- *Wastani wa watu 15 wafia kwenye foleni kila siku
*Ugonjwa wa kuhara damu waibuka kwa kasi kubwa
*Ofisa Kilimo Wilaya ya Misungwi afia kwenye foleni
*Zahanati haina dawa, wahudumu, glovu, vitanda
*Wanajeshi kutoka Kenya wafika kijijini Samunge
kwamba wastani wa watu 15 wanafia kwenye foleni na wengine miili yao kuharibikia ndani ya magari.
Maelfu kwa maelfu ya watu wamekwama kwenye foleni ambayo hadi jana ilifikia kilometa 35 kutoka nyumbani kwa Mchungaji (mstaafu), Ambilikile Masapile, katika Kijiji cha Samunge.
Hali ikiwa inazidi kuwa mbaya, Serikali Kuu, hasa ngazi ya kitaifa ni kama imelala usingizi wa pono, ikionekana kutojali kabisa janga hili.
Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Elias Wawalali ndiye anayeonekana kuhangaika zaidi na janga hili, ilhali suala hili sasa likiwa limewazidi uwezo wilaya na mkoa.
Kwa hali ilivyo sasa, MTANZANIA inawashauri wananchi wafute safari za kuja huku hadi hapo Serikali itakapokuwa imejiridhisha juu ya usalama wa watu wanaofika huku.
Zahanati haina dawa
Wakati magonjwa ya mlipuko yakiwa yameanza kwa kasi, imebainika kuwa Zahanati ya Samunge haina dawa, vifaa wala madaktari na wauguzi wa kutosha. Hadi jana walikuwapo wahudumu watatu pekee.
Imebainika kuwa hakuna insulin, ambayo ni kwa ajili ya wagonjwa wa kisukari wala dawa aina ya aminophilline ambayo ni muhimu mno katika kukabiliana na pumu.
Magonjwa ya milipuko
Hali ya magonjwa ya mlipuko inaweza kuwa mbaya zaidi kutokana na mvua kubwa zilizoanza kunyesha.
Pia kwenye foleni yote hakuna maji safi na salama, na pale yanapopatikana, chupa moja yenye ujazo wa lita 1.5 inauzwa kwa Sh 3,000. Soda yenye ujanzo wa mililita 350 juzi ilikuwa ikiuzwa kwa Sh 2,000. Biskuti ambayo kawa kawaida huuzwa Sh 150 au Sh 200, sasa inauzwa kwa Sh 1,000.
Hali hiyo imewafanya watu wengi watumie maji machafu ya mito na yaliyotuama porini. Maji hayo, licha ya uchafu wa kawaida, yamechanganyika na vinyesi, mkojo na uchafu mwingine wa kibinadamu.
Gari moja aina ya Fuso lenye namba T124 AFJ lililokuwa na shehena lilivamiwa na wananchi waliotaka wauziwe bidhaa zilizokuwamo. Hali ilikuwa ya vurugu kubwa kutokana na watu kupigana vikumbo kupata mahitaji.
Licha ya Mchungaji Masapile kusema yeye si hospitali ya rufaa, bado kuna wagonjwa wengi walio mahututi ambao wanapelekwa kwake, ambao wamekuwa wakikata roho hata kabla ya kupata matibabu.
Maelfu ya watoto wanaendelea kutaabika wakiwa wanalia kutokana na kukosa mahitaji muhimu, hasa vyakula na maji.
Gari linalohudumia wagonjwa mahututi ni moja na halifiki sehemu yote ya foleni kutokana na magari kufunga barabara. Njia pekee ya kuwafikia walengwa ni mbili, ama kupanua barabara ya pembeni (service road) itakayotumiwa na magari ya wagonjwa, au kutumia helikopta.
Mtu aliyetajwa kuwa Afisa Kilimo wa Wilaya ya Misungwi, imeelezwa kuwa amefia kwenye foleni baada ya kupata ugonjwa wa kuhara.
Wanajeshi kutoka Kenya
Timu ya Mtanzania imeshuhudia wanajeshi wa Kenya wakiwa wamevalia magwanda wakifika Sumange kupata dawa.
Awali, wanajeshi hao waligundulika wakila hotelini katika eneo la Wasso-kilometa 50 kabla ya kufika Samunge. Baadaye walitoka kwa kasi na juhudi za kuwapata zilikwama.
Walipofika kwenye foleni walitelekeza gari na kutembea kwa mguu. Walitumia gari lenye namba za usajili za Kenya, KAN 961 C. Hata hivyo, kwenye vioo vyote vya gari hilo kulikuwa na namba za usajili za SU 31953. Kwa kawaida namba hizo ni za usajili wa magari ya mashirika ya umma hapa nchini.
Usalama wa nchi
Hali ya usalama katika ukanda huu wa Kaskazini sasa ni wazi kuwa iko shakani kwani hakuna upekuzi wowote kwa wageni na wenyeji.
Mbali na wanajeshi wa Kenya, juzi, kwa mara ya kwanza walionekana pia wanajeshi wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) waliovalia sare za Jeshi wakiwa kwenye foleni kuelekea Samunge.
Foleni sasa inatisha
Hali ya foleni imezidi kutisha kutokana na urefu wake. Magari yanayotoka mikoa ya Kanda ya Ziwa yanakutana na mengine yanayotoka mikoa ya Singida, Arusha, Manyara na Kilimanjaro katika eneo la Vibaoni ambako ni kilometa 15 kabla ya kufika Samunge kwa Mchungaji.
Kilichopo sasa ni kama mito midogo midogo inayoingia kwenye mto mkubwa. Kimsingi, kama foleni ingekuwa moja (bila matawi) urefu wake ungekuwa kilometa zaidi ya 50.
Habari hii imeandikwa na Manyerere Jackton, Masyaga Matinyi na Eliya Mbonea, waliopiga kambi Samunge.
chanzo:gazeti la Mtanzania