Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ilifanya kikao chake cha kawaida mjini Dodoma Mei 21, 2013 chini ya Mwenyekiti wa CCM Rais Jakaya Mrisho Kikwete. Pamoja na mambo mengine Kamati Kuu ilijadili na kutafakari masuala mbali mbali yanayohusu Uchumi, Ustawi wa Jamii na Maendeleo ya Taifa.
MIGOGORO YA WAKULIMA NA WAFUGAJI
Migogoro ya wakulima na wafugaji imekuwa mingi na imeenea sana katika taifa letu. Migogoro hii inatokana na sababu nyingi: mabadiliko ya tabia nchi; ongezeko la idadi ya watu na mifugo. Kamati Kuu inasikitishwa na kuendelea kwa migogoro hii ambayo imekuwa tishio la amani na usalama katika jamii, na pia kusababisha wakulima kupata hasara baada ya mazao yao kuliwa na mifugo. Tumeishuhudia migogoro hii mkoani Morogoro hivi karibuni, katika ziara ya Katibu Mkuu Ndugu Abdulrahman Kinana na imeripotiwa katika maeneo mengine ya nchi yetu.
Kamati Kuu inaiagiza Serikali kuishughulikia na kuitafutia ufumbuzi wa kudumu migogoro hii. Kamati Kuu inaiagiza Serikali kuharakisha zoezi la kutenga maeneo kwa ajili ya wakulima na wafugaji na kujenga miundombinu ya malisho, maji, na majosho ili kuwezesha wafugaji kutohamahama na mifugo yao.
KULINDA HIFADHI
Kamati Kuu imezungumzia suala la mahusiano kati ya Hifadhi za taifa, wafugaji na wananchi waishio katika vijiji vinavyozunguka Hifadhi hizo. Kamati Kuu inatambua umuhimu wa Hifadhi kwa manufaa ya taifa letu na vizazi vijavyo. Inasisitiza msimamo wake wa kuzilinda Hifadhi za taifa sanjari na kuanzisha na kuendeleza mahusiano hayo.
Kamati Kuu inaiagiza Serikali kuwashirikisha wananchi katika kutenga maeneo ya Hifadhi, kulinda maeneo ya wanyama pori na kutenga maeneo ya malisho ili kuondosha migogoro isiyo ya lazima katika maeneo yanayozunguka Hifadhi.
ZAO LA KOROSHO
Kamati Kuu ilijadili matatizo yanayolikabili zao la korosho ambayo ni: kuyumba kwa bei ya korosho, malipo ya wakulima kuchelewa, tozo nyingi wanazolipishwa wakulima na udhaifu wa baadhi ya vyama vya ushirika.
Tatizo hili limedumu kwa muda mrefu na linastahili kushughulikiwa kwa njia ya kipekee.
Kwa kutambua kwamba wapo baadhi ya viongozi na watendaji wa Serikali, viongozi wa vyama vya ushirika na wafanyabiashara binafsi wanaochangia katika kuendeleza matatizo yanayowakabili wakulima wa korosho:
Kamati Kuu inatamka kwamba hali hii haivumiliki. Kamati Kuu inaitaka Serikali kukaa na wadau wote na kuchukua hatua zitakazotoa ufumbuzi wa kudumu wa matatizo haya kwa zao la korosho. Kamati Kuu pia inaitaka Serikali kuwachukulia hatua za kisheria hao wote wanaochangia kuendelea kwa matatizo haya kwa wakulima wa korosho.
MIGOGORO YA KIDINI
Kamati Kuu imepokea taarifa ya namna migogoro ya kidini inavyoshughulikiwa na hatua zinazochukuliwa. Kamati Kuu inaipongeza Serikali na vyombo vya dola kwa namna inavyoendelea kukabiliana na wahalifu wanaotumia mgongo wa dini kuanzisha vurugu na uvunjifu wa amani katika nchi yetu. Kamati Kuu inatoa mwito kwa Watanzania kukataa vitendo vyote vinavyochochea migogoro ya kidini; wananchi wajihadhari na watu waovu wenye nia mbaya ya kuligawa taifa letu.
