HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE, KWENYE MAADHIMISHO YA MIAKA 75 YA KANISA LA TANZANIA ASSEMBLIES OF GOD, UWANJA WA SOKOINE, MBEYA, TAREHE 13 JULAI, 2014
Dkt. Barnabas Weston Mtokambali, Askofu Mkuu wa
Tanzania Assemblies of God;
Ndugu Mkuu wa Mkoa;
Maaskofu na Wachungaji Wote Mliopo Hapa;
Viongozi Wenzangu;
Ndugu Waumuni;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Pongezi na Shukrani
Nakushukuru Baba Askofu Mkuu kwa kunialika kwenye sherehe zenu za kuadhimisha ya miaka 75 ya uhai wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG). Tukio hili ni muhimu sana kwa maisha ya kanisa lenu na Taifa letu pia. Hii ni miaka 75 ya upendo, uponyaji na uenezaji wa injili nchini. Pia ni miaka 75 ya kueneza dini bila kufarakana na dini nyingine na madhehebu mengine ambayo mliyakuta na yale yaliyowakuta. Sote bila kujali tofauti zetu za kidini na madhehebu tuliyopo tumefaidika na uwepo wenu. Kazi yenu na huduma zenu za kiroho na kijamii mnazozitoa kwa watu wote bila ubaguzi, zimewanufaisha Watanzania wengi.
Naungana na Watanzania wote kukupongeza Baba Askofu, viongozi wa kanisa unaloliongoza na waumini wote wa kanisa hili kwa kutimiza miaka 75. Katika miaka hii 75 mmetimiza matarajio yetu na sote tumefurahia kazi yenu. Umri huu ni mkubwa wa kutosha hivyo ni sahihi kabisa kusema kuwa kanisa hili limeota mizizi na kukomaa. Inafurahisha pia kwamba, mmeendelea kuonyesha ukomavu huo, hekima na busara katika kuchangia kudumisha amani, upendo na mshikamano miongoni mwa Watanzania. Daima mmekuwa wamoja wetu, miongoni mwetu na ndio sababu nasi tunajiona kuwa sehemu kamili ya miaka 75 ya mafanikio ya kanisa lenu. Ndiyo maana pamoja na mambo mengine nimetafuta wasaa kuja kuungana nanyi kusheherekea miaka 75 ya uwepo wenu, na kuwatakia mafanikio makubwa zaidi katika kazi yenu adhimu ya kueneza neno la Mungu.
Uimara wa Kanisa la TAG
Nakupongeza Baba Askofu Mkuu kwa maelezo yako mazuri kuhusu historia ya kanisa hili hapa nchini. Umesema kwamba misingi na nguzo sita za kanisa lenu zimeliwezesha kufikia umri huu kwa mafanikio ya kujivunia. Umezitaja nguzo hizo kuwa ni Ibada; Elimu rasmi ya Kiroho; Utumishi; Uinjilisti; Mfumo wa Kanisa la kienyeji lenye kujitegemea na kuongozwa na maono. Uimara wa nguzo hizi unadhihirishwa na kuthibitishwa na mafanikio makubwa ambayo kanisa lenu limepata.
Inatupa moyo na matumaini makubwa tunaposikia ukiendelea kusisitiza umuhimu wa nguzo hizi sita. Tunafurahia kwa kuwa unazidi kutuhakikishia nia na dhamira njema ya kanisa unaloliongoza katika kudumisha upendo, umoja, amani na kupanua huduma za kiroho na kijamii nchini. Pia, unatupa sababu ya kuziangalia nyakati zilizo mbele yetu kwa matumaini makubwa.
Mabadiliko ya Kijamii na Changamoto za Leo za Dini na Kanisa
Baba Askofu,
Wageni Waalikwa,
Tunasherehekea miaka 75 ya kanisa hili katika mazingira tofauti sana na yale yaliyokuwepo nchini lilipoanzishwa rasmi mwaka 1939. Idadi ya watu ilikuwa ndogo, hali kadhalika idadi ya madhehebu na changamoto za kueneza neno la Mungu nazo zilikuwa ndogo. Kazi kubwa na nzito ilikuwa ni katika kuwafikia wananchi walio wengi ambao wengine hawakuwa wamefikiwa na huduma za Kimisionari na Kiinjili. Ukubwa wa kazi hii haukutokana na ugumu wa watu kupokea huduma ya neno la Mungu bali miundombinu ya kuwafikia huko waliko. Ingawa wananchi wengi walikuwa wakiamini katika dini zao za asili, imani yao kwa Mungu na uadilifu katika maisha yao vilikuwa ni vitu ambavyo vikijidhihirisha katika maneno, mienendo na matendo yao. Vitu hivi viwili, yaani imani na uadilifu vilifanya kazi ya Kanisa kueneza neno la Mungu kuwa nyepesi.
