Lowassa Asema Nina Ari, Shauku na Uwezo wa Kuongoza Tanzania…!

Mtangaza nia ya kuwania Urais wa Tanzania kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Monduli, Mh. Edward Lowassa (kulia).

Mtangaza nia ya kuwania Urais wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Monduli, Edward Lowassa akiaga wananchi.

Mtangaza nia ya kuwania Urais wa Tanzania kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Monduli, Edward Lowassa (kulia).

Mtangaza nia ya kuwania Urais wa Tanzania kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Monduli, Edward Lowassa akiwapungia mkono wananchi kwenye mkutano wake.

WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Ngoyai Lowassa amesema ana ari, shauku na uwezo wa kuongoza Taifa wakati alipotangaza nia yake ya kugombea urais kwa tiketi ya CCM katika mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na maelfu ya watu kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid. Lowassa, ambaye ni mbunge wa Monduli akihutubia maelfu ya wakazi wa Arusha, katika Uwanja a Sheikh Amri Abeid Aluta, alisema ameamua kujitokeza tena kuwania urasi kwa kuwa anaamini yeye ndiye mtu sahihi wa kuiongoza nchi wakati huu.

Zaidi ya watu 30,000 walifurika kwenye uwanja huo wakiwa wamekaa kwenye viti na wengine ndani ya kiwanja cha mpira huku, mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombare Mwiru akiongoza mlolongo wa watu mashuhuri waliojitokeza kumuunga mkono mbunge huyo wa Monduli katika mbio za kuelekea Ikulu anazoziita “safari ya Matumaini”.

Kwa kawaida uwanja huo una uwezo wa kuchukua watu 25,000. Umati huo ulipiga kelele kulazimisha Lowassa ahutubie mapema na kulazimisha waratibu wasitishe matukio mengine yaliyopangwa kufanyika kabla ya mtangazania huyo. Akihutubia mkutano huo, Lowassa alisema pamoja na kuwa viongozi waliopita wameliongoza taifa hili vizuri, bado linahitaji kiongozi mwenye uthubutu na uongozi madhubuti unaoweza kufanya maamuzi magumu.

“Kuamini kama una uwezo na shauku, hakuna budi kwenda sambamba na uwezo wa kusimamia yale unayoyaamini. Na kwangu haya mawili ni dhahiri. Nina ari, nina shauku na nina uwezo, kama rekodi yangu inavyothibitisha,” alisema Lowassa huku akishangiliwa.

“Tunapomtafuta Rais wa Jamhuri ya Muungano ni lazima tukumbuke kwamba tunamtafuta mtu ambaye atakuwa pia ni Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama katika nchi yetu. Na kwa Chama cha Mapinduzi tunamtafuta mtu ambaye atakuwa pia mwenyekiti wa chama chetu.

“Naamini kwa vigezo vyote, nina kila sifa ya kubeba dhamana hizo nzito. Katika mambo ambayo najivunia, na sitayasahau katika historia yangu ni kushiriki kwangu kuilinda nchi yetu pale nilipohitajika. Nilishiriki kikamilifu katika Vita vya Kagera nikiwa miongoni mwa askari wa mstari wa mbele wa mapambano.”

Lowassa pia alikumbusha tukio la mwaka 1995 alipojitokeza kugombea urais kwa pamoja na Rais Jakaya Kikwete.

“Wakati ule sote tulikuwa wanasiasa vijana. Pamoja tulikwenda kuchukua fomu na baadaye kwa pamoja tukazungumza na waandishi wa habari. Tulileta hamasa kubwa pale tulipofanya jambo ambalo halikuzoeleka kwa Watanzania kwa kutangaza kwamba yeyote atakayepita kati yetu, mwenzake ambaye hatafanikiwa angemuunga mkono,” alisema na kuongeza:

“Natarajia safari hii, Kikwete ataniunga mkono.”

Hata hivyo, Kikwete hakupitishwa na CCM mwaka huo na akagombea peke yake 2005, mwaka ambao Lowassa alisema aliamua kwa dhati kumuunga mkono mwenzake.

Ataja sifa za kiongozi anayehitajika
Katika hotuba yake, Lowassa alitaja sifa za kiongozi ambaye anaamini anafaa kuiongoza Tanzania, akisema Taifa linahitaji uongozi wenye uthubutu, uongozi thabiti, makini na usioyumba na wenye ubunifu na upeo mkubwa. Baada ya kusema maneno hayo, umati ulishangilia na kumtaka arudie tena sifa hizo na akatulia kwa muda kabla ya kuzitaja tena na kusababisha watu walipuke tena kushangilia.

“Naamini wananchi wanamtaka Rais ajaye wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aweze kuwaunganisha Watanzania, abuni sera na kusimamia utekelezaji wa mikakati ya kuinua uchumi, abuni sera na kusimamia utekelezaji wa mikakati ya kuzalisha ajira kwa vijana na awe mfano wa kuchapa kazi na kuwajibika,” alisema mbunge huyo wa Monduli.

Kadhalika Lowassa alisema kiongozi anayefaa kuiongoza nchi hana budi kuwa na uwezo wa kutumia kibiashara fursa za kijiografia, asimamie matumizi ya rasilimali ili kutokomeza umaskini na pia atokomeze mianya ya rushwa kwa vitendo.

Lowassa, ambaye alijiuzulu uwaziri mkuu baada ya kutokea kashfa ya Serikali kuingia mkataba wa uzalishaji umeme wa dharura na kampuni iliyosadikiwa kuwa haikuwa na uwezo ya Richmond RDC ya Marekani, alisema juhudi kubwa zimefanyika ili kumchafua lakini hajakata tama.

