WAZIRI Mkuu mstaafu na Mbunge wa Monduli Edward Lowassa(CCM) amevunja ukimya kwa mara ya kwanza Bungeni kwa kuamua kutema cheche kwa kuitaka Serikali kuchukua maamuzi mazito katika mambo mbalimbali nchi iweze kusonga mbele na anaamini hilo linawezekana.
Amesema ni bora viongozi waliopo Serikali wakawa wanafanya maamuzi kuliko kutofanya maamuzi ni makosa makubwa ni bora ukaalaumi kwa maamuzi uliyofanya kuliko kulaumiwa kwa kutofanya maamuzi.
Lowassa ambaye ajiuzulu nafasi ya Uwaziri Mkuu baada ya kuamua kukaa pembeni kutokana na taarifa ya Kamati ya Bunge iliyokuwa imepewa jukumu la kuchunguza kashfa ya kampuni ya kufua umeme wa dharura wa megawati 100 kumuingiza katika sakata hilo .
Tangu Lowassa alipojiuzulu nafasi hiyo amekuwa kimya muda mrefu lakini kwa jana amaemaumua kuvunja ukimya na hatimaye kutoa ufafanuzi wa mambo mbalimbali na nini Serikali ifanye ili nchi iweze kusonga mbele huku akitumia muda mwingi kuelezea mafanikio ambayo yamepatikana.
Akizungumza wakati akichangia bajeti ya fedha ya mwaka 2011/2012 kwa ajili ya Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo iliwasilishwa juzi na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Lowassa alisema hakuna sababu ya viongozi kutofanya maamuzi bali ni wakati muafaka wa kuchukua maamuzi ili kuweza kufanikisha mambo kusonga mbele.
“Viongozi waliopita katika nchini hii kuanzia awamu ya kwanza ya Mwalimu Julius Nyerere, mzee Mwinyi, Mkapa na sasa Rais Jakaya kikwete wameweza kufanya mambo mengi kila kiongozi kwa nafasi yake.Ni wajibu wetu kusifu maendeleo ambayo yamepatikana.
“Sasa nchi yetu imefikisha miaka 50 tangu kupata uhuru wetu, kuna mambo mengi yamefanyika katika nchi hii, wapo ambao wanataka kubeza maendeleo yaliyopatikana. Tunapozungumzia mafanikio tuliyonayo yote yametokana na Chama Cha Mapinduzi (CCM). Tunakila sababu ya kupongeza, Watanzania wanajua ulimwengu unajua,” alisema Lowassa.
Alisema kuwa yamefanyika mambo mengi katik nchi na hakuna sababu ya kubezwa kama ambavyo baadhi ya watu wanafanya na kutumia nafasi hiyo kufafanua kuwa historia ya nchi hii inaonesha tulikota na tulipo sasa na kupongeza vyombo vya habari ambavyo vinaonesha na kutangaza historia ya nchi tangu kupatikana kwa uhuru.
“Serikali imeweza kujenga Chuo Kikuu cha Dodoma(UDOM) kwa fedha zetu zaidi ya sh. trilioni moja, Watanzania wanajua na ulimwengu unajua. tumejenga shule za sekindari za kata Watanzania tunajua na ulimwengu unajua, tumefanikisha mradi wa maji safi ya Ziwa Victoria Watanzania wanajua na ulimwengu unajua.
“Tutoe maamuzi tuache woga.Unaweza kusema fedha za kujenga nchi yetu zitatoka wapi, hapanma fedha zipo tukiamua tunaweza, nasema tunaweza na ndio maana hata maendeleo ambayo yanaonekana tuliamua tukaweza kuyafanya. Tunaweza kukopa fedha kwa kutumia gesi tuliyonayo nchini.
“Wanaofuatilia siasa, wanakumbuka wiki iliyopita tu nchi ya Marekani imekuwa ikijadili uwezekano wa kuongeza deni lake la Taifa kwa kukopa fedha kutoka mataifa mengi kwanini sisi tunaogopa kukopa. Tanzania kwanini tusikope,” alisema Lowassa.
Akizungumza zaidi wakati anachangia bajeti ya Waziri Mkuu, Lowassa alisema umefika wakati wa kuamua kujenga reli mpya kutoka Dar es Salaam hadi Kigoma, ni wakati muafaka wa kujenga upya bandari ya Tanga lakini pia ni wajibu wa kujenga sasa bandari ya Tanga.
Aliongeza kuna ulazima wa kufanya mambo ya maendeleo kwa ajili ya Watanzania na hilo linawezekana kikubwa ni kuthubutu na kuamua kufanya kile ambacho kitakuwa na tija kwa wananchi.
“Haya yote tutafanya kwa kuamua sasa. Tukiamua tunaweza, uchumi wetu umekuwa kwa asilimia saba kasi ambayo ni kubwa ya ukuaji wa uchumi Watanzania wanajua na ulimwengu wanajua. Lakini pamoja na kukua huko kwa uchumi ni wakati sasa wa kuhakikisha unawafikia wananchi katika matumbo yao.
“CCM tumefanya mambo makubwa, hatuna sababu ya kuogopa kuelezea mafanikio ambayo yamepatikana. Mambo yaliyofanyika yametupa heshima kubwa Watanzania wanajua ulimwengu unajua. Tuliamua kujenga reli ya Tazara kwa kushirikiana na Zambia, tuliweza,” alisema.