Maabara ya Mkemia Mkuu Yabaini kg 6,428 za ‘Unga’
Na Fatma Salum MAELEZO
WAKALA wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali imefanikiwa kubaini jumla ya kilogram 6,428.12 za sampuli mbalimbali za dawa za kulevya kwa kipindi cha kuanzia Januari hadi Desemba 2013.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi ya Makosa ya Jinai na Vinasaba kutoka Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Bi.Gloria Omari katika mkutano na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam.
Bi Gloria alisema kuwa kiasi hicho cha madawa kimepatikana baada ya uchunguzi wa majalada 208 yaliyopokelewa na kufanyiwa uchunguzi katika mwaka huo.
“Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali umefanya Uchunguzi wa vielelezo vidhaniwavyo kuwa ni dawa za kulevya ambapo majalada 208 yaliyopokelewa kwa mwaka 2013 na kubaini jumla ya kilogram 6,428.12 za dawa hizo”Alsema Bi. Gloria.
Akitaja idadi ya majalada na sampuli za dawa hizo Bi Gloria alisema kuwa dawa aina ya Bangi imeongoza kwa kuwa na kiasi kikubwa cha uzito wa sampuli ikiwa na kilogram 3765.12 kwa idadi ya majalada 72 wakati Heroin imeongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya majalada ambapo majalada 112 yalichunguzwa na kilogram 46.67 ziligunduliwa.
Aina nyingine ya dawa zilizotajwa ni Cocaine ikiwa na idadi ya majalada mawili yaliyochunguzwa na kilogram 4.22 ziligunduliwa, majalada 21 ya mirungi yalichunguzwa na kupatikana kilogram 2579.8 na jalada moja la Ephedrine lilikuwa na kilogram 32.31.
Bi Gloria aliongeza kuwa shughuli za uchunguzi wa sampuli za dawa hizo umesaidia utoaji wa ushahidi mahakamani pamoja na kupambana na usafirishaji wa dawa za kulevya.
Akijibu swali la waandishi wa habari Mkuu wa kitengo cha Sayansi ya Makosa ya Jinai Kemia kutoka Ofisi hiyo Bw. Elias Mulima alibainisha kuwa kuna uhalali wa matumizi ya dawa aina ya Cocaine hospitalini kama tiba hasa kwa wagonjwa wenye maumivu makali na wanaofanyiwa upasuaji.