Loliondo ni kivumbi

  • *Wabunge washindana kupeleka wapigakura kwa mabasi
  • *Mratibu Ukimwi Mkoa asalimisha wafanyakazi kwa Babu
  • *Sheikh ataka Waislam wakapate kikombe kwa Mchungaji
  • *KKKT wafungua akaunti kwa ya kuboresha miundombinu

SIKU chache baada ya mbunge wa Monduli (CCM), Edward Lowassa na wa Moshi Mjini (CHADEMA), Philemon Ndesamburo kusafirisha wapigakura wao kwenda Loliondo kupewa kikombe, sasa wabunge wanashindana kupeleka wapigakura wao.

Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema naye amejitolea kusafirisha wagonjwa 100 katika jimbo lake, kuwapeleka kwa Mchungaji Ambilikile Mwasapile aliyerejeshwa kazini hata baada ya kustaafu kutokana na huduma anayoitoa.

Mbunge huyo ametenga Sh milioni 50 kusafirisha wapiga kura wa jimbo lake kwa awamu tofauti akianza na wagonjwa wasio na uwezo wa kufika huko.

Aizungumza na waaandishi wa habari ofisini kwake jana, Lema alisema ameamua kukatisha semina ya wabunge inayoendelea Dare salaam awahudumie wapiga kura wake waliokosa fedha za kuwafikisha Samunge kwa Babu wakanywe kikombe cha dawa itakayowaponyesha maradhi sugu yanayowasumbua kwa muda mrefu.

“Nimejitolea kuwasafirisha wagonjwa 100 wasiojiweza hasa kwa wale wajane na yatima waliokosa mtu wa kuwapatia japo nauli ya kufika huko… lakini mimi kama mbunge wao nitawapeleka na kuwarudisha wapiga kura wangu,” alisema Lema.

Aliwatahadharisha wananchi waliojitokeza kuwa ofisi ya mbunge itafanya utafiti wa kina kubaini familia zisizokuwa na uwezo ndizo zitakazopewa kipaumbele na kwamba kadi ya kujiandikishia kupiga kura itakuwa kielelezo cha kwanza kuwabaini.

“Kama mnavyofahamu kazi ya kujitolea ni ngumu sana, vivyo hivyo inahitaji umakini wa hali ya juu kuwatambua wale wenye mahitaji ambao tunataka kuwasaidia… lakini kuna uwezekano mkubwa kwa watu kutumia fursa hii vibaya kwa maana ya kujaribu kuzamia na hata kuligeuza jambo lenyewe kuwa la kisiasa, tuko makini sana,” alisema.

Alisema ofisi ya mbunge tayari inashughulikia taratibu za kupata basi maalumu litakalofika huko Samunge bila kukwama kutokana ubovu wa barabara, ili wananchi hao wanaotarajiwa kuondoka leo wasafri na kurudi kuungana na familia zao salama.

“Nimepata taarifa kuwa barabara sio nzuri, tumefanya jitihada za kukodisha basi maalumu ambalo tuna hakika litawafikisha wagonjwa tunaowasafirisha,” alisema.

Akizungumza na Mtanzania mmoja wa wagonjwa aliyekuwa katika msururu wa kujiandikisha nje ya jengo la Mkuu wa Wilaya ziliko ofisi za mbunge, alimpongeza mbunge huyo kwa kuwajali wapiga kura wake hasa katika kipindi hiki ambapo wafanyabiashara wanatumia matatizo ya watu wengine kujinufaisha.

“Hapa wengine wanaweza kusema hii ni siasa, lakini sio kweli mbunge wetu ameona matatizo yetu na sasa anachukua hatua ya kutusaidia,” alisema mgonjwa huyo.

Tangu huduma ya Mchungaji Mwasapile kuanza kushuhudia wagonjwa mbalimbali kupona na kujitokeza kushuhudia jinsi walivyopona, watu wa kada mbalimbali wamejitokeza kuwapeleka wagonjwa waliougua kwa muda mrefu katika kijiji hicho kilicho umbali wa kilometa 400 kaskazini mashariki mwa Tanzania.

Waziri Mkuu kupata kikombe

Habari zilizolifikia gazeti hili muda nfupi kabla ya kwenda mitamboni, zilisema mmoja wa mawaziri wakuu wastaafu leo atakuwa njiani kwenda Loliondo kwa Babu kupatiwa kikombe.

Mratibu wa Ukimwi

MRATIBU wa Ukimwi Mkoa wa Arusha, Samwel Kaaya, naye amebisha hodi kwa Mchungaji mstaafu Ambilikile Mwasapile, na kunywa dawa inayosadikika kutibu maradhi matano hatari, ukiwamo ukimwi.

Kaaya alizungumza na MTANZANIA juzi na kusema alikuwa amefika katika Kijiji cha Samunge, kwa ajili ya kufuatilia taarifa za waathirika wa ukimwi.

“Nimefika hapa na watumishi wenzangu kwa ajili ya kuangalia mazingira na kikundi, lakini sikuja kikazi,” alisema.

