Maadhimisho ya 68 ya Siku ya Umoja wa Mataifa Yaanza Leo Dar

IMG_0004

 

Naibu Katibu Mkuu wa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Rajabu Gamaha (kulia) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani), Kushoto ni  Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa Tanzania, Alberic Kacou.

IMG_0036

IMG_0020

IMG_0039

 

Picha anuai juu ni baadhi ya waandishi wa habari wakifuatilia mazungumzo ya Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa Tanzania, Alberic Kacou pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Rajabu Gamaha walipozungumza na wanahabari juu ya Siku ya Maadhimisho ya Umoja wa Mataifa.

MAADHIMISHO ya Siku ya Umoja wa Mataifa (UN) yameanza leo jijini Dar es Salaam. Akizungumza na waandishi wa Habari kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Balozi Rajabu Gamaha alisema maandhimisho ya mwaka huu ambayo ni ya 68 yataambatana na matukio muhimu maeneo anuai hivyo kuwataka wananchi na wadau wengine wa maendeleo kujitokeza.

Balozi Gamaha alisema katika maadhimisho hayo yatakayofanyika takribani kwa wiki moja yataambatana na mjadala wa wazi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambao utafanyika na kushirikisha watu wa kada tofauti hivyo kuwataka wananchi kujitokeza kushiriki katika matukio hayo. “UN ni taasisi muhimu sana hapa Tanzania kutokana na shughuli zake…,” alisisitiza Gamaha.

Alisema maadhimisho ya mwaka huu yamebeba kauli mbiu ya ‘Tanzania ya Kesho Tunayoita’ mada ambayo itakuwa sehemu ya mjadala wa wazi. Aliongeza kuwa kutakuwa na maonesho ya shughuli mbalimbali ambayo yatafanyika katika viwanja vya Karimjee na kuwaomba wananchi kushiriki kujionea shughuli anuai zitakazo oneshwa katika maadhimisho.

Aidha alisema siku ya kilele cha maadhimisho yaani tarehe 24, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernald Membe atafanya tukio la kupandisha bendera ya UN ikiwa ni ishara ya kilele cha shughuli hizo muhimu kwa taifa na taasisi yenyewe.

Naye Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa Tanzania, Alberic Kacou akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na maadhimisho hayo, alimpongeza Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete na Watanzania wote kwa kuendelea kuimarisha amani na utulivu na ushirikiano mzuri wanaoutoa kwa taasisi hiyo jambo ambalo linaiwezesha kuendesha shughuli zake vizuri.

Alisema kumekuwa na miradi mbalimbali ambayo UN imekuwa ikiitekeleza kwa Tanzania ili kuhakikisha inashiriki katika kuwaletea maendeleo Watanzania na kuwa chachu ya mafanikio kiujumla. Alisema UN inatekeleza miradi anuai ya kimaendeleo katika nyanja za Elimu, Afya, Utawala Bora, Mazingira na kushiriki kulinda amani, ambapo aliipongeza Tanzanisha kwa moyo wa kuendelea kushiriki katika kulinda amani kwa mataifa mengine ya nje hali ambayo imekuwa ikigharimu walinzi wa amani.