Na Rebecca Kwandu
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), George Simbachawene amewaagiza Wakuu wa Mikoa kuhakikisha wanakusanya mapato vizuri kwa kutumia Mfumo wa Kielektroniki wa Ukusanyaji wa Mapato na kutumia vizuri fedha zilizokusanywa ili kuwaletea maendeleo wananchi katika mikoa yao.
Akizungumza katika kikao kati yake na Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa cha kujadili mwelekeo wa bajeti za Mikoa na Halmashauri iliyofanyika katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam hivi karibuni, Simbachawene aliwataka Wakuu wa Mikoa kutumia umahiri na ustadi zaidi katika kubuni vyanzo vipya vyama pato zaidi ya vile vilivyozoeleka kila siku ili kupata fedha za kutekeleza shughuli za maendeleo katika maeneo yao.
“Mipango ya bajeti zetu lazima zinakisi matatizo yaliyopo, hakikisheni rasilimali chache zinazopatikana zinatumika vizuri na pia hakikisheni Kuwa kila fedha inayopatika na inawekezwa katika eneo husika na kwa kufanya hivyo maendeleo yataonekana.” Alisema Waziri.
Simbachawene aliwataka Wakuu wa Mikoa kuwatumia Wakuu wa Wilaya katika maeneo yao kutatua kero na migogoro ya wananchi kwani alisema kwa kufanya hivyo itaepusha wananchi kufikisha malalamiko yao ngazi za juu kwa kuwa tayari matatizo yao yatakuwa yameshughulikiwa katika ngazi za chini.
“Migogoro mingi inayowasilishwa na wananchi inahusu dhuluma, migogoro ya ardhi na kutotendewa haki kwa wananchi. Ukiona wananchi wanakuja juu kuleta malalamiko ujue huko chini hawakushughulikiwa vizuri. Jaribuni kumaliza matatizo ya wananchi huko chini na kuwafanya wananchi kuishi kwa amani na furaha,” alisisitiza Simbachawene.
Waziri wa Nchi pia aliwataka Wakuu wa Mikoa kukuza ajira katika maeneo yao kwa kuanzisha viwanda vidogo na vya kati ili kuwaletea vijana ajira na kuisaidia serikali kufikia lengo lake la kuwa nchi yenye uchumi wa kati baada ya kila Mkuu wa Mkoa kutafsiri matarajio ya Serikali Kuu kwa vitendo.
“Anza kutekeleza malengo kwa kuangalia dira ya serikali ya kuifanya nchi yetu kufikia uchumi wa kati na wakati unapoanza kutekeleza mapema anza kuona kama kuna vikwazo vya kufikia lengo na kuliwasilisha sehemu husika ili serikali ione namna ya kukusaidia kufikia lengo. Alieleza Simbachawene.
Aidha, aliwaagiza Wakuu wa Mikoa kuhakikisha wanasimamia vizuri suala la utoaji wa Elimu Msingi bila malipo pamoja na kuhakikisha Mamlaka za Serikali za Mitaa hazizalishi madeni na hivyo kutoruhusu madeni kuongezeka. Katika kikao hicho Wakuu wa Mikoa pia waliwasilisha kwa Waziri wa Nchi-TAMISEMI taarifa za zoezi la uhakiki wa watumishi hewa katika mikoa yao ambapo Waziri Simbachawene alizipokea na alieleza kuwa ataziwasilisha kwa Waziri wa Utumishi kwa ajili ya kuziweka vizuri na baadaye zitawasilishwa kwa Rais Dk. John Pombe Magufuli.