Mratibu huyo ni miongoni mwa mamia ya maelfu ya watu maarufu na wa kawaida wanaofika nyumbani kwa Mchungaji huyo mstaafu kwa ajili ya kunywa dawa hiyo.

Maelfu ya wananchi wameendelea kumiminika katika Kijiji cha Samunge. Wanatoka sehemu zote nchini pamoja na nchi jirani za Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).

Mchungaji Ambilikile alinukuliwa akisema kwamba watu wanaoendelea kumiminika kupata dawa hiyo ni tone tu, na kwamba ameoteshwa kuna wageni wengi kutoka mbali watakaofika kunywa dawa hiyo.

Kijiji cha Samunge na maeneo yote jirani yamekuwa na idadi kubwa ya watu, huku wajasiriamali wakijipatia fedha kutokana na biashara.

Ulinzi na usalama vimeimarishwa, na hakuna matukio mengi ya uvunjifu wa amani. Polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) wameongezwa pamoja na vitendea kazi.

Umeanzishwa utaratibu mpya wa watu kunywa dawa wakiwa ndani ya magari. Uamuzi huo umesaidia kupunguza msongamano mkubwa uliokuwapo awali.

Hata hivyo, suala la usafi bado ni tete kutokana na kutokuwapo vyoo vya kutosha. Hali hiyo imesababisha watu wengi wajisaidie vichakani, na ni huko huko ambako kumejaa wajasiriamali wanaouza vyakula na huduma nyingine.

Tayari uongozi wa Kijiji cha Samunge umeshapitisha utaratibu wa kutoza Sh 2,000 kwa kila gari linalofika kijijini hapo ili sehemu yake itumike kwa usafi.

Chupa tupu za maji, makasha ya biskuti na makopo ya sharbati (juice) yamezagaa kila mahali, na hivyo kuzidi kuchafua mazingira.

Baadhi ya watu wanafika Samunge kwa kutumia usafiri wa helikopta. Kuna kampuni imeanzisha mradi wa mahema na kukodisha kwa wapangaji.

Sheikh: Waislamu nenda kwa Mchungaji

SHEIKH Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mustafa Rajab Shaaban, ametaka Serikali kufanya utaratibu wa kuboresha huduma za utoaji wa dawa za Mchungaji wa Kanisa la KKKT, Ambilikile Mwasapile.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, alisema ni vizuri Serikali ikatambua mchango anaoutoa Mchungaji wa utoaji wa tiba na kumboreshea mazingira ikiwemo vifaa vya kutolea tiba hiyo.

“Ni muhimu kwa Serikali kutoa vifaa mbalimbali vya kumsaidia mchungaji huyo ili watu wengi zaidi waweze kupata huduma hiyo kwa urahisi,” alisema.

Licha ya Serikali kutakiwa kuboresha tiba hiyo, Sheikh Shaaban pia aliitaka kufanya haraka uchunguzi wa dawa anayoitoa Mchungaji Mwaisapile kujua ubora wake.

Alisema kwa kufanya hivyo italeta imani kwa wananchi ili wajitokeze kwa wingi kwenda kupatiwa matibabu hayo.

Alisema yeye binafsi hana pingamizi lolote kuhusu dawa hiyo kwa kuwa inatumia miti shamba ambayo ndio chanzo cha dawa zote duniani.

Pamoja na kuwa dawa hiyo ipo kiimani zaidi, alisema hakuna ubaya wowote kwa muumini wa dini ya Kiislamu kwenda kupata tiba hiyo kwa kuwa kwa kufanya hivyo si kwamba amekiuka maadili ya dini au imani yake.

“Ile ni tiba inayotumia miti shamba na haimbadilishi mtu imani yake, na kuwa Babu anapoitoa hamuombei mgonjwa bali anaiombea dawa,” alisema.

Alisema dini ya Kiislamu inaruhusu ushirikiano na imani zingine ili kuweza kutatua matatizo mbalimbali yaliyoko katika jamii jambo ambalo hata mtume aliwahi kulifanya.

“Mbona wapo waumini wa dini ya Kiislamu wanokwenda kutibiwa katika hospitali za misheni, lakini wanaendelelea na dini zao, halikadhalika wapo madaktari Waislamu wanaowatibu Wakristo,” alisema Sheikh Shaaban.

Aliwataka wananchi wasiangalie nani anatoa tiba bali ubora wa tiba hiyo kutokana na matatizo yanayowasumbua.

KKKT wafungua akaunti

Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) limeamua kufungua Akaunti katika Bank ya CRDB kwa ajili ya kupata fedha za kurekebisha miundombinu katika Kijiji cha Samunge, kilichopo Loliondo, wilayani Ngorongoro, mkoani Arusha.

Kwa mujibu wa Askofu Thomas Laizer wa Dayosisi ya Kaskazini, akaunti hiyo itahusika na kurekebisha miundombinu ya kufika kwa Mchungaji, Ambilikile Mwasapile. Hata hivyo, walisema akaunti hiyo haijafunguliwa wapo hatua za mwisho na wataitaja hivi karibuni.

