Lumumba: Miaka 52 ya Kifo Chake, Afrika Ipo Vile vile

Patrice Lumumba

Na Zitto Kabwe

‘MSINILILIE, wazalendo wenzangu, najua kuwa nchi yangu, inayoumia sana hivi sasa, itaweza kulinda Uhuru wake. Idumu Kongo! Idumu Afrika’.

‘…hakuna mateso wala vitendo vyovyote vya kinyama vitakavyonifanya kuomba huruma, ni bora kufa kwa heshima, nikiamini kabisa na kujiamini kuhusu hatma ya nchi yangu kuliko kuishi kwenye utumwa na kuvunja misingi yangu. Ipo siku historia itasema;sio historia iliyoandikwa Umoja wa Mataifa, Washington, Paris au Brussels, lakini historia itakayofundishwa katika nchi zilizoondoa ukoloni na vibaraka wake. Afrika itaandika historia yake iliyojaa utuna heshima’

Haya ni maneno kutoka kwenye barua ya Patrice Lumumba kwenda kwa mkewe Pauline aliyoandika akiwa kwenye selo yake gerezani siku chache sana kabla hajauwawa. Leo tarehe 17 January, ndio siku ambayo Lumumba aliuwawa kwa kupigwa risasi na mwili wake kuzikwa mahala kusikojulikana katika Jimbo la Katanga huko Kongo. Lumumba alikuwa Waziri Mkuu wa Kwanza wa Kongo aliyeleta uhuru kwa Taifa hilo na Mwanamapinduzi wa kweli ambaye Afrika ilinyanganywa mapema sana ikiwa anahitajika sana.

Patrice Emery Lumumba alikuwa Waziri Mkuu wa Kongo akiwa na umri wa miaka 37 tu na kwa kweli mabeberu hawakumruhusu kuongoza nchi yake kwa uhuru kuanzia siku ya kwanza ya Uhuru wa Taifa hilo. Akiwa kijana wa miaka 27 alianza mapambano ya kupigania Uhuru wa nchi yake, alifungwa, alipigwa, aliteswa na kudhalilishwa kwa kila namna na maafisa wa Kibeligiji lakini hakukata tamaa na alihakikisha Taifa lake linapata ukombozi wa kweli.

Mabeberu, kwa tamaa ya utajiri wa Kongo kamwe hawakutaka nchi hiyo ipate uhuru wa kweli. Kwa kutumia vibaraka wao kama Tshombe, Kasavubu na Mobutu, Wabeligiji na rafiki zao Wamerekani walihakikisha wanammaliza mkombozi huyu. Leo ndio siku ambayo Lumumba aliuwawa. Siku ambayo ni ya majonzi makubwa kwa Afrika nzima. Lumumba alipewa adhabu ya juu kabisa binaadamu kupewa kwa kosa moja tu – kutaka uhuru wa kweli kwa Waafrika wa Kongo.

Lumumba alijipa hukumu ya kifo siku ya kwanza kabisa ya Uhuru wa Kongo. Katika sherehe za Uhuru tarehe 30 Juni 1960, Mfalme wa Ubeligiji Baudouin alitoa hotuba katika Jumba la Taifa (Palais de le Nation – Kinshasa) ambayo ilimsifia sana babu yake Mfalme Leopold II kwa kuijenga Kongo. Alisema ‘ Uhuru wa Kongo ni mwendelezo wa kazi iliyotukuka iliyopangwa na mtu mwenye akili sana Mfalme Leopold kwa ujasiri wa hali yajuu na uvumilivu mkubwa wa Taifa la Ubeligiji.
Msiharibu maisha yenu ya baadaye kwa kufanya mageuzi ya haraka haraka na msiondoe muundo ambao Ubeligiji umewajengea mpaka hapo mtakapoweza kufanya vema zaidi’. Wakati Mfalme huyu anatoa maneno haya ya kifedhuli kwa wananchi wa Kongo, Lumumba ambaye hakuwa kwenye orodha ya wazungumzaji siku hiyo alikuwa anaandika hotuba yake kwa mkono na kwa haraka haraka. Hakutaka ufedhuli ule wa Mfalme wa Ubeligiji upite bila kujibiwa. Akajibu kwenye Hotuba ambayo haikuwa kwenye ratiba kabisa.