Leo, miaka 75 baadae, nchi yetu imepiga hatua kubwa ya maendeleo. Idadi ya watu imeongezeka, idadi ya waumini imeongezeka, idadi ya madhehebu imeongezeka sana, hali kadhalika idadi ya Maaskofu na siku hizi nasikia kuna hata Manabii. Katika hali ya kawaida, tungetegemea kuwa maovu katika jamii yetu yangepungua sana. Maana, leo tunazo nyenzo za kisasa zaidi za kufanya kazi ya kueneza neno la Mungu. Tunazo televisheni, redio, barabara nzuri, waumini wenye uwezo zaidi kifedha na kielimu. Kinyume chake maovu katika jamii yameongezeka sana kiasi cha kushuhudia hata yale maovu ambayo hatukuwahi kuyafikiria. Baadhi ya hayo hufanywa hata na wale waliopewa dhamana ya kulea watu kimwili na kiroho.
Mmong’onyoko wa maadili umezidi kuwa mkubwa, upendo na kuaminiana kunapungua miongoni mwa wanadamu siku hadi siku. Watu wanazungumzia visasi, kumwaga damu, kutiana vilema, kudhulumiana na kufarakana. Wakati mwingine sisi Serikalini tumekuwa tunalazimika kubadili Sheria na kutunga Sheria kali zaidi. Kwa mfano, tumeongeza idadi ya makosa katika Sheria ya Rushwa kutoka makosa 4 hadi 24, kutunga Sheria ya Makosa ya Kujamiiana (SOSPA) yenye adhabu ya kifungo cha maisha na nyinginezo nyingi. Hivi sasa, tunajiandaa pia kutunga Sheria kali ya kupambana na biashara ya dawa za kulevya. Hata hivyo, idadi ya makosa haijapungua na Magereza yanaendelea kujaa, tena basi, wafungwa na mahabusu walio wengi magerezani ni waumini wa dini zetu kubwa mbili za Ukristo na Uislamu.
Msingi wa Dini ni Imani
Askofu Mkuu,
Wageni Waalikwa;
Nyakati tulizonazo leo zinatutaka sote tufikiri na tuenende tofauti na mazoea yetu. Tunapaswa kutazama upya namna Serikali, Dini na Jamii zinavyowaandaa na kuwalea watu wake kiroho, kielimu na kimaadili. Maana kwa jinsi mambo yalivyo leo, ni dhahiri kuwa kuna mahala ama tumepotoka au tumekosea. Ili kutoka hapa tulipo, hatuna budi Serikali, Dini zetu na Jamii kushirikiana kwa karibu kwani hakuna mmoja wetu anayeweza kuwa na majawabu peke yake. Maana, ukamilifu wa mwanadamu ni kukamilika kwa afya ya mwili, akili na roho.
Nitakuwa mchoyo wa fadhila nisipotambua mchango wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) katika sekta za elimu na maji. Tunawashukuru kwa kujitoa kwenu kuunga mkono juhudi za Serikali katika kutimiza wajibu wake wa kutoa huduma hizi muhimu za jamii. Kuwepo kwa shule za seminari za Faraja kule Kilimanjaro, Ebenezer kule Iringa na sasa kule Eyasi kunasaiadia kutoa fursa kwa watoto wa Kitanzania kupata elimu na maarifa bora. Nimefurahishwa pia na taarifa za mchakato wa kujenga vyuo viwili vya ualimu na miradi ya visima virefu vya maji huko Dodoma, Singida, Same na Manyara. Hatuna maneno ya kutosheleza kuelezea shukrani na furaha zetu kwa mchango wenu huu mkubwa. Nasema asanteni sana. Mola awaongezee maradufu pale mlipopunguza.