Pamoja na jitihada za vyombo vya dola hadi sasa, Kamati Kuu inaitaka Serikali iandae mkakati wa kuzuia migogoro ya kidini kabla haijajitokeza.
MAKAMPUNI NA VIWANDA VILIVYOBINAFSISHWA
Kamati Kuu imetafakari hali ya viwanda hivi. Ni muongo mmoja umepita tangu ubinafsishaji ulipokamilika. Kuuzwa kwa mashirika na viwanda vya umma kwa watu na makampuni binafsi kumekuwa na matokeo ya aina mbili: yako yale yaliyobinafsishwa na yakawa na maendeleo mazuri na kuchangia uchumi wa Taifa. Na
yako ambayo yanaendeshwa kwa kiwango cha chini au yamefungwa.
Kamati Kuu inasikitishwa na hali hii, kwani viwanda vilivyofungwa ni vile vilivyokuwa vikifanya kazi muhimu ya uzalishaji.
Viwanda hivi ni vya korosho, usindikaji wa pamba, mafuta ya kula, viwanda vya mazao ya ngozi, na vinginevyo. Hali hii inalikosesha Taifa fursa za ajira, kukua kwa mapato, kuimarika kwa uzalishaji na kuongezeka kwa uuzaji wa bidhaa zilizosindikwa na kuzalishwa nchini.
Imedhihirika kuwa wafanyabiashara waliochukua viwanda hivyo ndiyo hao hao wanaofanya biashara ya kununua mazao ya kilimo na mifugo na kuuza nje kama bidhaa ghafi, wakati huo huo wakiwa wamevifunga viwanda hivi.
Kamati Kuu inaiagiza Serikali kufanya tathmini ya viwanda vilivyobinafsishwa ili kuvitambua vile vilivyofungwa, na kuwataka waliouziwa wavifungue na iwapo watashindwa kutimiza masharti yaliyowekwa, Serikali iandae utaratibu wa kuwapa watu wenye uwezo wa kuviendesha.
WAKULIMA WADOGO WA MIWA –
Kumekuwapo na migogoro ya muda mrefu kati ya wakulima wadogo wa miwa na Kiwanda cha Sukari cha Mtibwa mkoani Morogoro. Matatizo haya yameshughulikiwa na watendaji mbalimbali bila ya kupatikana kwa ufumbuzi wa kudumu.
Kamati Kuu inaiagiza Serikali kuushughulikia mgogoro huu na kuyapatia ufumbuzi wa kudumu matatizo ya wakulima wadogo wa miwa haraka iwezekanavyo.
PEMBEJEO ZA KILIMO
Chama kimejiridhisha kuwa suala la utoaji wa pembejeo za kilimo ni zuri na lenye mafanikio. Hata hivyo Kamati Kuu imepokea taarifa kuhusu matatizo yanayohusiana na usambazaji wa mbolea ya ruzuku.
Kwa baadhi ya maeneo mbolea ya ruzuku imekuwa ikitolewa kwa watu wasiohusika na wakati mwingine walanguzi wamekuwa wakiingilia kati ili kujinufaisha nayo.
Kamati Kuu inaiagiza Serikali kusimamia kwa umakini na kutafuta utaratibu bora zaidi na wenye tija wa kuwafikishia wakulima mbolea, kwa wakati na kwa uhakika.
MRADI WA UJENZI WA NYUMBA ZA WATUMISHI
Kamati Kuu imepokea taarifa na kuipongeza Serikali kwa kutayarisha mpango kabambe wa ujenzi wa nyumba za watumishi wake. Mpango huu utatoa fursa kwa wafanyakazi ya kupata mikopo yenye masharti nafuu na hivyo kuwawezesha kuwa na makaazi yenye uhakika.
Kamati Kuu imeitaka Serikali kuwasilisha utekelezaji wa maagizo haya mara kwa mara.