya kaya.

Pia kukatisha masomo kwa sababu ya ujauzito kunamsababishia msichana kubaguliwa na jamii inayomzunguka ikiwa ni pamoja na wazazi,wanafunzi wenzake pamoja na waalimu kwani jambo hili halikubaliki katika mila za kiafrika hivyo mtoto hupachikwa majina mabaya na yasiofaa.

Hivyo aliitaka jamii kushirikiana katika kutokomeza tatizo hili la mimba za utotoni na kutetea upatikanaji wa huduma nzuri za afya na kusaidia uanzishwaji wa elimu ya stadi za maisha kwa wasichana na wavulana walioko shuleni na nje ya shule.