“Tumezoea dhihaka na matusi, tumepigwa asubuhi mchana na usiku, kwa sababu sisi ni watu weusi. Tumeona ardhi yetu ikinajisiwa. Tumeona sheria zikitambua wenye nguvu na sheria tofauti kati ya watu weusi na watu weupe.
Hatutasahau mamlaka zikijaza watu kwenye jela, watu ambao hawakukubali kwamba haki ni ukandamizaji na unyonyaji” Maneno haya yalifurahiwa sana na wananchi wa Kongo lakini yalikuwa ndio hukumu ya kifo ya Lumumba maana baada ya hotuba hii Wabeligiji waliamua kuwa ni lazima auwawe. Kweli siku kama ya leo mwaka 1961 Lumumba aliuwawa. Hakuna kaburi lake wala nguzo zake za mwisho. Alichomwa yeye na wenzake wawili. Mauaji yaliyoratibiwa kwakaribu sana na Serikali ya Marekani chini ya Shirika lake la Ujasusi.

Patrice Emery Lumumba aliuwawa wakati Kongo ipo chini ya majeshi ya Umoja wa Mataifa. Askari wa kulinda amani wa Ghana walipoona Lumumba amekamatwa na askari wa Mobutu walitaka kumwokoa na kumweka chini ya ulinzi wa Umoja wa Mataifa lakini wakuu wa Umoja wa Mataifa wakasema hiyo sio kazi yao, sio ‘mandate’ yao.

Wakuu wa Umoja wa Mataifa walisahau kabisa kwamba Lumumba alikuwa ni Mbunge na hivyo alikuwa na Kinga na hadhi ya Kulindwa kwa mujibu wa sheria. Lakini kwa kuwa umoja wa Mataifa wenyewe walikuwa wanafanya kazi ya Ubeligiji na Marekani, waliacha Lumumba, adui yao mkubwa, auwawe. Hivi sasa Bunge la Ubeligiji limeruhusu uchunguzi maalumu kuhusu Kifo cha Lumumba, miaka kadhaa baada ya Serikali ya Ubeligiji kuomba radhi kwa kuhusika na kifo hicho.
Serikali ya Marekani, pamoja na nyaraka kuonyesha kuhusika kwake na mauaji ya mwanamapinduzi huyu, bado haijaomba radhi. Pamoja na Rais Barack Obama kuwa na asili ya bara la Afrika, hatutaraji kama ataomba radhi kwa mauaji haya ya kinyama dhidi ya Mzalendo namba moja barani Afrika.

Wakati Waafrika tunamkumbuka hayati Lumumba katika siku yake hii, masuala tunayopaswa kuyatafakari ni kama tunasimamia yale ambayo Mwanapanduzi huyu aliyasimamia. Lumumba alitaka uhuru kamili wa bara la Afrika, sio uhuru wa bandia. Alitaka utajiri wa Afrika utumike kwa ajili ya kuendeleza waafrika. Leo tunaona Afrika inaendelea kunyonywa na mataifa makubwa.

Uchumi wa Afrika umemezwa kabisa kabisa na nchi nyingine. Utajiri wa Afrika unaendeleza mataifa yale yale ya magharibi. Kama alivyosema afisa mmoja wa jeshi la Ubeligiji mara baada ya uhuru wa Kongo ‘Kabla ya Uhuru sawasawana Baada ya Uhuru’.Afrika yenye utu na heshima yake bado. Nchi yenyewe ya Kongo bado imegubikwa mauaji. Mamilioni ya wananchi wa Kongo wameuwawa toka mwaka 1996.