Ahadi ya Serikali kwa Kanisa
Sisi kwa upande wa Serikali tunayo dhamira ya dhati ya kutimiza ule wajibu wa kutoa elimu ya hapa duniani, kuhakikisha upatikanaji wa huduma za kijamii na kutunga Sheria na kuunda taasisi za kusimamia sheria hizo. Tunaahidi kuendelea kuhakikisha mazingira mazuri ya kuwawezesha viongozi wa dini na taasisi za dini kutekeleza wajibu wenu wa kujenga watu wetu kiroho. Tutaendelea kuheshimu na kulinda uhuru wa kuabudu na ule wa kuendesha shughuli za kidini. Tunaahidi pia kuendelea kushirikiana na dini zote katika shughuli za kuwaletea maendeleo Watanzania na katika kudumisha amani, umoja na mshikamano. Sisi sote tunayo kazi moja tu ya kuwahudumia wana kondoo wa Bwana. Tofauti yetu ni aina ya huduma. Ninyi za kiroho na sisi za mahitaji yao ya maisha yao duniani. Tunajenga nyumba moja, hatuna sababu ya kunyang’anyana fito.
Ombi kwa Viongozi wa Dini
Ombi langu kwenu, nawaomba mtusaidie sana kujenga imani miongoni mwa watu wetu. Historia ina mifano na mafunzo mengi kuwa dini pekee bila imani haitoshi. Kwa kivuli cha dini, maovu mengi yamefanyika na damu imemwagika. Watu wabaya wametumia mwamvuli wa dini kueneza chuki na kuchochea mifarakano katika jamii. Tusiruhusu hali hii ikaendelea katika jamii zetu. Turejeshe imani miongoni mwa jamii yetu, kwa kutoa msisitizo katika kulea mioyo ya watu wetu. Jamii yenye watu wenye imani, watu hupendana, husikilizana, husameheana na huishi kwa amani. Tukifika hapo, hata sheria na taasisi zetu za kusimamia sheria na kutoa haki zitapungukiwa na mzigo mkubwa zinazoubeba leo.
Katiba Mpya
Baba Askofu Mkuu;
Ndugu Waumini;
Baba Askofu Mkuu ameelezea masikitiko ya Kanisa lenu kuhusu kukwama kwa mchakato wa Katiba, na ametoa rai kwa wadau wote kurejea Bungeni mapema mwezi ujao. Masikitiko yenu ndiyo masikitiko yangu na ndiyo masikitiko ya Watanzania wote. Rai yenu ndiyo yangu na ndiyo ya Watanzania wote ambao matumaini yao wameyaweka kwenye mchakato huo kuwapatia Katiba mpya inayolingana na wakati tulionao na mbele tuendako. Nafarijika kusikia kuwa nanyi viongozi wetu wa dini mkizisihi pande zote kurejea Bungeni na kumaliza tofauti zao kwa mazungumzo ndani ya Bunge. Hamko peke yenu. Watu wengi wameelezea umuhimu wa Wajumbe kurejea Bungeni. Wametumia hoja mbalimbali na kuelezea mantiki zenye kushawishi wale waliotoka Bungeni kurejea bila mafanikio. Pengine mkisema ninyi watu wa Mungu na kuzungumza na mioyo yao wataitikia na kuwasikia.
Napenda kuwahakikishia kuwa matumaini yenu ndiyo matumaini yangu, na ndiyo matumaini na matarajio ya Watanzania wenzetu wengi, kwamba tupate Katiba Mpya. Wakati mwingine nia hii njema imekuwa ikipotoshwa kwa makusudi. Napenda kurudia na kusisitiza kuwa nilibuni wazo na kuanzisha mchakato huu kwa lengo la kuwapatia Watanzania Katiba Mpya iliyo bora zaidi ya tuliyonayo sasa. Tulitengeneza misingi mizuri ya kutufikisha hapo. Kama mtakavyokumbuka, tulianza kwa kutunga Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Pamoja na changamoto zilizokuwepo wakati wa mchakato wa kutunga Sheria hiyo, tarehe 18 Novemba, 2011, Bunge la Jamhuri ya Muungano likapitisha Sheria hiyo.
Kwa mujibu wa Sheria hiyo, mchakato wa kuunda Katiba Mpya ulipangwa kuanza kwa kuunda Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Tume hiyo ilipewa jukumu la kusikiliza maoni ya wananchi na taasisi mbalimbali katika jamii, kisha kutengeneza Rasimu ya Katiba Mpya inayotokana na maoni ya wananchi pamoja na utafiti na maoni ya Tume. Baada ya Tume kukamilisha kazi yake, Sheria imeagiza kuwa Rasimu hiyo ifikishwe kwenye Bunge Maalumu la Katiba kujadiliwa na Katiba Mpya kutungwa. Ukamilifu wa mchakato wa kupata Katiba mpya ni pale itakapopitishwa na wananchi, ambao ndiyo wenye mamlaka ya mwisho kuhusu Katiba hiyo kwa kupiga kura. Mchakato utahitimishwa kwa wananchi kupiga kura ya maoni.
