M23 Kusitisha Mapigano, Wachina Wakamatwa na Meno ya Tembo Tanzania

Mzigo wa meno ya Tembo.

Mzigo wa meno ya Tembo.

KIONGOZI wa wapiganaji wa kundi la M23 Mashariki mwa Jamhuri ya Demokrasi ya Congo ametangaza kuwa watasitisha mapigano katika vita vyao na Jeshi la Serikali. Bertrand Bisimwa alisema kwenye taarifa yake kwamba anawasihi wapiganaji wote kusitisha mapigano na wanajeshi, ili kuwezesha kuanza kwa mazungumzo ya amani.

Hata hivyo wakati kauli hiyo ya M23 ikitolewa wanajeshi wa serikali, wakisaidiwa na kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa, hivi karibuni walijigamba kuwarudisha nyuma wapiganaji na kuwatoa katika ngome zao nchini. Mazungumzo ya amani yanafanywa mjini Kampala, Uganda.

Wakati huo huo; raia watatu wa nchini China wamekamatwa nchini Tanzania huku wakiwa na meno 706 ya tembo, ikiwa inakadiriwa kuwa ni sawa na tembo 353 waliouawa katika hifadhi mbalimbali nchini humo.

Pia watuhumiwa hao wa Kichina wamekutwa na fedha taslim shilingi milioni 30.2 za Kitanzania, sawa na zaidi ya dola elfu 18 za Kimarekani. Kwa mujibu wa Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki akifuatana na kikosi maalum cha Polisi, waliwanasa Wachina hao katika makazi yao jijini Dar es Salaam.

Waliokamatwa na meno hayo ya tembo wametajwa kuwa ni Chen Jinzha, Huang Qin na Xu Fujie wote kutoka mji wa Guangdung nchini China.

Raia hao wa China wamekuwa wakiishi katika nyumba walimokamata meno ya tembo kwa miaka mingi huku wakijifanya kuendesha biashara ya vitunguu swaumu nchini Tanzania kutoka China huku wakisafirisha nje makombe ya konokono wa baharini.

Akizungumza na waziri Kagasheki, mtuhumiwa Huang Qin amesema shehena yote iliyokamatwa ndani mwake ilikuwa ikiletwa kidogo kidogo na rafiki yake ambaye hakumtaja jina. Kukamatwa kwa meno haya ya tembo Jumamosi, kumekuja wakati tayari serikali imetangaza kusitisha “Operesheni Tokomeza Ujangili”, ambayo ililenga kunusuru wanyama walio hatarini kutoweka kutokana na kuuawa katika hifadhi za taifa nchini Tanzania. Wanyama wanaolengwa zaidi na majangili kutokana na meno yao na pembe ni tembo na faru.

Matukio ya kukamatwa kwa meno ya tembo kutoka Afrika Mashariki yamekuwa yakiripotiwa kila mara. Oktoba, 20, 2012, tani nne za meno ya tembo yenye thamani ya dola milioni 3.4 za Kimarekani yalikamatwa Hong Kong, yakidaiwa kusafirishwa kutoka Kenya na Tanzania.

Pia Agosti 16 mwaka huu polisi wa Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, walimkamata raia mmoja wa Vietnam akiwa na meno ya tembo yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 18 sawa na dola za Kimarekani zaidi ya elfu 11, yakisafirishwa kwenda nje.
-BBC