Mataifa jirani ya Kongo yanashiriki kabisa katika kuleta machafuko nchini humo. Umoja wa Mataifa bado upo Kongo na wala hawawezi kuzuia uvamizi. Waafrika wenyewe kwa wenyewe tunatumika dhidi yetu. Lumumba alishirikiana na wenzake kama Nyerere, Nkrumah, Kenyatta nk katika kupigania uhuru. Viongozi wa sasa wa Afrika wanashirikiana na mabeberu kuinyonya Afrika.

Nitamalizia kumbukumbu yangu ya hayati Lumumba kwa hadithi niliyohadithiwa na marehemu Kanyama Chiume, Waziri wa kwanza wa Mambo ya Nje wa Malawi. Mmoja wa wanamapinduzi ambaye alibahatika kuonana na kufanya kazi na Lumumba. Nilimwuliza, nikiwa mwaka wa kwanza Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alimjuaje Lumbumba? Akanijibu ‘walimvumbua wapi Lumumba?’ Yeye na wenzake. Ni hadithi ya kukumbukwa na vizazi na vizazi.

Ujumbe wa Chama cha kupigania Uhuru Afrika Mashariki Kati na Kusini (PAFMECSA) ulikuwa umetua jijini Kinshasa wakielekea Accra kwenye Mkutano wa nchi za Africa ulioitishwa na Rais Kwame Nkrumah wa Ghana mwaka 1958 (All Africa Conference).

Ujumbe huu ulimjumuisha Julius Nyerere wa Tanzania, Abdurahman Babu wa Zanzibar, Tom Mboya wa Kenya na Kanyama Chiume wa NyasaLand. Wakiwa jijini humo, Kanyama Chiume na Babu wakawa wanatembea tembea mjini kusubiri ndege ya kuwabeba kuwapeleka Accra, walikuwa pale kwa siku 5 hivi. Katika kuuliza uliza kuhusu harakati za ukombozi katika Kongo, ndio wakaambiwa kuna kijana anapigapiga kelele mjini pale anaitwa Lumumba, wakaomba kumwona. Wakashangaa namna ambavyo habari za kupigania Uhuru Kongo hazijulikani kabisa nje ya Kongo.

Walivutiwa sana na Lumumba. Wakamkatia tiketi ya ndege (Tom Mboya ndio alitumia fedha za wapigania uhuru wa Kenya kununua tiketi ya Lumumba). Wakaenda naye Accra. Afrika ikamjua Lumumba. Mapambano ya Kongo ya Kongo yakapata nguvu kubwa na hatimaye Uhuru ukapatikana.

Katika kikao cha Mwalimu Nyerere wa Tanganyika na Rais Ahmed Sekou Toure wa Guinea, Lumumba ndiye alikuwa mfasiri maana yeye alijua Kiswahili na Kifaransa, Mwalimu alijua Kiingereza na Kiswahili na Sekou Toure alijua Kifaransa tu. Namna ambavyo wapigania uhuru walivyokuwa wanashirikiana inasisimua mwili. Kizazi hiki cha viongozi wa Uhuru kimekwisha. Viongozi wa sasa wamejaa tamaa ya mali na sifa za kusifiwa na Mataifa ya magharibi.

Lumumba mpaka anakufa alikuwa jasiri. Wazungu waligopa hata maiti yake ndio maana walimwunguza kwa tindikali. Hata barua yake ya mwisho kwa mke wake ilionyesha ni mtu wa namna gani. Badala ya kuanza kusema ameacha akiba yake wapi yeye alisema ‘historia ya kweli ya Afrika itaandikwa na Waafrika wenyewe’. Mwanaume wa shoka. Tutakukumbuka daima. Hata kama waliokufuata wameshindwa kuandika historia ya kweli ya mapambano ya Afrika, maneno yako yatabaki daima kama kishawishi kwa Waafrika. Afrika itakombolewa tu. Pumzika kwa amani Patrice Emery Lumumba, Mwafrika kindakindaki.