Babab Askofu Mkuu;
Kama sote tujuavyo, tarehe 18 Februari, 2014 Bunge Maalumu la Katiba lilianza kwa kuchagua Mwenyekiti wa Muda, kuapisha Katibu na Naibu Katibu kisha kuwaapisha Wajumbe. Baada ya hapo ilifuatia kazi ya kutunga Kanuni za kuendesha Bunge lenyewe. Walipomaliza kutengeneza Kanuni wakachagua Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Bunge hilo. Lakini kabla ya kuanza kazi ya kujadili Rasimu ya Katiba walimalizia mjadala wa jambo waliloliacha kiporo kwenye Kanuni ambalo lilihusu upigaji wa kura uweje: wa Siri au Wazi.
Askofu Mkuu na Ndugu Waumini;
Baada ya kukamilisha Kanuni, ndipo tarehe 18 Machi, 2014 Mwenyekiti wa Tume alipowasilisha Rasimu ya Katiba Mpya katika Bunge na tarehe 21 Machi, 2014 nililizindua rasmi Bunge Maalumu la Katiba. Baada ya hapo ndipo Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba walianza kazi ya kujadili Rasimu. Kwa mujibu wa Kanuni za Bunge Maalumu, Wajumbe waligawanywa katika Kamati 12 ili kutoa muda wa kutosha kwa Wajumbe kutoa maoni yao kuhusu vifungu mbalimbali vya Rasimu.
Kwa uamuzi wa Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba walikubaliana kuanza Sura ya Kwanza na ya Sita ya Rasimu. Busara iliwatuma wafanye hivyo kwa sababu hizo ndizo sura mama za Rasimu, kwani ndizo zinazotambulisha na muundo wa Muungano. Sura nyingine zilizosalia zinahusu namna ya kuendesha shughuli mbalimbali za taifa na za Serikali ambazo zinatawaliwa na aina ya nchi na Muundo wa Muungano tuutakao. Walikubaliana kuwa watumie siku 14 katika Kamati kisha warudi kwenye Bunge zima kupokea taarifa ya maoni na mapendekezo ya kila Kamati. Katika kuwasilisha taarifa walikubaliana katika Kanuni kuwa maoni ya wengi yatawasilishwa kwa dakika 40 na maoni ya wachache kwa dakika 20. Aidha, kwa upande wa wachache walipewa dakika nyingine 30 kutoa ufafanuzi wa maoni yao. Kwa maneno mengine walio wengi wamepewa dakika 40 kutoa maoni yao na wachache dakika 50 za kutoa maoni. Hivyo basi, Kanuni zimetoa fursa ya kutosha kwa kila upande kutoa maoni yake na upande wa Kamati ya upinzani wamepewa dakika 10 zaidi ya upande wa Chama tawala.
Baadhi ya Kamati ziliongezewa muda baada ya kushindwa kumaliza kazi ndani ya siku 14. Kwa sababu hiyo ilichukua siku 19 kwa Kamati zote kumaliza kazi ya kujadili Sura ya Kwanza na ya Sita ya Rasimu. Kila Kamati ilipiga kura kwa utaratibu wa kura za Wajumbe wa Tanzania Bara na Zanzibar wakipiga kwa upande wao.
Baada ya hapo, tarehe 10 Aprili, 2014, Bunge Maalum la Katiba lilikutana tena katika kikao cha Wajumbe wote na kuanza kupokea taarifa za Kamati. Ilipofika tarehe 13 Aprili, 2014 taarifa za Kamati zote 12 zilikuwa zimewasilishwa kwa maana ya maoni ya wengi na ya wachache. Tarehe 14 – 25 Aprili, 2014 mjadala wa taarifa za Kamati uliendelea Bungeni. Katika hali isiyokuwa ya kutarajibiwa tarehe 16 Aprili, 2014 Wajumbe wa kutoka baadhi ya vyama vikiwemo vyama vya CHADEMA, NCCR Maguezi na CUF walitoka nje ya Bunge na kusema hawatarudi tena. Walitoa sababu ya kufanya hivyo ni lugha ya matusi na kejeli. Hawakutoa masharti ya kurudi. Hapo ndipo Bunge Maalumu la Katiba lilipoingia katika mgogoro uliopo sasa.
