Lowassa Ataka Mfumo wa Elimu Tanzania Ufumuliwe

WAZIRI Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa

WAZIRI Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa amesema kuna haja ya kutathmini upya mfumo wa elimu nchini, ili kuona kama bado unafaa au la.Alisema hatua hiyo inapaswa kufanywa sasa kabla mambo hayajaharibika zaidi na kwamba anaamini kuwa tangu mfumo uliopowekwe enzi za Mwalimu Nyerere, kuna mabadiliko mengi yamejitokeza.

Lowassa alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) ofisini kwake jijini Dar es salaam.

“Mimi nasema kuwa sasa wakati umefika kama taifa. kuunda tume ya elimu, ili kuangalia na kupitia mfumo wote wa elimu, kuangalia mitalaa yetu kuanzia elimu ya awali mpaka vyuo vikuu, kuangalia ubora wa elimu hiyo, vitabu gani vitumike, maslahi ya walimu, yaani kwa ujumla tuangalie upya kuhusu mfumo wa elimu yetu.” alisisitiza Lowassa.

Lowassa alipendekeza kuundwa kwa tume ya elimu kwa ajili ya kufanya kazi hiyo, ili kwenda na wakati. “Tume hiyo iundwe kuchunguza, kutathmini na kuona, endapo mfumo wa elimu wa sasa unaendana na wakati,”

Lowassa alisema nchi zote zilizoendelea duniani, zimekuwa zikifanya hivyo.
“Marekani hivi sasa kuna mchakato wa kuangalia elimu inayotolewa kama inaendana na changamoto za karne ya 21,” alisema.

Kumekuwa na malalamiko mengi miongoni mwa wadau wa sekta ya elimu kwamba mitalaa ya elimu nchini, haimwandai mwanafunzi kukabiliana na changamoto za maisha ya karne hii ikiwa ni pamoja na kujiajiri.

Lowassa ambaye pia ni Mbunge wa Monduli, amesema Serikali ya CCM imefanya mambo makubwa sana katika sekta ya elimu, hususan awamu hii ya nne ambayo kwa mafanikio makubwa, imeweza kujenga shule za sekondari katika kata zote nchini.
Katika mkutano wake mkuu wa nane hivi karibuni mjini Dodoma, CCM ilitoa mapendekezo kadhaa miongoni mwao likiwa la kuboresha elimu nchini.

“Mimi nilipata bahati ya kuongoza juhudi hizo za Serikali kwa mafanikio makubwa kujenga shule hizo, lakini mafanikio hayo yamekuja na changamoto zake,” alisema.

Alisema changamoto kubwa zilizojitokeza katika mafanikio hayo ni ubora wa elimu inayotolewa na shule hizo, uhaba wa walimu na vitendea kazi vikiwemo vitabu na masilahi kwa walimu. Alisema Tanzania ina bahati ya kuwa na wasomi waliobobea ambao wanaweza kazi hii ya kuangalia mitalaa inayotumika ili kuona kama inakidhi haja na matakwa ya karne ya sasa.

CHANZO:- http://www.mwananchi.co.tz