Pia Askofu Laizer alisema akaunti hiyo itarekebisha maeneo ya kukaa watu bila shida na mahitaji mengine muhimu katika eneo hilo. Tayari wasanifu wako katika eneo hilo kuweka michoro na kurekebisha maeneo mbalimbali ambayo yanaitaji marekebisho.

Alisema Kanisa limetoa zaidi ya Sh milion 75 kwa ajili ya kuanza kazi hiyo: “Akaunti hiyo itachangiwa na mtu yeyote mwenye mapenzi mema ambaye anaona umuhimu wa watu wenye matatizo mbalimbali ya maradhi wanapata tiba kwa njia rahisi zaidi kuliko ilivyo hivi sasa ambapo wagonjwa wanapata shida ya kufika huko, pia pa kulala na hata eneo la kusubiria matibabu,” alisema Askofu Laizer.

Akimzungumzia Mchungaji Mwasapile, alisema alimfahamu siku nyingi akiwa fundi masoni katika
Wilaya ya Babati, mkoani Manyara na alianza kazi ya Uinjilisti mwaka 1980, ambapo alienda kusomea Uchungaji katika Misionari ya Oldonyo Sambu na kuhitimu Uchungaji miaka miwili baadae.

Baada ya kuhitimu Uchungaji alipangiwa kituo cha Bonga, wilayani Babati na Askofu Laizer ndiye aliyemsimika ambapo alikaa hapo miaka saba na ndipo ilipotokea shida ya Mchungaji wa kwenda katika maeneo ya Sonjo, wilayani Ngorongoro baada ya aliyekuwepo kustaafu na kila Mchungaji kukwepa kwenda huko.

“Unajua zamani kwenda Sonjo ni sawa na wafanyakazi wa Serikali wanavyokwepa kwenda vijijini, lakini baada ya kanisa kuliaona hilo tuliita mkutano wa wachungaji wote zaidi ya mia na kutaka mwenye moyo wa kwenda kufanya kazi katika maeneo hayo ajitokeze mwenyewe… na ndipo Mchungaji Mwaisapile alipojitokeza na kusema yeye yuko tayari kutumwa huko. Amefanya kazi yake vizuri mpaka amestaafu, lakini mpaka sasa analipwa mshahara na kanisa,” alisema Askofu
Laizer.

Akiwazungumzia baadhi ya viongozi wa makanisa ambao wanajaribu kutoa kashfa kuhusu Mchungaji
huyo akiwepo Askofu Zachary Kakobe, alisema viongozi hao wamezoea kuwanyan’ganya wanawake na wasichana mikufu na kutaka kujua pato la kila muumini ili kuwalazimisha kutoa fungu la kumi
ndio maana wanaona muda unafika wa watu kung’amua ukweli ni lazima wapige kelele.

Kijiji cha Samunge kipo karibu na Mji wa Loliondo na kuna umbali wa kilometa 300 ambapo zaidi ya nusu ya barabara ya kufika huko si nzuri na pia kutokana na wingi wa watu ambao wanakadiriwa zaidi ya 600 kwa siku wamekuwa katika hali ngumu ya kupata mahitaji ya kila siku.

Mbatia aitupia CCM kombora

KITENDO cha watu wengi kwenda kupewa tiba na Mchungaji (mstaafu) wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Ambilikile Masapile, kimeelezwa kuwa ni dalili ya Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kushindwa kuboresha huduma za afya.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia, alisema kitendo hicho ni ishara ya wazi kwamba Taifa halifikirii tena.

“Uwezo wa Taifa kufikiria umefikia mwisho, watu hawafikirii tena na matokeo yake wamekata tamaa. Hatua ya watu kukata tamaa ni hatari sana, na hii yote inatokana na huduma za afya kuwa mbovu.

“Ninachoweza kusema kuhusu tiba inayotolewa na yule Babu wa Loliondo ni kwamba asaidiwe na aendelee na matibabu yake, lakini kama Taifa tunatakiwa kuwa na umakini wa kufikiria na sasa hivi tunacheza na Watanzania, kwani akili zote za watu zimehamia Loliondo,” alisema Mbatia.

Kwa upande wake, Thomas Mongi ambaye ni Katibu wa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), alisema pamoja na kwamba tiba ya Mchungaji Masapile ni imani, lakini watu wanakimbilia huko kwa kuwa hawana imani na huduma zinazotolewa na hospitali za Serikali.

Mongi alitoa kauli hiyo kwa niaba ya Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Julius Mtatiro.

“Sisi hatuingizi tiba ya Loliondo katika siasa, lakini watu wanakimbilia kule kwa kuwa hawana imani tena na hospitali za Serikali, kwani wakati mwingine unaweza kwenda hospitali halafu ukaambiwa hata panadol hakuna.

“Tiba ya Liliondo ni ishara mojawapo ya matatizo makubwa yaliyopo katika sekta ya afya. Kutokana na hali hiyo, ndio maana wiki hii Profesa Lipumba ataanza ziara mikoani kuwaeleza wananchi namna Serikali yao waliyoichagua ilivyoshindwa kazi,” alisema Mongi.

source: gazeti la mtanzania