Baba Askofu Mkuu;
Baada ya taarifa ya Kamati zote 12 kupokelewa kinachofuatia, kwa mujibu wa Kanuni za Bunge Maalumu, ni Wajumbe kufanya uamuzi kwa kupiga kura kwa sharti la theluthi mbili ya Wajumbe wa kutoka pande zote mbili za Muungano kukubali. Hata hivyo, kwa mujibu wa Kanuni, kabla ya kufanya hivyo Bunge litapokea taarifa ya Kamati ya Uandishi kuhusu marekebisho ya kufanywa katika Sura hizo mbili. Kamati ina Wajumbe wa pande zote mbili za Muungano na kambi mbili za siasa na Wajumbe wa kutoka kundi la 201.
Kwa maneno mengine kazi ya msingi kuhusu Sura ya Kwanza na ya Pili imekwishafanywa. Kilichobaki ni kupiga kura. Kazi hiyo iko mashakani kwa sababu ya Wajumbe wa vyama hivyo kutoka Bungeni. Wakierejea na kura kupigwa mchakato utaingia hatua mpya. Na, iwapo watakubaliana kuhusu sura hizo mbili kazi iliyosalia haitakuwa na ugumu sana kama hii ya Muundo wa Muungano.
Baba Askofu Mkuu;
Bahati nzuri kuanzia wiki iliyopita wawakilishi wa vyama vya CCM, CHADEMA, CUF, NCCR-Mageuzi wamekuwa wanakutana kwa juhudi za Msajili wa Vyama vya Siasa. Nimeambiwa bado wanaendelea na mazungumzo. Napenda kutumia nafasi hii kutoa pongezi za dhati kwa viongozi wa vyama hivyo kwa uamuzi wao wa kukutana na kuzungumzia namna ya kusonga mbele. Hivyo ndivyo uongozi unavyotakiwa kuwa. Tunatoa pongezi maalumu kwa Msajili wa Vyama vya Siasa, Mheshimiwa Jaji Mutungi kwa kufanya uamuzi mzuri wa kuwakutanisha viongozi wetu hao.
Baba Askofu Mkuu;
Wageni Waalikwa;
Maombi yangu kwenu ni kuwaombea viongozi wetu wawe na mazungumzo mazuri na yenye mafanikio. Wakubaliane juu ya kuendelea na kuukamilisha mchakato katika siku 60 za nyongeza kuanzia tarehe 5 Agosti, 2014. Tuombe kwa nguvu zetu zote ili Bwana Mungu awaongoze viongozi hao wapate muafaka utakaoliwezesha taifa kupata Katiba mpya nzuri inayotekelezeka. Katiba itakayodumisha umoja, mshikamano na upendo miongoni mwa watu wa nchi yetu licha ya tofauti zetu za rangi, kabila, dini na maeneo tutokako. Katiba itakayodumisha amani na utulivu nchini na kuchochea maendeleo ya nchi yetu yatakayojumuisha na kunufaisha watu wote. Katiba itakayolinda haki za binadamu ikiwemo uhuru wa kuabudu.
Wakati nawaomba viongozi wa dini kuwaombea viongozi wa CCM, CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi wapate baraka na maongozi ya Mola wetu, nawaomba Watanzania wenzagu tuwape nafasi viongozi wetu hao wazungumze kwa utulivu. Hebu kwanza tuache maneno maneno yatakayowachanganya. Maana siku hizi wasemaji wamekuwa wengi na kauli nyingi na nyingine ni za upotoshaji na uchochezi. Kwa sasa tuwaache wazungumze. Tuwaombee wakubaliane kwani siyo tu tutapata Katiba bali pia tunaiepusha nchi yetu dhidi ya machafuko na kuvunjika kwa amani.
Hitimisho
Baba Askofu Mkuu;
Maaskofu, Wachungaji, Waumini naWageni Waalikwa;
Kwa kumaliza napenda kurudia kushukuru kualikwa katika siku hii adhimu. Mmenipa heshima kubwa ambayo nitaikumbuka daima. Ninawahakikishia ushirikiano wangu binafsi na ule wa Serikali ninayoiongoza katika kuwezesha Kanisa lenu kufanya kazi yake kwa ufanisi. Nimepokea maombi ya Kanisa kwangu kuhusu kiwanja, shule zilizotaifishwa na ukiritimba katika usajili wa shule za Kanisa. Nikiri kuwa, maombi haya yanatawaliwa na sheria, kanuni na taratibu hivyo, si rahisi kwangu kuyatolea amri ya papo kwa papo. Naahidi kuyachukua na kuangalia uwezekano wa kuyapatia majawabu. Nitawapeni majibu. Aidha, hongereni kwa kutimiza miaka 75 yenye mafanikio makubwa yanayoonekana.
Asanteni sana kwa kunisikiliza.