*Maonesho ya shughuli za JWTZ yavutia wananchi
Na Joachim Mushi
SHEREHE za Maadhimisho ya Miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara zilizofanyika leo jijini Dar es Salaam katika Uwanja wa Uhuru zimefana kwa kiasi kikubwa baada ya kupambwa na maonesho ya Majeshi ya Ulinzi na Usalama wa nchi.
Sherehe hizo zilizoongozwa na Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete zimeambatana na maonesho ya zana za kivita za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), na kazi zao, maonesho ya kazi za Jeshi la Polisi kwa baadhi ya vikosi na gwaride maalumu lililoandaliwa kwa shughuli hizo.
Akihutubia mara baada ya shughuli mbalimbali, Rais Kikwete amesema Tanzania imetoka mbali na inamaendeleo ya kuridhisha ukilinganisha na kipindi ambacho ilikuwa chini ya wakoloni ambao hawakuacha chochote cha kujivunia sasa.
Amesema maendeleo ya kimiundombinu ambayo imetapakaa na kuimarika kwa sasa ni moja ya mambo ya kujivunia katika maadhimisho hayo, hivyo kutaka wananchi waendelee kushirikiana na kudumisha umoja kwa nia ya kuleta maendeleo zaidi.
Aidha amewataja waasisi 15 wa Uhuru wa Tanzania ambao amesema wanastahili pongezi kubwa kwani ndiyo waasisi wa mafanikio yote. Waasisi hao aliowataja katika hotuba yake fupi uwanjani hapo ni pamoja na Julius Kambalage Nyerere, Ali Sykes, Lameck Makaranga, Gosbert Milinga, Gelmandus Pacha, Jeseph Kimalando, Japhet Kirilo, Abubakar Ilanga, Saadan Kandoro, Suleiman Kitwara, Kisunguta Kabara, Chewa Said Chewa, Dosa Aziz, Patrick Kunambi, Joseph Kasela Mbantu, John Rupia, Abdulah Sykes.
Amesema Watanzania wana kila sababu ya kusherehekea siku ya leo kwani ni tukio la kusherehekea nusu karne ya mafanikio makubwa ambayo Taifa limeyapata tangu Uhuru.
“Tunasherekea ushindi tulioupata katika kukabiliana na changamoto mbalimbali tulizokubana nazo katika miaka hiyo 50, tunasherekea jinsi tulivyojipanga kukabiliana na changamoto zilizopo mbele yetu,” alisema Kikwete katika hotuba yake.
Amesema katika miaka 50 iliyopita Tanzania ina kila sababu ya kujivunia kwani imeweza kulinda uhuru na kudumisha amani ya Watanzania hata katika mipaka yake yote. Alisema licha ya Tanzania kuwa na makabila 128 lakini imeweza kuishi kwa amani, umoja na ushirikiano jambo ambalo ameeleza ni la kujivunia kimafanikio.