Dira na matarajio yake
Lowassa pia alitaja dira na matarajio yake iwapo atapewa nafasi ya kuiongoza nchi, akisema ataimarisha Muungano kwa kuangalia kasoro zilizopo na kuyalinda yale yanayotuunganisha. Alisema atashughulikia matumizi mabaya ya siasa za udini, ukabila na ubaguzi wa aina yoyote ili kuimarisha siasa zilizoshiba uzalendo na kutuelekeza kwenye utanzania wetu.

Alisema kwa msisitizo kuhusu nia yake ya kuliondolea taifa sifa mbaya ya kuombaomba. “Kwa wingi wa rasilimali tulizo nazo na neema ya ardhi, maziwa, mito na bahari, Tanzania tuna kila sababu ya kuacha kuwa ‘bakuli la ombaomba’ na badala yake kuwa ‘mkoba wa neema’ katika Afrika,” alisema huku akirudia suala la nchi kuwa ombaomba kila mara kwenye hotuba yake. Alisema katika uongozi wake anatarajia kuweka kipaumbele kwenye elimu na kusema kuwa elimu ndiyo mhimili wa maendeleo kwa nchi maskini kama Tanzania.

“Kama Waingereza wameweka msisitizo katika elimu, sembuse sisi. Mambo haya ndiyo yatakuwa msingi mkubwa nikipewa ridhaa ya kuongoza nchi na CCM,” alisema

Pamoja na kuitaja dira na matarajio yake pindi atakapopewa uongozi, hotuba ya Lowassa iligusa ramani ya uongozi anayoiamini na kusema atakuwa mwanzo wa mchakamchaka wa maendeleo katika misingi ya utawala bora na utendaji utakaojengwa katika nguzo za katiba.

“Maendeleo yatakuja pale tu tutakaporejea kwenye katiba katika kuainisha nia, dhamira na malengo yetu ya kujenga jamii inayozingatia misingi ya demokrasia, udugu na amani,” alisema.

Pamoja na mambo mengine Lowassa alisema uongozi wake unataka kujenga uzalendo, uadilifu pamoja na kuimarisha uwazi na kupambana na rushwa. Pia alirejea kauli yake kuhusu tatizo la ajira akisema likiachwa linaweza kuiingiza nchi kwenye matatizo.

“Vijana wanataka kuona ukuaji wa uchumi na ugunduzi wa utajiri huo unakwenda sambamba na uzalishaji wa ajira zenye maana ili waweze kukabiliana na changamoto za maisha yao,” alisema.

“Niliwahi kusema kwamba tatizo la ukosefu wa ajira likiachwa bila ya kutafutiwa ufumbuzi ni bomu linalosubiri kulipuka. Vijana wasio na ajira hupoteza matumaini na ni rahisi kughilibiwa ili kuingiza nchi katika machafuko. Tunahitaji uongozi imara kuweza kuikabili hali hiyo na kuitafutia suluhisho maridhawa.”

Mengine aliyotaja Lowassa ni kujenga Serikali madhubuti, makini na yenye nidhamu inayoendeshwa kwa misingi ya sheria, uwazi na uwajibikaji. Akihitimisha hotuba yake, Lowassa alisema siku si nyingi nchi hii itaanza safari yenye mwelekeo wa matumaini lakini kwa ushirikiano kutoka kwa wananchi.

“Naomba nihitimishe kwa kuwaomba wana CCM ikiwa ni pamoja na wagombea wenzangu, waniunge mkono na tujumuike kwa pamoja katika safari hii ya matumaini. Safari tuianze leo, hatuna kesho nyingine,” alisema.

Kabla ya kuanza mkutano huo, viongozi wawili wa dini ambao ni Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri, Dayosisi ya Kaskazini, Dk Martin Shao na Sheikh Haruna Nkumilwa, walifanya sala ya kumuombea Lowassa afanikiwe katika safari hiyo ya matumaini.

Miongoni mwa viongozi waliopewa nafasi ya kuzungumza kuonyesha kumuunga mkono Lowassa katika safari yake ni pamoja na mwenyekiti wa CCM wa Arusha, Onesmo Ole Nangolo, mbunge wa Mwibara, Kangi Ligola na mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Geita, Joseph Kisheku maarufu kwa jina la Msukuma ambaye aliingia uwanjani hapo kwa helikopta wakati shughuli ikiwa imeshaanza.

Hadi kufikia majira ya saa 4:00 asubuhi uwanja huo ulikuwa umeshafurika watu kutoka mikoa mbalimbali nchini huku ukiwaacha wenyeji wa Arusha wakipigania kuingia uwanjani baadaye jioni.
Mabasi 30 aina ya Toyota Coaster na magari madogo ambayo idadi yake haijulikani, yalisafirisha watu kutoka mjini Moshi hadi Uwanja wa Sheikh Amri Abeid kushuhudia tukio hilo.

Kuanzia saa 1:30 na saa 3:00 asubuhi, gazeti hili lilishuhudia mabasi hayo yakiondoka eneo la Posta, Club ya Huggos na wanafunzi wa vyuo vikuu mbalimbali wakiondoka na mabasi hayo yaliyokodiwa kwa michango mbalimbali ya Marafiki wa Lowassa.

Mabasi mengine yalikwenda moja kwa moja Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Mwenge, Chuo Kikuu cha kumbukumbu ya Stefano Moshi, Chuo Kikuu cha Ushirika na chuo cha Veta kubeba wanafunzi marafiki wa Lowassa. Kwenye baa na hoteli zenye runinga kubwa kulifurika watazamaji huku wananchi wengi wakibaki majumbani kufuatilia tukio hilo kwenye runinga zao.
CHANZO:- http://www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/Lowassa–Nina-ari–shauku-na-uwezo/-/1597296/2735076/-/item/3/-/y99thfz/-/index.html